May 22, 2016 23:12 UTC
  • Jumatatu,23 Mei 2016

Leo ni Jumatatu 16 Shaaban mwaka 1437 Hijria sawa na tarehe 23 Mei mwaka 2016 Miladia.


Katika siku kama ya leo miaka 398 iliyopita, Waprotestanti wa Czeck ambao walikuwa wakilalamikia mbinyo mkubwa wa uhuru wao uliokuwa ukifanywa na Mfalme Ferdinand wa Pili wa Rome, walichukua uamuzi wa kuwauwa wajumbe wawili wa mfalme huyo, na kusababisha kuanza vita vya kidini vilivyochukua muda wa miaka 30. Katika vita hivyo, nchi za Ufaransa, Sweden na Denmark zilikuwa zikiwaunga mkono Waprotestanti, huku Wahispania na Ufalme wa Rome wakiwaunga mkono Wakatoliki kwenye vita hivyo. Vita hivyo licha ya kuleta maafa na uharibifu mkubwa na kupelekea kugawanyika Ujerumani, viliudhoofisha utawala wa mfalme wa Rome na kwa upande wa pili Ufaransa kuzidi kujipatia nguvu za kijeshi.


Siku kama ya leo miaka 71 iliyopita, alijiua Heinrich Himmler Mkuu wa zamani wa Shirika la Kijasusi na Usalama la Ujerumani ya Kinazi (Gestapo). Himmler alizaliwa mwaka 1900 na alipofikisha umri wa miaka 34 aliweza kupanda cheo na kuwa mkuu wa shirika hilo la kijasusi na usalama la Ujerumani. Heinrich Himmler anahesabiwa kuwa mmoja kati ya viongozi makatili na aliyeongoza operesheni kadhaa za mateso na kuuwa watu nchini humo. Himmler alitiwa mbaroni baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na kuhukumiwa adhabu ya kifo kwenye mahakama ya Nuremberg nchini Ujerumani, lakini kabla ya kutekelezwa hukumu hiyo aliamua kujiua mwenyewe baada ya kunywa sumu aina ya sianidi.


Miaka 110 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Henrik Ibsen mwandishi wa tamthiliya wa nchini Norway. Alizaliwa mwaka 1828 kusini mwa Norway. Shauku na mapenzi ya Ibsen ya kuwa mwandishi wa tamthiliya ndiyo yaliyomsukuma kwenye taaluma hiyo. Mwandishi huyo wa Kinorway ameandika drama na tamthiliya nyingi. Moja kati ya tamthmliya zake mashuhuri ni ile iitwayo, An Enemy of the People yaani Adui wa Watu. ***


Na siku kama ya leo miaka 34 kulingana na kalenda ya Hijria Shamsia, mji wa Khorramshahr wa Iran ulikombolewa na wapiganaji wa Kiislamu na ukaondoka katika uvamizi wa majeshi vamizi ya Iraq. Mji wa Khorramshahr uko katika mkoa wa Khozestan kusini magharibi mwa Iran. Mji huo ulikuwa chini ya uvamizi wa majeshi ya Iraq kwa muda wa karibu miezi 20. Uvamizi dhidi ya mji huo ulijiri mwanzoni mwa vita vya miaka minane vya kulazimishwa Iran vilivyoanzishwa na utawala wa dikteta Saddam Hussein.