Jumapili tarehe 4 Julai 2021
Leo ni Jumapili tarehe 23 Dhulqaada 1442 Hijria Qamariya inayosadifiana na 13 Tir mwaka 1400 Hijria Shamsiya sawa na Julai 4 mwaka 2021
Siku kama ya leo miaka 245 iliyopita, yaani tarehe 4 Julai mwaka 1776 Miladia, wawakilishi wa majimbo 13 ya awali ya Marekani walisaini "Tangazo la Uhuru" wa nchi hiyo katika mji wa Philadelphia. Ardhi ya Marekani kwa maelfu ya miaka ilikuwa makazi ya Wahindi Wekundu. Mwishoni mwa karne ya 15 Miladia wavumbuzi wa Ulaya waliwasili Marekani na nchi mbalimbali za Ulaya zikavamia na kukalia kwa mabavu kila eneo la Marekani. Wazungu hao wa Ulaya waliandamana na mamilioni ya watumwa kutoka Afrika ambao walitumiwa katika kazi ngumu za mashambani na viwandani.
Miaka 74 iliyopita katika siku kama ya leo, visiwa vya Ufilipino vilijitangazia uhuru wake kutoka kwa Marekani. Fernando Magellan mvumbuzi wa Kireno pamoja na wenzake ndio waliokuwa Wazungu wa kwanza kutoka Ulaya kuwasili katika ardhi ya Ufilipino na hiyo ilikuwa mwaka 1521. Katika kipindi cha nusu karne baadaye, Uhispania ikawa imeidhibiti ardhi yote ya nchi hiyo. Mkoloni Muhispania alipora mali na utajiri wa Ufilipino kwa muda wa karne tatu.
Katika siku kama ya leo miaka 11 iliyopita, Ayatullah Sayyid Muhammad Hussein Fadhlullah mmoja wa maulama mashuhuri na marja taqlidi wa Kiislamu alifariki dunia. Allama Fadhlullah alizaliwa mwaka 1935 katika mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq katika familia ya kidini yenye asili ya Lebanon. Allama Fadhlullah alianza kujifunza elimu ya dini katika Chuo Kikuu cha Kidini (Hawza) cha mji wa Najaf Iraq akiwa bado kijana mdogo. Alijishughulisha na uandishi wa makala na vitabu na alikuwa na alikuwa mshairi. Ayatullah Fadhlullah alikuwa miongoni mwa waungaji mkono wakubwa wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Lebanon Hizbullah na jambo hilo liliikasirisha sana Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel ambazo zilifanya majaribio kadhaa ya kutaka kumuua. Ayatullah Muhammad Hussein Fadhlullah ameandika vitabu vingi vya thamani ikiwemo tafsiri ya Qur'ani ya "Min Wahyil Qur'an."
Siku kama ya leo miaka 50 iliyopita yaani 13 Tir mwaka 1350 Hijria Shamsiya alifariki dunia mwalimu mkubwa wa fasihi wa Iran Dakta Muhammad Muin baada ya kufanya juhudi kubwa za miaka mingi katika nyanja za utamaduni na mila za Kifarsi. Dakta Muin alizaliwa katika mji wa Rasht kaskazini mwa Iran. Alijifunza fasihi ya Kiarabu ujanani na baada ya kukamilisha masomo yake katika skuli ya Darul-Funun alielekea katika Chuo Kikuu cha Tehran na kujiunga na masomo katika kitengo cha fasihi na falsafa. Mwaka 1321 Hijria Shamsiya Ustadh Muin alianza kufanya kazi ya kufundisha na utafiti katika Chuo Kikuu cha Tehran akiwa mhitimu wa kwanza wa shahada ya udaktari wa lugha na fasihi ya Kifarsi