May 26, 2016 23:04 UTC
  • Ijumaa, 27 Mei 2016

Ijumaa, 27 Mei 2016

Leo ni Ijumaa tarehe 20 Shaaban mwaka 1437 Hijiria, inayosadifiana na tarehe 27 Mei 2016 Miladia
 Siku kama ya leo miaka 1052 iliyopita, yaani tarehe 20 Shaaban mwaka 385 Hijria Ibn Nadim, mwanahistoria na mtaalamu wa masuala ya vitabu wa Kiislamu alifariki dunia. Umashuhuri wa mtafiti huyo unatokana zaidi na kitabu chake maarufu cha Faharasa. Katika kitabu hicho Ibn Nadim amezitaja takriban elimu zote mashuhuri katika ustaarabu wa Kiislamu na kisha kufafanua maisha na historia ya wanazuoni maarufu katika elimu hizo. Kadhalika Ibn Nadim amevitaja humo vitabu na makala zilizoandikwa kuhusiana na elimu hizo.
Siku kama ya leo miaka 106 iliyopita, yaani tarehe 27 Mei 1910, aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 67 Robert Koch, mgunduzi wa vijidudu maradhi aina ya bakteria na tabibu mashuhuri wa Kijerumani aliyegundua chanzo cha maradhi ya kifua kikuu au TB. Daktari Robert Koch alianza kutwalii na kufanya utafiti mkubwa juu ya sababu au vyanzo vya kutokea baadhi ya magonjwa kama vile kipindupindu, kimeta na kifua kifuu, baada ya kuhitimu masomo yake katika fani ya tiba. Mwaka 1882 Miladia, Robert Koch alifanikiwa kugundua vijidudu maradhi vinavyoitwa mycobacterium tuberculosis vinavyosababisha kifua kikuu. Ili kukamilisha uchunguzi wake tabibu huyo Mjerumani alisafiri katika nchi za Afrika Kusini, Misri na India na kutwalii magonjwa mengineyo maarufu katika maeneo hayo kama vile Malaria. Mwaka 1905 Robert Koch alitunukiwa Tunzo ya Nobel katika uwanja wa Tiba.
Na siku kama ya leo miaka 179 iliyopita, yaani tarehe 27 Mei 1837, ulitiwa saini mkataba wa amani kati ya Ufaransa na Amir Abdulqadir wa Algeria kiongozi wa wapigania uhuru wa nchi hiyo. Tangu mwaka 1832 baada ya mashambulizi ya jeshi la Ufaransa nchini Algeria Amir Abdulqadir aliendesha mapambano dhidi ya wavamizi huko Algeria na kusimama kidete dhidi yao kwa miaka kadhaa na kujulikana kama kiongozi wa wanamapambano wa Algeria dhidi ya Ufaransa. Baada ya kufikiwa makubaliano hayo maeneo mengi ya Algeria yaliyokuwa chini ya Ufaransa yalipewa uhuru.