Jan 10, 2022 16:50 UTC
  • Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (37)

Assalaam alaykum wapenzi wasikilizaji popote pale yanapokufikieni matangazo haya ya Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu ili tuweze kufungua ukurasa mwingine katika kurasa za historia ya Maulamaa na wanazuoni wa Kishia pamoja na mchango wao katika Uislamu. Kipindi chetu kilichopita kilitupia jicho kwa mukhtasari historia na maisha ya Muhammad bin al-Ḥassan bin Ali bin al-Ḥussein mashuhuri zaidi kwa jina la Sheikh al-Hurr al-Amili mwanazuoni na msomi mwingine maarufu wa Kishia mwandishi wa kitabu cha Wasa'il al-Shia, moja ya vitabu mashuhuuri vya hadithi vya Waislamu wa madhehebu ya Kishia. Kipindi chetu cha juma hili ambacho ni sehemuu ya 37 ya mfululizo huu kitamzungumzia Sayyid Hashim Bahrani au Allamah Bahrani. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

 

Sayyid Hashim Bahrani mtoto wa Sayyid Suleiman Bahrani mashuhuri zaidi kwa jina la Allama Bahrani ni mmoja wa wanazuoni na Maulamaa wakubwa wa Kishia katika elimu ya hadithi ambaye ameacha na kuvirithisha vizazi vilivyokuja baadaye yake dafina na utajiri mkubwa wa vitabu. Alizaliwa katika nusu ya kwanza ya karne ya 11 Hijria katia kijiji cha Gatkan moja ya viunga vya mji wa Tubli. Katika zama hizo, Tubli ulikuwa mji mkuu wa kisiasa na kielimu wa Bahrain.Tarehe hasa ya kuzaliwa kwake haijasajiliwa katika vitabu vya historia lakini baadhi ya wanahistoria wanasema kuwa, alizaliwa baina ya mwaka 1030 na 1040 Hijria. Inaelezwa kwamba, nasaba yake inaishia kwa Imam Mussa al-Kadhim (as), Imam wa Saba kati ya Maimamu 12 kutoka katika kizazi cha Bwana Mtume (saww). Tubli ulikuwa mji na makao makuu ya watawala wa zama hizo huko Bahrain na uliondokea kuwa mashuhuri kutokana na kuwa kitovu na makao makuu ya kisiasa na kielimu. Katika zama hizo Sheikh Muhammad bin Majid bin Masoud Bahrani alikuwa Marjaa na kiongozi wa kielimu na kimaanawi katika eneo hilo.

Sayyid Hashim Bahrani alisoma masomo yake ya msingi huko Bahrain. Kuhusiana na hilo hakuna taarifa kamili NA za kutosha. Hata hivyo nafasi ya kijamii ya alimu na mawanazuoni huyu ilikuwa muhimu na ya kuzingatiwa. Baada ya kusoma kwa muda, alifunga safari na kuelekea katika mji mtakatifu wa Najaf huko Iraq lengo likiwa ni kwenda kujiendeleza zaidi kielimu. Akiwa huko Allama Bahrani alihudhuria masomo ya walimu mahiri na watajika wa zama hizo. Baada ya miaka kadhaa na baada ya kufikia daraja ya juu ya kielimu na kimaanawi ya Ijitihad akawa Marjaa mkubwa wa Chuo Kikuu hicho cha Kiislamu (Hawza). Licha ya kuwa, mwaka hasa aliowasili huko Najaf haufahamiki lakini nyaraka za historia zinaonyesha kuwa, mwaka 1063 Hijria alikuwa akihudhuria darsa na masomo ya mwalimu mkubwa wa Najaf Fakhrudin Turaihi. Baada ya kusoma na kufundisha kwa muda huko Najaf, Allama Bahrani alirejea eneo alilozaliwa huko Bahrain na baada ya kuaga dunia Sheikh Muhammad bin Majid, Bahrani alichukua jukumu la Umarjaa na uongozi wa kidini na kielimu. Wigo wa Umarjaa wake ulipanuka zaidi na kufika katika ardhi nyigine za Kiislamu nje ya Bahrain ambapo kulikuweko na Mashia wengi waliokuwa wakimkalidi na kumfuata katika hukumu za kisheria.

Mahali alipozikwa Sayyid Hashem Bahrani

 

 

Allama Bahrani mbali na kufundisha, kualifu vitabu na kutekeleza majukumu yake kama Marjaa na kiongozi wa kidini, alikuwa akifanya hima ya kuboresha hali ya kijamii kwa kuwasaidia watu wahitaji na wasiojiweza. Alisifika kwa misimamo thabiti na kutotetereka hasa katika kukabiliana na watawala wa wakati huo wa Bahrain. Kudumu kwake katika kuamrisha mema na kukataza maovu ni mambo yaliyowafanya watu wazidi kumpenda na kugeuka kuwa kipenzi cha Waislamu nchini Bahrain na viunga vyake. Allama Bahrani alikuwa mcha Mungu na mkemea maovu ambaye hakuwa na mzaha kabisa na magavana na watawala kama ambavyo alikuwa mtetezi mkubwa wa haki za watu na kimbilio lao.

