Jumatatu tarehe 22 Novemba 2021
Leo ni tarehe 16 Rabiuthani 2021 Hijria sawa na tarehe 22 Novemba 2021.
Siku kama ya leo miaka 978 iliyopita alifariki dunia Abdulkarim ibn Hawazin al-Qushayri, maarufu kwa jina la Zainul-Islam, faqihi na mmoja wa maulama wakubwa wa Kiislamu. Alizaliwa mwaka 376 Hijiria eneo Quchan, kaskazini mashariki mwa Iran na baadaye alielekea Nishapur kwa ajili ya kutafuta elimu. baadaye alikwenda Makkah na Baghdad, Iraq kwa ajili ya kujiendeleza kielimu. Al-Qushayri alikuwa hodari katika elimu ya sharia za Kiislamu (fiqhi), teolojia, tafsiri ya Qur'ani na Hadithi, na miongoni mwa magwiji wa kisufi. Ameacha vitabu kadhaa, maarufu zaidi kikiwa ni "Al Risaalatul-Qushayriyyah', 'Al-Tayssir fi al Tafsir' na 'Latwaaiful-Ishaaraat.'
Siku kama ya leo miaka 202 iliyopita, alizaliwa Bi. Mary Ann Evans maarufu kwa jina la George Eliot, mwandishi wa riwaya na simulizi wa Uingereza. Akiwa mtoto mdogo, Evans alipendelea zaidi kusoma vitabu, na taratibu akaingia katika fani ya uandishi. Evans alikuwa na misimamo mikali ya dini ya Kikristo akiwa bado kijana. Hata hivyo misimamo hiyo ilipungua baadaye. Akiwa na umri wa miaka 30, Ann Evans alifasiri kitabu cha ‘Maisha ya Nabii Issa (as)’ (The Life of Jesus) kilichoandikwa na David Friedrich Strauss. Riwaya za Eliot zinahesabiwa kuwa miongoni wa vitabu maarufu zaidi vya karne ya 19 nchini Uingereza.
Siku kama ya leo miaka 78 iliyopita, kufuatia kujiri kwa Vita vya Pili vya Dunia, nchi ya Lebanon ilijipatia uhuru wake. Lebanon ilitoka katika udhibiti wa utawala wa Othmania mnamo mwaka 1918 Miladia na kudhibitiwa baadaye na Ufaransa. Mwaka 1923 Miladia Ufaransa iliikalia nchi hiyo kwa idhini ya Umoja wa Mataifa. Tangu wakati huo Lebanon ikaanza kushuhudia siasa za ukoloni wa Mfaransa vikiwemo vitendo vya ubaguzi na machafuko. Nchi hiyo ilijipatia uhuru wake mwaka 1943.
Katika siku kama ya leo miaka 58 iliyopita, John F. Kennedy, rais wa wakati huo wa Marekani aliuawa na raia mmoja wa nchi hiyo akiwa ziarani katika mji wa Dallas huko katika jimbo la Texas. Kennedy alizaliwa mwaka 1917 na alikuwa mwakilishi wa bunge la Marekani kwa duru tatu kuanzia mwaka 1946 na duru moja alikuwa mwakilishi wa seneti ya nchi hiyo. Siku kadhaa baadaye Lee Harvey Oswald ambaye alimuua Kennedy naye pia aliuawa na mtu aliyejulikana kwa jina la Jack Ruby na polisi ya Marekani ilidai kuwa mtu huyo vilevile aliaga dunia baadaye akiwa jela kutokana na maradhi ya saratani.
Siku kama ya leo miaka 54 iliyopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio nambari 242 kuhusu Palestina. Miongoni mwa vipengee vya azimio hilo ni udharura wa kuondoka askari wa utawala ghasibu wa Israel katika ardhi zote za Palestina zilizokaliwa kwa mabavu Juni mwaka 1967 katika vita vya Waarabu na Israel, kusimamishwa operesheni za kijeshi na kutatuliwa kadhia ya wakimbizi wa Palestina kwa njia ya uadilifu. Hata hivyo kutokana na himaya ya pande zote ya Marekani na nchi za Magharibi kwa utawala ghasibu wa Israel, utawala huo haramu umekataa kutekeleza azimio hilo.