May 11, 2016 01:34 UTC
  • Jumatano, Mei 11, 2016

Leo ni Jumatano tarehe 4 Shaaban 1437 Hijria sawa na tarehe 11 Mei 2016.

Siku kama ya leo miaka 1411 iliyopita, yaani tarehe 4 Shaaban mwaka 26 Hijria, alizaliwa Abbas bin Ali bin Abi Talib mashuhuri kwa lakabu ya Abul Fadhl. Mama yake ni Ummul Baniina, ambaye aliolewa na Imam Ali (A.S) baada ya kufariki dunia bibi Fatima Zahra AS. Abbas alifahamika mno kutokana na elimu, ukweli na uchaji Mungu wake. Kutabahari kwake kielimu kuliwafanya watu wengi kurejea kwake kwa ajili ya kutatuliwa masuala mbalimbali ya kielimu. Alikuwa akimpenda sana kaka yake, yaani Imam Hussein (as) na alikuwa pamoja naye hadi alipouawa shahidi katika Medani ya Karbala.

******* 

Siku kama ya leo miaka 81 iliyopita kituo cha kwanza cha kurushia matangazo ya televisheni kwa jina la Nipkow kilianza kazi rasmi katika mji wa Berlin huko Ujerumani, hatua ambayo iliwawezesha watu kuanza kutumia runinga au televisheni. Kituo hicho cha kwanza cha matangazo ya televisheni kilipewa jina la Nipkow kwa shabaha ya kumuenzi Paul Gottlieb Nipkow ambaye alikuwa miongoni mwa wavumbuzi asili wa televisheni. Nipkow alivumbua njia ya kubadili picha na kuwa mawimbi na kisha kuyarejesha mawimbi hayo katika sura ya picha.

*******

Miaka 76 iliyopita katika siku kama ya leo, majeshi ya pamoja ya Ufaransa na Uingereza yaliwasili nchini Ubelgiji kwa ajili ya kuisaidia nchi hiyo iliyokuwa ikikabiliwa na uvamizi wa vikosi vya Ujerumani ya Kinazi. Hatua hiyo ya Ufaransa na Uingereza ya kuiunga mkono Ubelgiji ilikuwa ni kwa mujibu wa makubaliano yaliyokuwako baina yao. Licha ya kuweko muungano huo wa kijeshi, vikosi vya Ujerumani ya Kinazi mbali na kuyashinda majeshi ya Ubelgiji yalivishinda pia vikosi vya pamoja vya Uingereza na Ufaransa na kuikalia kwa mabavu ardhi yote ya nchi hiyo.

*******

Tarehe 11 Mai miaka 152 iliyopita alizaliwa Ethel Lilian Voynich mwandishi wa Kiingereza. Akiwa na umri wa miaka 21 Bi Lilian alielekea Russia na kusoma fasihi ya lugha ya Kirusi. Ni katika kipindi hicho ndipo alipoanza taratibu kuwa na shauku na fani ya uandishi na fasihi ya lugha. Bi Ethel Lilian aliaga dunia mwaka 1960.