Oct 09, 2021 02:36 UTC
  • Jumamosi, 09 Oktoba, 2021

Leo ni Jumamosi tarehe Pili Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1443 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 9 Oktoba 2021.

Siku kama ya leo miaka 813 iliyopita, aliaga dunia Ibn Athir Jazari, mwanahistoria, mtaalamu wa fasihi na mpokezi mkubwa wa hadithi. Ibn Athir alizaliwa mwaka 555 Hijria huko Iraq na kujifunza taaluma mbalimbali. Alipata umashuhuri katika masuala ya lugha na fasihi ya Kiarabu. Kitabu maarufu zaidi cha Ibn Athir ni al Kamil fi Tarikh. Kitabu kingine cha mwanazuoni huyo mkubwa wa Kiislamu ni Usdul Ghabah Fi Ma'rifatis Swahabah ambacho kinaeleza wasifu wa masahaba 7500 wa Mtume Muhammad (saw). ***

Ibn Athir Jazari,

 

Siku kama ya leo miaka 59 iliyopita, mwafaka na tarehe 9 Oktoba 1962, nchi ya Uganda iliyo Afrika Mashariki ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza. Kuanzia mwaka 1890 Uganda ilikuwa nchini ya makampuni ya Kiingereza yaliyokuwepo Afrika Mashariki, na baada ya kupita miaka kadhaa, ikatawaliwa rasmi na Uingereza. Baada ya kutawaliwa na mkoloni Mwingereza, wananchi wa Uganda walipigania uhuru na hatimaye kufanikiwa kujipatia uhuru wao mwaka 1962 katika siku kama ya leo. ***

Bendera ya Uganda

 

Miaka 54 iliyopita katika siku kama ya leo, aliuawa Ernesto Che Guevara mwanamapinduzi mashuhuri wa Amerika ya Latini pamoja na wenzake kadhaa. Che Guevara alizaliwa mwaka 1928 nchini Argentina. Fikra ya Ernesto Che Guevara ya kuendesha mapambano dhidi ya ubepari ilizidi kupanuka baada ya kushuhudiwa umaskini na ubaguzi uliotokana na siasa za kipebari za Marekani za kuyanyonya mataifa ya Amerika ya Latini. Ernesto che Guevara alifahamiana na Fidel Castro huko Mexico na viongozi hao wawili ndio walioongoza mapinduzi ya Cuba hadi kupatikana ushindi. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Cuba mwaka 1959, Che Guevara alielekea Bolivia na kuasisi kundi la wapiganaji wa msituni. Alianza kupambana na serikali ya nchi hiyo iliyokuwa tegemezi kwa Marekani. Lakini katika siku kama ya leo mwaka 1967, wanajeshi wa Bolivia wakisaidiwa na shirika la ujasusi la CIA waligundua maficho ya Che Guevara na kumuuwa kwa kummiminia risasi. ***

Ernesto Che Guevara

 

Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita, Majid Abu Sharar, shakhsiya mwingine wa Palestina aliuawa na utawala haramu wa Israel nchini Italia. Abu Sharar ambaye alikuwa afisa wa kampeni wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO aliuawa na vibaraka wa shirika la ujasusi la utawala wa Kizayuni wa Israel Mosad mjini Roma, Italia. Israel imekuwa ikitumia njia ya kuwauwa kigaidi shakhsiya mbalimbali wa Palestina kama moja ya njia zake kuu za kusitisha mapambano ya ukombozi ya Wapalestina. ***

Majid Abu Sharar,

 

Leo tarehe 9 Oktoba ni Siku ya Kimataifa ya Posta. Posta ndio chombo cha kale zaidi na kikubwa cha mawasiliano baina ya wanadamu wa nchi na maeneo mbalimbali ya dunia. Taasisi hiyo ya posta ni miongoni mwa asasi za kijamii zilizobakia hai hadi leo. Kutumiana ujumbe na barua ni miongoni mwa haja za kijamii za wanadamu tangu kiumbe huyo alipoanza maisha ya kijamii na posta ndiyo iliyokuwa chombo cha kukidhi mahitaji hayo kwa minghi mingi. ***

Siku ya Kimataifa ya Posta

 

Tags