Apr 28, 2022 06:13 UTC
  • Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (43)

Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu

 

Kipindi kilichopita kilimzungumzia Allama Bahbahani. Msomi huyu alikuwa mashuhuri kwa harakati zake dhidi ya Akhbariyun, kundi la Maulamaa linaloamini kwamba, dhahiri ya hadithi inatosha kwa ajili ya kufahamu maamrisho na maagizo ya dini. Mkabala na mrengo huo kuna mrengo wa Usuliyun ambao unaamini kwamba, ili kuainisha kwa njia sahihi hukumu za dini, ni lazima mtu awe na utaalamu na ubobezi wa kielimu na kuna haja ya kuweko watu ambao kutokana na umahiri na kutabahari kwao kwa vyanzo vya dini na kwa kutumia mbinu makini za kielimu na kiakili wanyambue hukumu za dini kuhusiana na masuala mbalimbali. Sehemu ya 43 ya mfululizo huu juma hili inamzungumzia msomi mwingine mahiri wa Kishia ambaye ni Allama Bahrul Ulum. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki. 

Sayyid Muhammad Mahdi Tabataba'i Najafi ambaye ni mashuhuri kwa jina la Allama Bahr al-Ulum, fakihi, mpokezi wa hadithi na arif mwenye tawfiki kubwa wa Kishia alizaliwa katika siku ya Eidul Fitr mwaka 1155 Hijria katika mji wa Karbala huko Iraq. Baba na babu zake walikuwa wasomi na wanazuoni wa dini na anahesabiwa kuwa mmoja wa wajukuu wa Majlisi wa Kwanza.

Sayyid Muhammad Mahdi alianza kuhudhuria darsa za wanazuoni wakubwa katika Hawza ya Najaf Iraq wakati huo akiwa angali kijana mdogo. Alisoma masomo ya awali na ya msingi huko Najaf kwa baba yake msomi na mwanazuoni mkubwa yaani Sayyid Murtadha Tabatabai Boroujerdi na Sheikh Yusuf Bahrani mmoja wa wanazuoni wakubwa katika zama hizo.  Baada ya kuwa amesoma kwa kiwango cha kutosha kwa walimu hao alirejea Karbala ili aweze kuhudhuria darsa na vikao vya elimu vya Allama Wahid Bahbahani ambaye katika zama hizo alikuwa na jukumu la Marjaa wa Mashia.

Sayyid Muhammad Mahdi Tabataba'i Najafi ambaye ni mashuhuri kwa jina la Allama Bahr al-Ulum

 

Baada ya Sayyid Muhammad Mahdi kusoma katika Vyuo vya Kidini vya Najaf na Karbala mwaka 1186 Hijria alifanya safari katika mji wa Mash'had ambapo akiwa kando ya Haram ya Imam Ali bin Mussa Ridha (as) alijishughulisha na kulea nafsi sambamba na kushiriki katika masomo na elimu mbalimbali.

Katika kipindi hicho mbali na kushiriki katika masomo ya kawaida ya Hawza, alikuwa akishiriki somo la falsafa kwa Mirza Muhammad Mahdi Khorasani mwenye lakabu ya Shahidi wa Nne.

Siku moja wakati somo linaendelea, Mirza Khorasani ambaye alikuwa ameshangazwa mno na akili na maarifa ya hali ya juu ya mwanafunzi wake alimhutubu kwa kumwambia: انما انت بحرالعلوم

Yaani kwa hakika wewe ni bahari ya elimu.". Ni kuanzia kipindi hicho, ndipo msomi huyo akaondokea kuwa mashuhuri kwa jina la Sayyid Bahrul Ulum, lakabu ambayo alibakia nayo mpaka mwishoni mwa umri wake. Baada yake pia familia yake iliondokea kuwa mashuhuri kwa lakabu hii ya Bahrul Ulum.

 

Katika kipindi cha masomo na kutafuta kwake elimu katika mji wa Mash'had Allama Bahrul Ulum alifanikiwa kufikia daraja la mwalimu katika masomo ya fikihi, hadithi na falsafa na kuzingatiwa mno na akthari ya Maulamaa na walimu katika zama hizo.

