Apr 22, 2022 01:54 UTC
  • Ijumaa tarehe 22 Aprili 2022

Leo ni Ijumaa tarehe 20 Ramadhani 1443 Hijria sawa na Aperili 22 mwaka 2022.

Siku kama ya leo miaka 1435 iliyopita jeshi la Kiislamu lililokuwa na wapiganaji elfu kumi chini ya uongozi wa Mtume Muhammad (saw) liliukomboa mji wa Makka. Mtume Mtukufu alichukua hatua hiyo baada ya makafiri kukiuka makubaliano ya amani ya Hudaibiya ambayo yalisainiwa mwaka wa Sita Hijria kati yake na wakuu wa Makuraishi. Mtume Muhammad (saw) alitoa msamaha kwa wakazi wote wa Makka baada ya kukombolewa mji huo katika hali ambayo huko nyuma watu hao walikuwa wakipinga na kupiga vita Uislamu na pia walimuudhi mno Mtume na kuwatesa Waislamu wengi. Muamala huo wa huruma na upendo wa Mtume (saw) uliwavutia watu wa kabila la Kuraishi kuingia katika dini tukufu ya Uislamu. Kwa msingi huo mji wa Makka ulikombolewa pasina kuwepo umwagaji damu.

Siku kama ya leo miaka 901 iliyopita, alifariki dunia Ibn Shajari Baghdadi, fasihi na mtaalamu wa elimu ya nahau wa Waislamu. Abu Sa'adat Hibatullah Ibn Ali Alawi Hassani, mtaalamu wa nahau, lugha ya Kiarabu, fasihi na malenga wa Kishia, alizaliwa mwaka 450 Hijiria. Nasaba ya msomi huyo inarejea hadi kwa Imam Hassan (as) mjukuu wa Mtuke Muhammad (saw) na ni kwa ajili hiyo ndio maana akaitwa Alawi, Hassani. Akiwa kijana alianza kusomea fasihi, nahau, hadithi na elimu mbalimbali za zama zake na kamwe hakuwahi kuacha kusoma, kama ambavyo hata alipokuwa mzee, bado aliendelea kujifunza kwa wasomi wa zama zake. Aidha alifundisha lugha ya nahau kwa kipindi cha miaka 70 ambapo alitokea kupata wanafunzi mashuhuri katika uwanja huo. Miongoni kwa athari zake ni pamoja na kitabu kinachoitwa 'Al-Aamaal' 'Al-Hamaasah' na 'Mandhumat Ibn Shajarah.' Hatimaye alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 92 mjini Baghdad Iraq na kuzikwa mjini hapo.

Siku kama ya leo miaka 817 iliyopita, alifariki dunia Yaqut Hamawi mmoja wa waandishi na msomi mtajika wa Kiislamu wa karne ya Saba Hijria na mtaalamu mashuhuri wa jiografia. Alizaliwa mwaka 539 Hijria huko Baghdad ambapo ujanani mwake alikamatwa mateka na kufanywa mtumwa. Hata hivyo baada ya kupita muda mfanyabiashara mmoja wa Baghdad alimnunua Hamawi na baadaye akamuachia huru. Miongoni mwa athari za uandishi za Yaqut Hamawi tunazoweza kuziashiria ni vitabu vyake viwili alivyovipa majina ya "Muujamul-Buldan" na Muujamul- Udabaa."

Yaqut Hamawi

Siku kama hii ya leo miaka 127 iliyopita wananchi wa Cuba kwa mara nyingine tena walianzisha mapambano ya kupigania uhuru wao kutoka kwa wakoloni wa Uhispania. Hayo yalikuwa mapambano yao ya tatu katika nusu ya pili ya karne ya 19 Miladia kwa ajili ya kutaka kujitawala. Uhispania ilituma wanajeshi laki tatu nchini humo kwa ajili ya kupambana na wanamapinduzi hao. Kufuatia vurugu hizo Marekani ilitumia fursa hiyo na kwa kisingizio cha kulipuliwa meli yake ya kivita karibu na pwani ya Cuba mwaka 1898 Miladia, kuingia katika vita hivyo dhidi ya Uhispania. Manuari za kivita za Uhispania ziliangamizwa katika maji ya Cuba na hatimaye nchi hiyo ya Amerika ya Latini ikakaliwa kwa mabavu na Marekani.

Bendera ya Cuba

Miaka 118 iliyopita katika siku kama hii ya leo alizaliwa mwanafizikia na mtengenezaji wa bomu la atomiki wa Marekani Robert Oppenheimer. Kabla ya Vita vya Pili vya Dunia mtaalamu huyo alifanya utafiti kuhusiana na jinsi ya kupasua atomu na kupata nishati ya nyuklia. Wakati wa vita hivyo alipewa wadhifa wa kusimamia kitengo cha utafiti katika Wizara ya Vita ya Marekani na chini ya usimamizi wake yakatengenezwa mabomu matatu ya kwanza ya nyuklia. Hata hivyo, wakati Marekani ilipoishambulia Japan kwa mabomu ya nyuklia mwaka 1945, makumi ya maelfu ya watu wasio na hatia waliuawa katika kipindi kifupi, hali iliyomfanya Oppenheimer kujutia kitendo chake hicho na akatoa wito wa kutumiwa nishati ya atomiki katika masuala ya amani.

Robert Oppenheimer

Miaka 74 iliyopita mwafaka na siku kama hii ya leo, yaani tarehe 22 Aprili 1948, Wazayuni waliushambulia mji wa bandari wa Haifa huko kaskazini magharibi mwa Palestina wakati wa kukaribia kuanzishwa utawala haramu wa Israel. Wazayuni waliwauwa shahidi Wapalestina 500 katika mashambulizi hayo makubwa na kuwajeruhi wengine 200 ambao walikuwa wanawake na watoto waliokimbilia huko Haifa wakisubiri kupelekwa katika maeneo mengine.

Bandari ya Haifa

Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita Imam Khomeini (M.A) mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitoa amri ya kuundwa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH). Kwa mujibu wa amri hiyo, jukumu kuu la jeshi hilo ni kulinda Mapinduzi ya Kiislamu dhidi ya maadui wa ndani na nje. Baada ya kuundwa, jeshi la SEPAH lilikabiliana na makundi yaliyopinga Mapinduzi ya Kiislamu, yaliyoanzisha mapambano ya silaha katika pembe mbalimbali za Iran na kuweza kuzima njama za maadui. Aidha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi liliweza kudhihirisha uwezo mkubwa wakati wa vita vya kulazimishwa kati ya Iraq na Iran vilivyoanzishwa na utawala wa dikteta Saddam Hussein kwa lengo la kuyaangamiza Mapinduzi ya Kiislamu na kuigawa Iran.