Ufufuo na Safari ya Kurejea kwa Allah (5)
Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi ni wakati mwingine tena wa kuwa nanyi katika kipindi hiki cha ufufuo na safari ya kurejea kwa Allah. Ni matarajio yetu mtaendelea kuwa nasi hadi mwisho wa kipindi hiki ambapo leo hii kitazungumzia hakika ya kifo na umauti na kupelekwa roho katika ulimwengu mwingine na ajal au kifo ambacho wakati wake haubadilishwi na kile ambacho wanawakti wake unaweza kubadilika. Karibuni.
Kifo ni kanuni jumla kwa ajili ya viumbe vyote ambayo takriban tunasika habari zake kila siku na baadhi ya wakati tunaishuhudia kwa macho yetu. Watu wengi wanaopenda maisha ya dunia na wanaojishughulisha na starehe na anasa za kidunia hudhani kwamba, kifo ni maangamizo na kwamba hakuna maana ya kuwepo maisha baada ya kifo. Kwa msingi huo watu hawa huogopa kifo na daima wanakimbia alama na ishara zake. Mwenyezi Mungu amewahutubu watu wa aina hiyo ndani ya Qur'ani Tukufu katika aya ya 78 ya Suratu Nisaa akisema kwamba: "Popote mtakapokuwa yatawafika mauti na hata kama mkiwa katika ngome madhubuti".
Dini tukufu ya Kiislamu inabainisha wazi kuwa, mauti hayana maana ya kuangamia kwa mwanadamu, bali ni dirisha la kuelekea kwenye maisha ya milele. Kwa maana nyingine tunaweza kusema kuwa, kifo kwa mwanadamu ni mwisho wa maisha yake ya hapa dunani na kuelekea kwenye ulimwengu mwingine, na ni mwanzo wa maisha mapya ya Akhera. Hali hiyo imefananishwa na kitoto kichanga kinapotoka ndani ya fuko la uzazi la mama yake na kuingia kwenye maisha ya duniani. Kichanga hicho huingia kwenye mazingira na ulimwengu mpana na mkubwa zaidi kuliko hapo awali kilipokuwa katika fuko la uzazi ndani ya tumbo la mama. Hivyo hivyo, mwanadamu anapofariki dunia, huanza maisha ya Akhera na anakuwa mithili ya mtoto mchanga aliyezaliwa na kuanza maisha mapya na bora zaidi dunia akitokea katika fuko la uzazi. Mtoto anapokuwa ndani ya fuko la uzazi hula chakula kupitia njia ya kitovu, lakini mara tu anapozaliwa njia hiyo hufungwa na badala yake hula chakula kwa kutumia mdomo. Baadhi ya viungo vya mtoto huyo kama vile vinavyotumika kusikilizia, kuonea, kugusia, kuonjea na kunusia huundika na kutengenezeka kipindi mtoto anaposimama kwa muda katika fuko la uzazi la mama yake na hutengenezwa kwa ajili ya awamu na kipindi kingine. Dunia pia ikilinganishwa na Akhera ni mithili ya fuko la uzazi la mama ambako viungo mbalimbali na sifa za kinafsi za mwanadamu huundika kulingana na ulimwengu wa Alkhera na kujifunza jinsi ya kuishi katika ulimwengu wa baadaye. Hivyo, iwapo mwanadamu atashindwa kuhamisha uwezo na vipawa vyake vya kiroho na kimaanawi na kuvipeleka katika ulimwengu wa Akhera, itakuwa na maana kwamba, baada ya ulimwengu wa ndani ya fuko la uzazi hakuna dunia nyingine na kwamba watoto wote hutoweka baada ya kumalizika kipindi cha kuishi ndani ya fuko hilo. Wakati huo italazimu kusema kuwa, viungo kama vile vya kusikilizia, kuonea, kugusia, kuonjea, kunusia, ubongo, mishipa ya fahamu, mapafu, utumbo na kadhalika, vimeumbwa hivihivi bure bilashi na bila ya faida wala lengo maalumu. Hii ni kwa sababu vimetoweka na kufa hivihivi bila ya kutumiwa. Mwenyezi Mungu SW anasema katika aya ya 115 ya Suratul Muuminun kwamba: "Je, mnadhani kuwa tuliwaumba bure na kwamba nyinyi Kwetu hamtarudishwa? <<< >>>>>
Mauti wapenzi wasikilizaji ni miongoni mwa siri za dunia. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, kifo ni uzoefu na tajiriba ya mtu binafsi ambayo hutokea kwa kukatika mawasiliano yote kati ya mtu na dunia hii. Kwa msingi huo mwenye zoefu na tajiriba hiyo hawezi kuwasimulia tajiriba yake wanadamu wengine.
