May 15, 2016 05:46 UTC
  • Jumapili, Mei 15, 2016

Leo ni Jumapili tarehe Nane Shaban 1437 Hijria sawa na tarehe 15 Mei mwaka 2016 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 876 iliyopita, alizaliwa mjini Andalusia, Uhispania, Ibn Rumiyyah mtaalamu wa hadithi, mimea na tiba wa Kiislamu katika karne ya sita Hijiria. Baada ya masomo yake ya msingi, alijifunza taalumu ya hadithi kutoka kwa wasomi wakubwa wa elimu hiyo sanjari na kusomea pia elimu ya dini na masuala ya mimea. Awali Ibn Rumiyyah alifanya utafiti mkubwa katika masuala ya mimea na baada ya hapo akafanya safari maeneo tofauti kama vile Misri, Iraq na Hijazi na kuendeleza utafiti huo. Msomi huyo ameacha athari nyingi katika uga wa elimu ya sheria za Kiislamu na hadithi ambapo hata hivyo kwa bahati mbaya baadhi ya athari hizo zimepotea. 

Siku kama ya leo miaka 329 iliyopita, mwaka mmoja baada ya Austria kudhibiti sehemu ya ardhi za Hungary, Mfalme Leopold wa Kwanza wa nchi hiyo alitoa amri ya kuundwa mahakama maarufu kwa jina la Apri kwa ajili ya kuwahukumu wapigania uhuru wa nchi hiyo ya Hungary. Mahakama hiyo iliyofanya kazi kwa kipindi cha miezi sita, ilifanya kazi usiku na mchana ambapo ilitoa hukumu ya kunyongwa watu elfu nane kupitia mauaji ya umati au ya mtu mmoja mmoja.

Siku kama ya leo miaka 240 iliyopita, ilitengenezwa meli ya kwanza yenye kutumia mvuke. Meli inayotumia nishati ya mvuke ilitengenezwa miaka 70 baada ya kuvumbuliwa nishati ya mvuke na mhandisi wa Kifaransa Denis Papin. Utumiaji wa nishati ya mvuke katika meli ulileta mabadiliko makubwa katika sekta ya usafiri wa baharini.

Siku kama ya leo miaka 157 iliyopita mwafaka na tarehe 15 Mei 1859, alizaliwa Pierre Curie msomi na mwanafizikia wa Ufaransa. Kipaji cha masomo ya hesabati na fizikia alichokuwa nacho, kilianza kuonekana tokea ujana wake na hatimaye kuibuka na kuwa mtafiti mkubwa katika nyanja hizo. Mnamo mwaka 1898 mwanafizikia huyo wa Kifaransa alifanikiwa kugundua Radium akisaidiana na mkewe Bi. Marie Pierre. Pierre Curie aliaga dunia mwaka 1906.

Siku kama ya leo miaka 97 iliyopita, sawa na tarehe 15 Mei 1919 mji wa Izmir moja ya miji ya kihistoria na muhimu nchini Uturuki, ulitekwa na wanajeshi wa Mustafa Kamal Pasha au kwa jina mashuhuri la Ataturk, mwasisi wa Jamhuri ya Uturuki, baada ya kujiri mapigano yaliyopelekea kuuawa watu wengi. Izmir iko magharibi mwa Uturuki, na harakati ya Warepublican ya Uturuki ilianzia katika mji huo wa kihistoria.

Na siku kama ya leo miaka 76 iliyopita, jeshi la Ujerumani liliivamia na kuikalia kwa mabavu nchi ya Uholanzi baada ya shambulio kubwa lililodumu kwa siku 5 katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia. Wanajeshi wa Kinazi wa Ujerumani walianza kuzishambulia nchi za Ufaransa, Ubelgiji, Uholanzi na Luxemburg huko magharibi mwa Ujerumani tangu tarehe 10 Mei na kufanikiwa kuzidhibiti nchi zote hizo. Uholanzi ilijipatia uhuru mwaka 1945