Jumatatu, 30 Mei, 2022
Leo ni Jumatatu tarehe 28 Mfunguo Mosi Shawwal 1443 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 30 Mei 2022 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 970 iliyopita alizaliwa Sanai Ghaznawi Hakim Abul-Majd Majdud ibn Ādam Sanai Ghaznavi, malenga, tabibu na mwanairfani mkubwa wa Iran mjini Ghazni. Ghaznavi alianza kusoma mashairi ya kuwasifu watawala akiwa bado kijana mdogo. Hata hivyo muda mfupi baadaye aliachana na mwenendo huo na kuanza kusomea elimu ya irfan (ya kumjua Mwenyezi Mungu). Kuanzia wakati huo alianza kuishi maisha ya kuwatumikia wananchi sambamba na kusoma mashairi ya kuwakosoa watawala dhalimu na mafisadi. Alianzisha pia mfumo wa aina yake katika usomaji wa mashairi. Miongoni mwa athari za Sanai Ghaznawi ni pamoja na kitabu cha 'Hadiqatul-Haqiqah' ambacho kina muundo wa mashairi na ndani ya kitabu hicho malenga huyo mkubwa ameweka wazi fikra zake za kimaadili na irfani. Vitabu vya 'Elahi Nameh' 'Karnameh Balkh' na 'Twariqut-Tahqiq,' ni miongoni mwa athari za Sanai Ghaznawi. ***

Miaka 278 iliyopita katika siku kama ya leo, Alexander Pope mshairi na mwanafalsafa mashuhuri wa Kiingereza aliaga dunia. Alizaliwa mjini Londone Mei 21 mwaka 1688 katika familia ya kitajiri, Hata hivyo kutokana na kuwa na ukilema wa viungo, baba na mama yake walimlea nje ya mji katika nyumba moja. Alipofikisha umri wa miaka 15 Alexander Pope alikuwa tayari anazifahamu vyema lugha za Kigiriki, Kifaransa na Kitaliano. Alitoa mjumuko wake wa kwanza wa mashairi alipokuwa na umri wa miaka 23.***

Katika siku kama ya leo miaka 244 iliyopita sawa na tarehe 30 Mei 1778, Francois - Marie Arouet maarufu kwa jina la Voltaire, mwanafalsafa na mwandishi wa Kifaransa alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 84. Katika maisha yake, Voltaire aliwahi kuwekwa mahabusu mara mbili na kubaidishwa kwa muda wa miaka mitatu nchini Uingereza. Kitendo hicho kilimkasirisha sana Voltaire na kumfanya kuwa dhidi ya utawala wa Ufaransa. ***

Na miaka 98 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Ali Akbar Khan Nafisi aliyejulikana kama Naadhimul Atibaa, daktari na mtaalamu wa lugha wa Kiirani, katika mji wa Tehran. Baada ya kumaliza masomo yake ya msingi alianza kujifunza masomo ya kidini na udaktari katika chuo cha Darul Funun cha Tehran. Baadhi ya vitabu vilivyoandikwa na Naadhimul Atibaa katika uwanja wa tiba vimetarjumiwa katika lugha za kigeni. Ali Akbar Khan Nafisi ambaye pia alikuwa mtaalamu wa lugha alifanya jitihada kubwa katika kukusanya maneno ya lugha ya Kifarsi na kuandika kamusi inayoitwa 'Kamusi ya Nafisi.' ***