Wasomi na wataalamu wa elimu na taaluma mbalimbali wameelezea nadharia zao kuhusiana na maudhui hii ya umauti kwa mitazamo tofauti. Wataalamu wa biolojia wanaeleza kuwa, mauti ni kusimama harakati za ubongo, moyo na hisia tano katika mwili wa mwanadamu na hatimaye mwili unapoteza joto lake na kuwa kiwiliwili kikavu. Kwa mtazamo wa wataalamu hawa wa biolojia, kifo kina maana ya kuangamia kwa mwili. Wasomi hawa wa biolojia kwa kawaida huwa hawazungumzii lolote kuhusiana na kutoka kitu katika mwili kwa jina la roho au nafsi wakati mwanadamu anapofariki dunia. Halikadhalika wataalamu wa sayansi za jamii, kila mmoja hukielezea na kukifasiri kifo kwa mtazamo wake na kulingana na taaluma yake.
Kwa upande wao baadhi ya wanafalsafa hukiarifisha kifo kuwa ni mtokeo ya mtengano wa kudumu wa roho au nafsi na mwili baada ya kuvurugika mfumo wa kimaumbile wa mwili. Wanafalsafa hawa hufananisha kifo, kutoka roho au nafsi kwenye mwili na mtu ambaye nyumba yake imeharibika na hana budi kuondoka na kuomba hifadhi sehemu nyingine.
Kitabu kitakatifu cha Qur'ani kina maelezo mengine kuhusiana na kifo au umauti. Qur'ani Tukufu inakielezea kifo kwa kutumia neno lenye maana ya kuchukuliwa kitu kwa ukamilifu. Qur'ani imetumia neno "tawaffa" kuzungumzia hakika ya mauti na kifo ambalo lina maana ya 'kuchukuliwa kitu kwa ukamilifu' na kuhamishiwa katika ulimwengu wa milele. Mwenyezi Mungu SW anasema katika aya ya 42 ya Suratu Zumar kwamba: "Mwenyezi Mungu huzichukua roho zinapokufa..". Kwa kutegemea aya hii, wafasiri wa Qur'ani Tukufu wanaeleza kwamba, roho ndiyo sehemu muhimu na kuu ya mwanadamu. Roho ndiyo inayojenga shakhsia na dhati halisi ya mwanadamu, wala siyo umbile na mwili wake wa kimaada. Hii ni kwa sababu Mwenyezi Mungu anasema, wakati wa kufariki dunia huichukua roho kikamilifu. Hii ni licha ya kwamba, mwili wa kimaada wa kiumbe hubaki humu humu duniani na hatua kwa hatua, nyama hujitenga na mifupa na kisha hulika na kutawanyika. Kwa msingi huo hakika ya uwepo wa mwanadamu ambayo Qur'ani Tukufu inaiita nafsi au roho, haiangamii na kutoweka, bali hutolewa katika ulimwengu huu wa kimaada na kuhamishiwa katika ulimwengu mwingine wa Akhera. Imam Ja'far Sadiq (as) anasema: Mwanadamu ameumbwa kutokana na mambo mawili ya dunia na Akhera. Wakati Mwenyezi Mungu anapokusanya pamoja mambo hayo mawili mwanadamu huishi duniani, na wakati Mwenyezi Mungu anapoyatenganisha, mtengano huo huwa na maana ya mauti na kifo, na katika hali hiyo jambo la Akhera hurejea mbinguni. Kwa msingi huo, maisha ni ya hapa duniani na kifo ni kuelekea Akhera. Hii ni kwa sababu, wakati wa kifo hutokea mtengano baina ya mwili wa kimaada na roho; roho hurejea mbinguni na mwili hubakia ardhini kwa sababu mwili hutokana na ardhi na dunia hii", mwisho wa hadithi. (Biharul Anwar, juzuu:6) <<<<<< >>>>>>