May 26, 2016 00:02 UTC
  • Alkhamisi, Mei 26, 2016

Leo ni Alhamisi tarehe 19 Shaaban mwaka 1437 Hijiria, inayosadifiana na tarehe 26 Mei 2016 Miladia


Miaka 1431 iliyopita katika siku inayosadifiana na hii ya leo ya tarehe 19 Shaaban mwaka wa sita Hijria, vita vya Banil Mustalaq vilitokea. Bani Mustalaq lilikuwa kabila miongoni mwa makabila ya Khaza'ah ambalo lilihamia katika vitongoji vya Makka. Viongozi wa kaumu hiyo walikuwa wakiabudu masanamu na kueneza ibada hiyo huko Makka. Bani Mustalaq walijiandaa kupigana vita na Uislamu baada ya Waislamu kupata nguvu na kushika madaraka huko Madina. Kwa msingi huo, Mtume Muhammad SAW aliingia vitani pamoja na wafuasi wake kadhaa na kutoa pigo kubwa kwa kabila hilo.


&&&


Siku kama ya leo miaka 135 iliyopita sawa na tarehe 26 Mei mwaka 1881, Ufaransa ilianza rasmi kuikoloni Tunisia. Kabla ya hapo Ufaransa ilianza kupenya Tunisia kupitia harakati za kiuchumi na kibiashara. Aidha kwa miaka kadhaa Tunisia ilikuwa ikidhibitiwa na Ufaransa. Hata hivyo katika muongo wa 1930 Miladia zilianza harakati za kupigania uhuru kwa uongozi wa Habib Bourguiba, na ilipofika mwaka 1957 nchi hiyo ikajipatia uhuru wake huku Bourguiba akiwa rais wa kwanza wa nchi hiyo. Hata hivyo hadi kufikia mwaka 1987 Bourguiba alianza kuiongoza nchi hiyo kwa mabavu na hivyo kupelekea kupinduliwa na Zine El Abidine Ben Ali. Ben Ali ambaye naye pia aliendeleza sera za udikteta na ukandamizaji aling'olewa madarakni kupitia mapinduzi ya wananchi ya mwezi Januari 2011, na kukimbilia Saudi Arabia. Tunisia yenye ukubwa wa kilometa mraba 163,610 iko kaskazini mwa Afrika na inapakana na nchi za Libya, Algeria na bahari ya Mediterania.


&&&


Na siku kama ya leo miaka 35 iliyopita sawa na tarehe 26 Mei mwaka 1981, kulitangazwa rasmi kuundwa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi. Baraza hilo linazijumuisha nchi 6 za kusini mwa Ghuba ya Uajemi ambazo ni Saudi Arabia, Kuwait, Bahrain, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati), Qatar na Oman. Malengo ya kuundwa baraza hilo ni kuimarisha uhusiano wa kiuchumi, kisiasa, kijeshi na kushirikiana nchi wanachama katika kukabiliana na vitisho vya kigeni.