May 25, 2016 09:51 UTC
  • Usekulari Katika Mizani ya Uislamu (21)

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki, ambacho lengo lake ni kuuchambua Usekulari kwa kutumia mizani ya mafundisho ya Uislamu ili kuweza kuelewa kasoro, dosari na udhaifu wa fikra na nadharia hiyo ambayo chimbuko lake ni Ulimwengu wa Magharibi. Ni mategemeo yangu kuwa mtanufaika na kuelimika na yale mtakayoyasikia katika kipindi hiki. Endeleeni kuwa pamoja nami basi kuitegea sikio sehemu hii ya 21 ya mfululizo huu.

Bila ya shaka wasikilizaji wa kawaida wa kipindi hiki mngali mnakumbuka kuwa baada ya kujadili katika vipindi kadhaa sababu za kujitokeza nadharia ya Usekulari katika Ulimwengu wa Magharibi pamoja na uhakiki wa ukosoaji kuhusu misingi ya kifikra ya nadharia hiyo kwa mtazamo wa Uislamu, tulichambua na kuifanyia ukosoaji pia maudhui ya 'Haki za Kimaumbile' ukiwa mmoja wa misingi ya haki za binadamu za Usekulari. "Haki za Binadamu" kwa maana inayotiliwa mkazo leo hii na Magharibi zina mafungamano makubwa na ya karibu na nadharia ya Usekulari. Wanafikra wengi, wakiwemo wanafikra Waislamu wamezungumzia maudhui ya haki za binadamu, wakaichambua na kuifanyia uhakiki wa kiukosoaji katika sura tofauti. Tofauti iliyopo baina ya haki za binadamu za Kisekulari na haki za binadamu za Kiislamu ni miongoni mwa masuala yanayojadiliwa katika uga huu. Na hiyo ndiyo maudhui ya kipindi chetu cha leo.

Baada ya mauaji na anuai za jinai zilizofanywa katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, nchi nyingi zilijiwa na wazo na hatimaye kuchukua hatua ya kuunda Umoja wa Mataifa. Kutungwa na kupitishwa Tangazo la Dunia la Haki za Binadamu mnamo mwaka 1948, yalikuwa moja ya mafanikio ya umoja huo, tangazo ambalo limezungumzia ndani yake aina kadhaa za uhuru wa mtu binafsi, usawa na heshima ya wanadamu. Japokuwa tangazo hilo lilitilia mkazo baadhi ya haki zisizo na shaka wala mjadala za mwanadamu na kuwafanya baadhi ya watu duniani waweze kuishi kwa raha na ustawi wa kiwango fulani, lakini wanafikra mbalimbali wanaamini kuwa katika Tangazo la Dunia la Haki za Binadamu kuna migongano na kasoro za msingi na kwamba tangazo hilo halikuzingatia na kufikiria kwa makini mahitaji na haki halisi za mtu. Na kwa sababu hiyo hatuwezi kuwa na mategemeo na matarajio ya tangazo hilo kutekelezwa katika nchi zote kwa ujumla wake na bila ya pingamizi wala masharti yoyote. Zaidi ya hayo kwa mtazamo wa wanafikra wengi Waislamu Tangazo la Dunia la Haki za Binadamu haliendani na mafundisho ya Kiislamu. Hapa ndipo linapokuja suali, nini hasa chanzo cha hitilafu kuhusu haki za binadamu?

Ukweli ni kwamba wanafikra katika uga wa siasa na falsafa wanakiri kuwa msingi wa Tangazo la Dunia la Haki za Binadamu ulijengwa juu ya sifa maalumu za utamaduni wa Magharibi yaani Usekulari (Secularism) na Umwanadamu (Humanism). Japokuwa haki za binadamu kwa maana ya haki za msingi na za awali kabisa, ambazo zinawashirikisha wanadamu wote kutokana na sifa moja inayowaunganisha ya ubinadamu, zina maana jumuishi na ya jumla ambayo kila mtu mwenye fikra huru anakubaliana nayo, lakini ukweli ni kwamba msingi na chimbuko la Tangazo la Dunia la Haki za Binadamu lililopitishwa na Umoja wa Mataifa ni fikra zilezile za Ubinafsi (Individualism), Umwanadamu na Usekulari zilizopata nguvu na kutawala katika Ulimwengu wa Magharibi baada ya kipindi cha Mvuvumko mkubwa wa Sanaa na Maarifa, kwa kimombo Renaissance. Fikra ambazo hazikosolewi katika Ulimwengu wa Kiislamu tu, bali zina wakosoaji wengi pia miongoni mwa wanafikra wa Ulimwengu wa Magharibi.

Bila ya shaka wapenzi wasikilizaji mngali mnakumbuka kuwa katika baadhi ya vipindi vyetu vilivyopita tuliwahi kuzungumzia kwa muhtasari upembuzi wa kiukosoaji wa Uislamu juu ya Umwanadamu na Ubinafsi. Tunachokusudia kufanya katika kipindi chetu cha leo ni kuonesha ni vipi haki za binadamu za Magharibi zilivyojengeka juu ya misingi ya Umwanadamu na Usekulari. Aidha tunataka kuzungumzia kwa muhtasari tofauti za kimsingi baina ya haki za binadamu za Kiislamu na haki za binadamu za Kisekulari.

