May 18, 2016 23:50 UTC
  • Alkhamisi, Mei 19, 2016

Leo ni Alkhamisi tarehe 12 Shaaban mwaka 1437 Hijria sawa na tarehe 19 Mei mwaka 2016 Miladia.


Siku kama ya leo miaka 495 iliyopita, wapiganaji wa utawala wa kifalme wa Othmania waliuteka mji muhimu wa Balkan mji mkuu wa Yugoslavia katika rasi ya Balkan. Utawala wa Othmania ulianza kusonga mbele katika eneo la Balkan kuanzia mwishoni mwa karne ya 14 Miladia na kuweka chini ya himaya yake karibu eneo lote hilo. Lakini kutokana na udhaifu uliojitokeza kwenye utawala huo, hadi mwanzoni mwa karne ya 20 taratibu maeneo mengi ya Balkan yakawa huru. ***


Miaka 254 iliyopita katika siku kama ya leo alizaliwa Johann Gottlieb Fichte mwanafalsafa wa Kijerumani. Fichte alizaliwa katika familia maskini. Johann alikuwa mmoja wa waasisi wakuu wa harakati ya kifalsafa iliyojulikana kama "German idealism", ambayo ilitokana na maandiko ya kinadharia na kimaadili ya rafiki yake Immanuel Kant. Johann Fitche ameandika vitabu vingi muhimu ambapo baadhi yake ni "Foundations of Natural Right, The Vocation of Man na The Way Towards the Blessed Life. ***


Miaka 91 iliyopita, alizaliwa Malcolm X, kiongozi wa harakati ya Wamarekani Weusi. Malcolm X ambaye jina lake la asili ni Malik Shabazz alizaliwa katika familia masikini. Alipofikisha umri wa miaka 4 nyumba ya wazazi wake ilichomwa moto na kundi la kibaguzi la Ku-Klux-Klan. Alilazimika kuacha masomo yake akiwa na miaka 15 kutokana na umasikini. Akiwa katika rika la ujana, Malcolm X alifahamiana na makundi ya vijana wa Kiislamu na hatimaye kusilimu. Itikadi ya mwanaharakati huyo wa Kiislamu iliwachukiza watawala wa Marekani na makundi ya ubaguzi wa rangi nchini Marekani. Malcolm X aliuawa wakati akihutubia akiwa mkutanoni. Alikuwa akisisitiza mara kwa mara kuwa, Wamarekani weusi ambao wanakandamiza na kubaguliwa na serikali ya Marekani wanaweza kujipatia uhuru na uadilifu chini ya mwamvuli wa utawala wa Kiislamu.***


Katika siku kama ya leo miaka 81 iliyopita, alifariki dunia katika ajali ya gari, mwanasiasa na afisa wa ujasusi wa Uingereza Thomas Edward Lawrence. Lawrence alizaliwa mwaka 1888 Miladia. Mwanasiasa huyo wa Uingereza alihudumu pia huko Iraq, Syria na Palestina, huku akiwa mtaalamu wa masuala ya akiolojia (elimu ya kale) katika kipindi cha miaka kati ya 1910 hadi 1914. Aidha alikuwa mfanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza na mwaka 1916 aliteuliwa kuwa mkuu wa idara ya ujasusi ya jeshi la Uingereza nchini Misri.***


Na miaka 80 iliyopita katika siku kama ya leo, rada ilivumbuliwa na Robert Watson Watt mvumbuzi wa Kiingereza. Kifaa hicho ambacho ni muhimu kinachotumiwa katika ugunduzi na utambuzi kwenye oparesheni mbalimbali za kijeshi na kiraia, kwa mara ya kwanza kilitumika katika moja ya viwanja vya ndege vya Uingereza. Rada ilihesabiwa kama chombo muhimu cha kutoa tahadhari katika Vita vya Pili vya Dunia na hivi sasa kinatumika katika masuala mbalimbali. ***