Jumatatu, Mei 16, 2016
Leo ni Jumatatu tarehe 9 ya mwezi Shaaban 1437 Hijria sawa na tarehe 16 Mei mwaka 2016 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 19 iliyopita, Jenerali Mobutu Sese Seko rais na dikteta wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Zaire ya zamani, aliikimbia nchi hiyo baada ya vikosi vya majeshi ya waasi vilivyokuwa vikiongozwa na Laurent Kabila kukaribia mji wa Kinshasa. Mobutu alichukua madaraka ya nchi hiyo mnamo mwaka 1965 kwa mapinduzi ya kijeshi na kisha kutawala kwa muda wa miaka 32. Licha ya kiongozi huyo kuwa dikteta asiye na huruma, lakini alikuwa akiungwa mkono na madola ya Magharibi hasa Marekani na Ufaransa. Kutokana na Congo DR kuwa katika eneo nyeti na muhimu kijiografia katikati mwa bara la Afrika na utajiri mkubwa wa madini na almasi, imekuwa ikizingatiwa na kumezewa mate na nchi za Magharibi. Siku moja baada ya Mobutu kuikimbia nchi hiyo, vikosi vya waasi viliuteka mji wa Kinshasa na kiongozi wao yaani Laurent Kabila, akashika hatamu za uongozi wa nchi. ***
Miaka 28 iliyopita katika siku kama ya lro, Jeshi Jekundu la Umoja wa Kisovieti lilianza kuondoka nchini Afghanistan. Baada ya Nur Muhammad Taraki kupinduliwa, serikali ya kwanza ya kikomunsti iliyokuwa ikipata himaya ya moja kwa moja ya Urusi ya zamani ikaanzishwa nchini Afghanistan. Utawala wa Taraki uliondolewa madarakani mwanzoni mwa mwaka 1979 kwa mapinduzi mengine yaliyoongozwa na Hafidhullah Amin mmoja wa watu wake wa karibu. Lakini Warusi waliingiwa na mtazamo mbaya na Hafidhullah ambaye alikuwa akitaka kujirubisha kwa Marekani na kuleta uhusiano wenye uwiano kati ya Afghanistan na Mashariki na Magharibi na hivyo wakaipindua serikali yake ***
Katika siku kama ya leo miaka 514 iliyopita, ardhi ya Honduras inayopatikana leo huko Amerika Kusini iliunganishwa na makoloni ya Muhispania. Kabla ya hapo Honduras ilikuwa kituo cha utamaduni wa kaumu ya Maya. Hata hivyo baada ya Honduras kuvamiwa na kukaliwa kwa mabavu na Uhispania, kabila hilo liliangamizwa na kupotea. Mwanzoni mwa karne ya 19 Miladia na kutokana na kuvurugika hali ya ndani ya Uhispania, Honduras kama ilivyokuwa kwa makoloni mengine, ilitumia fursa hiyo kuweza kujipatia uhuru wake. ***
Siku kama ya leo miaka 860 iliyopita, aliaga dunia Abul Barakaat Abdul Rahman bin Muhammad mashuhuri kwa jina la Ibn Anbari fakihi na mtaalamu wa lugha wac mjini Baghdad. Alihitimu masomo yake katika shule ya Nidhamiyah na kutokana na kupata alama nzuri na kuwa na maalumati mengi alianza kufunduisha katika shukle hiyo hiyo. Abul Barakaat ambaye ni fakihi mkubwa na mwenye daraja ya juu ameacha athari nyingi za vitabu na makala katika nyunga mbalimbali. Asrar al-Arabia ni moja ya athari zake ambazo tunaweza kuziashria hapa. ***
Na katika siku kama ya leo miaka 956 iliyopita, aliaga dunia Ibn Barraj mmoja wa mafaqihi na maulamaa mashuhuri wa Misri. Ibn Barraj alifahamika sana kwa jina la Trablosi kutokana na kuwa kwa muda fulani alikuwa na cheo cha kadhi katika mji wa Trablos yaani Tripoli huko kaskazini mwa Lebanon ya sasa. Msomi huyo wa Kiislamu alifunzwa na maulamaa kama vile Sayyid Murtadha na Sheikh Tusi. Ibn Barraj ni msomi mtajika wa Kiislamu ambaye fikra na mitazamo yake ilikuwa ikiheshimiwa na mafaqihi wakubwa wa zama hizo.