Haki za binadamu zimeelezwa kwa tafsiri na maana ifuatayo:"Haki za binadamu maana yake ni fursa jumla ambazo kila mtu anazo kutokana na maumbile yake ya ubinadamu". Kama tutataka kutoa maana na tafsiri ya kidini kuhusu haki za binadamu itapasa tuseme:" haki za binadamu ni haki chache ambazo Mwenyezi Mungu amempa mwanadamu kutokana na kuwa kwake mwanadamu bila kujali rangi yake, asili yake, lugha na utaifa wake, eneo la kijiografia alipo, mazingira na hali yake inayobadilika ya kijamii au kiwango cha uwezo wa kipekee na ustahiki wake wa binafsi." Kwa mintaarafu ya hayo, haki za binadamu ni hidaya itokayo kwa Mungu, wala hakuna mwanadamu yeyote mwenye mamlaka ya kujipa uwezo wa kumpa au kumnyima mtu haki hizo. Kwa hivyo waliosaini na kupitisha Tangazo la Dunia la Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa, sio waliobuni na kuanzisha haki hizo, bali wao walijaribu kwa njia bora zaidi, na kulingana na kiwango cha elimu yao kuhusu mwanadamu na maumbile yake kupambanua baadhi ya haki za dhati ya mwanadamu na kuwataka walimwengu wazichunge na kuziheshimu.

Inavyoonesha, katika kubainisha suala la haki za binadamu suali muhimu la kujiuliza ni utu hasa ni nini, na je watu wako sawa katika hali ipi ya utu? Uko katika dhahiri ya utu; yaani kiumbe cha miguu miwili chenye sifa na tabia maalumu, au katika hakika halisi ya utu? Na hakika halisi ya utu ni kitu gani? Mwanafalsafa Thomas Hobes yeye amesema:"Mwanadamu ni mbwa mwitu kwa mwanadamu mwenzake". Naye mwanafalsafa mwengine Baruch Spinoza, amesema:"Mwanadamu ni Mungu wa mwanadamu".

Kutokana na hayo inatubidi tujue kwanza kiuhakika, mwanadamu ni kiumbe wa aina gani, ndipo tuelewe ana haki na wajibu gani. Bila ya kuwepo msingi sahihi wa kifalsafa na kiakili haiwezekani kudai kwamba mwanadamu ni kiumbe mwenye asili na hadhi na ni mbora kuliko mnyama; na haiwezekani pia kuthibitisha kwamba mwanadamu anapasa kuheshimiwa katika ulimwengu huu, na ana haki ya kuvitumia vilivyomo katika ulimwengu wa maumbile kwa manufaa yake. Kwa maana hiyo haiwezekani kuwa na utambuzi sahihi wa haki za binadamu pasi na kuwa na mitazamo na tafsiri maalumu juu ya utambuzi wa mambo, utambuzi juu ya ulimwengu na utambuzi juu ya mwanadamu.

Katika kubainisha mitazamo hii, mojawapo ya tofauti muhimu zaidi na ya msingi kati ya haki za binadamu za Kiislamu na Tangazo la Dunia la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa ni kwamba tangazo hilo linamchukulia mwanadamu kuwa ni kiumbe wa kimaada tu anayeanzia wakati wa kuzaliwa na kuishia wakati wa kufa. Kwa hakika moja ya nukta za msingi za Usekulari ni huko kupuuza kwake uhusiano wa mwanadamu na asili yake na marejeo yake. Kifungu cha kwanza cha Tangazo la Dunia la Haki za Binadamu kinasema:"Wanadamu wote wanazaliwa wakiwa huru na wako sawa kwa mtazamo wa hadhi na haki". Kabla ya tangazo hilo, katika matangazo na taarifa za nchi tofauti kuhusu haki za mwandamu ilikuwa ikielezwa hivi:"Mwanadamu ameumbwa akiwa ni kiumbe huru". Kwa maneno mengine, ilikuwa ikithibitishwa kuwa mwanadamu ameumbwa na kuna uhusiano baina yake na muumba wa ulimwengu; lakini katika Tangazo la Haki za Binadamu, kama inavyoonekana, imezungumziwa "kuzaliwa" badala ya"kuumbwa". Hakika ni kwamba suala la kuumbwa mwanadamu na Mwenyezi Mungu halikutajwa ili uhusiano wa mtu na Mungu usiwe na nafasi katika haki za binadamu. 

Wapenzi wasikilizaji, muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki umefikia tamati. Hivyo sina budi kuishia hapa kwa leo hadi tutakapokutana tena wiki ijayo inshaallah katika siku na saa kama ya leo. Basi hadi wakati huo nakuageni huku nikikutakieni heri na fanaka maishani…/


Tags