Allama Bahrani aliufanya wakfu umri na maisha yake kwa ajili ya kukusanya, kuandika na kusahihisha hadithi na katu hakuchoka kutafuta vitabu vya hadithi na kukusanya nakala za vitabu hivyo ambapo sambamba na kusahihisha alifanya kazi ya kuzipanga hadithi ili iwezekane kuzitumia vyema. Msomi na mwanazuoni huyu ana athari na mchango mkubwa katika Uislamu kutokana na kazi kubwa aliyoifanya ya kuandika vitabu katika maudhui mbalimbali za elimu za Kiislamu. Wanahistoria wametaja vitabu 75 vya msomi huyu. Athari zake nyingi zinahusiana na kuthibitisha Uimamu, sifa maalumu, fadhila za Maasumina na hadithi zao.

Allama Bahrani alikuwa na mbinu na mtindo makini na maalumu katika kuandika vitabu vya hadithi na riwaya. Akiwa na lengo la kuthibitisha Uimamu wa Ali bin Abi Twalib (as) na Maimamu wengine Maasumina (as) alitumia hadithi za Waislamu wa madhehhebu ya Kisuni na alinukuu hadithi ya Manzila kupitia sanadi na mlolongo wa mapokezi mia moja kutoka kwa wasomi na wanazuoni wa Kisuni akitaja majina yao na vitabu vyao. Hadithi ya Manzila ni mashuhuri baina ya Maulamaa wa Kiislamu ambapo katika hadithi hiyo Bwana Mtume (saww) aliainisha na kubainisha nafasi, daraja na cheo cha Ali bin Abi Twalib (as) pale alipomwambia: Wewe kwangu mimi ni kama alivyokuwa Haruna kwa Mussa, isipokuwa hakuna Nabii baada yangu.

 

Moja ya athari muhimu ya Allama Bahrani ni tafsiri mashuhuri ya Qur'ani Tukufu ya al-Burhan fi Tafsir al-Qur'ani. Katika kueleza wasifu wa tafsiri yake hii ya Qur'ani Allama Bahrani ameandika: Kitabu hiki kimejumuisha akthari ya riwaya na hadithi za tafsiri kutoka kwa Ahlul-Baiti (as) kama ambavyo kimejumuisha fadhila zao nyingi na Aya zilizoshuka kwa haki yao na kina hukumu nyingi, adabu na visa vya Mitume na elimu nyingine ambazo huwezi kuzipata katika kitabu kingine.

Nchi ya Bahrain ambayyo inajulikana kama Lulu ya Ghuba ya Uajemi, kijiografia ipo kusini mwa eneo la Ghuba ya Uajemi. Nchi hii katika kipindi chote cha historia ya Uislamu daima imekuwa moja ya kambi muhimu na imara za Waislamu hususan Mashia na imekuwa chimbuko la wasomi na mafakihi wengi. Kimsingi ni kuwa, baada ya Iraq na Iran, nchi ya Bahrain ni Hawza na Chuo cha tatu kikubwa zaidi cha Kishia katika ulimwengu wa Kiislamu. Nafasi muhimu ya kiutamaduni, kisiasa na kijiografia ya Bahrain imeifanya nchi hiyo daima iandamwe na hujuma na uvamizi wa madola makubwa na yanayotumia mabavu kwa ajili ya kudhibiti na kupora ardhi ya nchi hiyo. Kutokana na uvamizi na hujuma hizo za mara kwa mara wananchi wa nchi hiyo wamekumbwa na hasara nyingi za kiroho na kimali. Hujuma hizo zilibana medani ya Maulamaa na kuwafanya wahajiri na kuelekea katika nchi jirani kama Iran na Iraq. Watoto wa Allama Bahrani ni miongoni mwa watu waliohajiri na kuja Iran na kuchagua mji wa Isfahan kuwa makazi yao.

Hatimaye baada ya kuishi umri uliojaa jihadi ya kielimu ni kiamali katika njia ya kusukuma mbele gurudumu la maktaba ya Ahlul-Baiti (as), Allama Sayyid Hashim Bahrani aliaga dunia mwaka 1107 Hijiria huko nchini Bahrain na kuzikwa huko Tubli jirani na msikiti mmoja mashuhuri. Kaburi lake hadi leo lingali linatembelewa na Waumini ambao huonyesha heshima na taadhhima maaluumu kwa msomi na mwanazuoni huyo. Tunamoumba Allah amfufue pamoja na Maasumina (as).

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh

Tags