Apr 02, 2021 22:04 UTC
  • Jumamosi, 3 Aprili, 2021

Leo ni Jumamosi tarehe 20 Shaaban 1442 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 3 Aprili 2021 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1057 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, Ibn Nadim mwanahistoria na mtaalamu wa masuala ya vitabu wa Kiislamu alifariki dunia. Umashuhuri wa mtafiti huyo unatokana zaidi na kitabu chake maarufu cha Al-Fihrist. Katika kitabu hicho Ibn Nadim amezitaja takriban elimu zote mashuhuri katika ustaarabu wa Kiislamu na kisha kufafanua maisha na historia ya wanazuoni maarufu katika elimu hizo. Kadhalika Ibn Nadim amevitaja humo vitabu na makala zilizoandikwa kuhusiana na elimu hizo. ***

Kitabu cha maarufu cha Al-Fihrist cha Ibn Nadim

 

Katika siku kama ya leo miaka 52 iliyopita, Zakir Hussein Rais Mwislamu wa India aliaga dunia. Zakir Husain alizaliwa 1897. Alisoma masomo yake ya juu katika Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Aligarh na baadaye kuhitimu masomo yake katika Chuo Kikuu cha Berlin nchini Ujerumani. Baada ya kuhitimu masomo kwa miaka mingi alijihusisha na harakati za kielimu na kisiasa. Mwaka 1962 akawa Makamu wa Rais wa India. Hatimaye mwaka 1967 alichaguliwa kuwa Rais kupitia uchaguzi. Zakir Husain alikuwa mpinzani mkubwa wa vitendo vya mabaرu vya Wahindu dhidi ya Waislamu na alikuwa akiafiki Pakistan kujitenga. ***

Zakir Husain

 

Katika siku kama ya leo miaka 109 iliyopita, aliaga dunia Mullah Muhammad Kashani akiwa na umri wa miaka 84. Mullah Muhammad Kashani alikuwa ameshikmana mno mna ibada na kumuabudu Mwenyezi Mungu kiasi cha kufumbia macho ladha zote za dunia. Walisoma kwake wasomi na wanazuoni wakubwa kama Ayatullahil Udhma Haj Agha Hussein Buroujerdi, Dhiyauddin Araqi, Sayyid Hassan Modarres na Mirza Hussein Naini. ***

Mullah Muhammad Kashani

 

Siku kama ya leo miaka 19 iliyopita, yaani sawa na tarehe 3 Aprili 2002, jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel lilianzisha mashambulizi makubwa katika mji wa Jenin ulioko Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, katika ardhi za Palestina. Mashambulio hayo yalikuwa mwendelezo wa mashambulizi ya wiki kadhaa ya Wazayuni kwenye eneo hilo, kwa shabaha ya kuzima Intifadha ya wananchi wa Palestina. Kwenye mashambulio hayo ya majeshi ya Wazayuni huko Jenin, asilimia 70 ya mji huo ilibomolewa kabisa, mamia ya Wapalestina kuuawa shahidi na watu wengine wasiopungua 5,000 kukosa makazi. ***

Jinai za utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Wapalestina hazina kikomo