Ni kwa msingi huo ndio maana Allama Wahid Bahbahani aliyekuwa Marjaa wa Mashia katika zama hizo na aliyekuwa mwishoni mwa umri wake, akamuita Najaf Allama Bahrul Ulum ili akachukue jukumu la uongozi wa Hawza na Umarjaa wa Mashia. Hii ni kutokana na kuwa, Allama Wahid alikuwa akihisi kwamba, kutokana na umri mkubwa, uzee na udhaifu wa mwili na fikra inastahiki wadhifa na jukumu hilo kubwa na zito likabidhiwe kwa mtu mwenye uwezo. Kwa muktadha huo, Allama Bahrul Ulum akiwa hajafikisha hata miaka 40 alichukua jukumu la kuwaongoza Waislamu huku akiendelea pia na kazi ya kufundisha na kualifu vitabu. Aidha alikuwa mstari wa mbele pia katika kushughulikia matatizo na hawaiji za masikini na watu wahitaji na wasiojiweza. Alimu huyu alikuwa akitatua shida za watu na kushughulikia matatizo ya kijamii ya watu.

Allama Bahrul Ulum akiwa na lengo la kufanikisha utatuzi wa masuala na matatizo mbalimbali ya kijamii yaliyokuwa yakiukumba Umma wa Kiislamu na kuleta nidhamu katika vyuo vya kidini (Hawza) aliwaita wanazuoni na mafakihi mahiri katika zama zake na kuwagawia majukumu. Ugavi huu wa majukumu uliokuwa na nidhamu na mpangilio maalumu ni jambo ambalo halikuwa limezoeleka baina ya Maulamaa. Kwa ubunifu huu usimamizi wa Hawza na kutoa majibu na kushughulikia mahitaji ya wananchi ukawa umerahisishwa na kuharakishwa zaidi.

 

Allama Bahrul Ulum alimteua Sheikh Ja'afar Kashif al-Ghitaa kuchukua jukumu la kutoa fatuwa, akamchagua Sheikh Hussein Najafi kuwa Imam wa Swala ya Jamaa mjini Najaf, akamkabidhi masuala ya mashtaka na utoaji hukumu yaani ukadhi Sheikh Muhiyidin na akampatia Sayyid Muhammad Jawad Amili jukumu la kualifu na kuandika masuala yanayohusiana na fikihi, ambapo matunda ya juhudi zake zikawa ni kuandika kitabu cha fikihi ambacho ni mashuhuri kwa jina la Miftahul Karamah. Aidha Allama Bahrul Ulum yeye akawa akijihusisha na masuala ya usimamizi na uongozi wa Hawza mjini Najaf pamoja na masuala yanayohusiana na masomo na elimu. Ni kwa kuzingatia hayo, ndio maana katika kipindi na zama za uongozi wa Bahrul Ulum katika Hawza ya Najaf, chuo hicho cha kidini kilinawiri na kuimarika mno kielimu na kiharakati.

 

Allama Bahr al-Ulum ameacha athari nyingi za vitabu alivyoandika katika elimu mbalimbali za Kiislamu ambapo miongoni mwa vitabu vyake muhimu ni Misbahul Ahkam, al-Durat al-Najafiyah na Mishkat al-Hidayah.

Allama Bahrul Ulum alikuwa mahiri pia katika utunzi wa mashairi na kuna athari nyingi pia za alimu huyu katika uga huu. Mwaka 1193 Hijria alifanya safari huko Makka na kulazimika kuficha itikadi yake ya Ushia ili asalimike na maadui. Watu wa kawaida na wasomi taratibu wakaanza kumkubali na kumsogelea mwanazuoni huyu ambaye baadaye alilazimika kukaa huko kwa muda wa miaka miwili baada ya kuona mazingira ya eneo hilo ni mwafaka kwa ajili ya kuendesha harakati za kielimu na kuwaongoza watu.

Baada ya kuenea habari ya Ushia wa Bahrul Ulum huko Hijaz, baadhi ya watu wenye taasubi kutoka katika madhehebu zingine waliamua kuanzisha mdahalo na majadiliano na alimu huyu. Hata hivyo, kutokana na Bahrul Ulum kubobea na kutabahari katika elimu alifanikiwa kuwashinda wote na hivyo kufanikiwa kulifanya kundi kubwa la watu kuingia katika madhehebu ya Ahlul-Baiti (as) akiwemo Imam wa Swala ya Ijumaa mjini Makka wakati huo aliyekuwa miongoni mwa Maulamaa wa Kisuni ambaye akiwa na umri wa miaka 80 aliamua kuuchana na madhehebu ya Kisuni na kuingia katika madhehebu ya Kishia.

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa leo umefikia tamati tukutane tena wiki ijayo, ambapo tutaendelea na maudhui yetu ya kumzungumzia Sayyid Muhammad Mahdi Tabataba'i Najafi ambaye ni mashuhuri kwa jina la Allama Bahr al-Ulum.

Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh

Tags