Jumatatu tarehe 20 Disemba 2021
Leo ni Jumatatu tarehe 15 Jamadil Awwal 1443 Hijria sawa Disemba 20 mwaka 2021.
Siku kama ya leo miaka 1405 iliyopita kwa mujibu wa baadhi ya nukuu za historia, alizaliwa Imam Ali bin Hussein (AS) maarufu kwa laqabu ya Zainul Abidin katika mji mtakatifu wa Madina. Mtukufu huyo ni mwana wa Imam Hussein bin Ali Bin Abi Twalib, mjukuu wa Bwana wetu Muhammad (SAW). Alikuwa kinara wa elimu, uchamungu, wema, ukarimu na upendo. Miongoni mwa sifa kuu za Imam Zainul Abidin ni kufanya ibada na kusali Swala za usiku. Alikuwa mwingi wa ibada na alipewa laqabu ya Sajjad kwa maana ya mwenye kusujudu sana na Zainul Abidin kwa maana ya 'Pambo la Wafanya Ibada' kutokana na sijda zake ndefu katika Swala. Imam Zainul Abidin alichukua jukumu la kuendeleza ujumbe wa mapambano ya Imam Hussein ya kupambana na ufisadi na dhulma ya watawala wa Bani Umayyah baada ya kuuawa baba yake katika medani ya Karbala. Aliishi miaka 35 baada ya tukio hilo chungu na aliuawa shahidi na mtawala wa Bani Ummayah Hisham bin Abdul Malik. Athari maarufu zaidi ya mtukufu huyo ni kitabu cha dua na miongozo ya Kiislamu cha al Sahifa as Sajjadiyya.

Tarehe 15 Jamadil Awwal mwaka 38 Hijria, yaani miaka 1405 iliyopita aliuawa shahidi Muhammad bin Abu Bakr ambaye alikuwa miongoni mwa maswahaba waaminifu wa Imam Ali bin Abi Twalib (as) na kamanda maarufu wa jeshi la Uislamu katika vita dhidi ya jeshi la Muawiya lililokuwa likiongozwa na Amr bin al As. Mtawala wa kizazi cha Banii Umayyah, Muawiya alituma jeshi la wapiganaji elfu sita nchini Misri kwa ajili ya kupigana na jeshi la Muhammad bin Abu Bakr lililokuwa na wapiganaji elfu mbili. Jeshi la Muhammad bin Abu Bakr lilishindwa katika vita hivyo na kiongozi huyo akauawa shahidi kwa kuchomwa moto baada ya kukamatwa mateka.

Siku kama ya leo miaka 142 iliyopita toleo la kwanza la gazeti la al Uruwatul Wuthqaa lilichapishwa chini ya uongozi wa Sayyid Jamaluddin Asadabadi maarufu kwa jina la Jamaluddin Afghani na Sheikh Muhammad Abduh mjini Paris, Ufaransa. Sayyid Jamaluddin aliasisi Jumuiya ya al Uruwatul Wuthqaa kwa shabaha ya kutimiza lengo lake la kujenga umoja na mshikamano kati ya mataifa ya Kiislamu na akaanza kuchapisha gazeti kwa kutumia jina hilo hilo.
Gazeti hilo lilisimamishwa mwezi Dhilhija mwaka huo huo baada ya kuchapishwa kwa kipindi cha miezi kadhaa tu katika nchi za Ulaya, India, Misri, Iran na katika nchi kadhaa za Kiarabu kutokana na mashinikizo ya kisiasa ya baadhi ya nchi.

Siku kama ya leo miaka 101 iliyopita aliaga dunia alimu na mwanazuoni Mulla Fat'hullah Gharawi Isfahani aliyejulikana kwa jina la Sheikhu Shari'a Isfahani. Alizaliwa mwaka 1228 Hijria Shamsia huko Isfahan katikati mwa Iran na kupata elimu ya dini katika mji huo. Baadaye kidogo alielekea katika mji mtakatifu wa Mash'had na mwaka 1257 alikwenda Najaf nchini Iraq kwa ajili ya kutafuta elimu na kusoma kwa walimu wakubwa na mashuhuri wa zama hizo. Ameandika vitabu kadhaa katika masuala ya sheria na fiqhi ya Kiislamu. Sheikhu Shari'a pia alikuwa mstari wa mbele katika mapambano ya kiutamaduni, kisiasa na kijeshi dhidi ya wakoloni wa Kiingereza na aliongoza harakati za wananchi wa Iraq dhidi ya wakoloni hao.

Siku kama ya leo miaka 86 iliyopita, Sheikh Izzuddin Qassam ambaye alikuwa miongoni mwa viongozi wa harakati ya mapambano ya ukombozi wa wananchi wa Palestina dhidi ya uvamizi wa Wazayuni maghasibu na ukoloni wa Uingereza, aliuawa shahidi. Baada ya kukamilisha masomo yake ya awali huko Syria, Sheikh Qassam aliendeleza masomo yake katika Chuo Kikuu cha al Azhar huko Misri. Wananchi wa Palestina walianza mapambana dhidi ya mkoloni Mwingereza mwaka 1930 chini ya uongozi wa Sheikh Izzuddin Qassam. Hata hivyo baada ya kupita miaka kadhaa Wazayuni maghasibu walishirikiana na wakoloni wa Kiingereza na kumuuwa kigaidi kiongozi huyo wa harakati ya mapambano ya Palestina.

Miaka 70 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Oman ilipata uhuru kufuatia makubaliano yaliyosainiwa kati ya nchi hiyo na Uingereza. Oman ina historia kongwe na hadi kabla ya kudhihiri Uislamu, nchi hiyo kuna wakati iliwahi kuwa chini ya mamlaka ya Iran. Nchi hiyo iliwekwa chini ya mamlaka ya Waislamu baada ya kuaga dunia Mtume Muhammad (saw). Karibu karne moja baadaye kundi la Khawarij lilianzisha ghasia na uasi huko Oman na kuitawala nchi hiyo kwa karne kadhaa. Baadaye Oman ikakoloniwa na Ureno na Waingereza.

Siku kama ya leo miaka 53 iliyopita, aliaga dunia John Steinbeck mwandishi wa riwaya wa Kimarekani baada ya kuishi kwa miaka 66. Alizaliwa mwaka 1902. Katika ujana wake Steinbeck alijishughulisha na kazi mbalimbali na hatimaye akaichagua taaluma ya uandishi. Mwandishi huyo alionesha kipaji cha hali ya juu alichokuwa nacho katika uwanja wa uandishi. Machungu ya Steinbeck katika maisha yake yalimuandalia uwanja wa kubainisha masaibu na machungu ya watu wasiojiweza katika maandishi na vitabuu vyake. Miongoni mwa vitabu vyake ni Travels with Charley, East of Eden, A Russian Jornal na Burning Bright.
