Sura ya Fuss’ilat, aya ya 13-18 (Darsa ya 876)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 876 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 41 ya Fuss’ilat. Tunaianza darsa yetu ya kwa aya ya 13 na 14 za sura hiyo ambazo zinasema:
فَإِنْ أَعْرَضُوا فَقُلْ أَنذَرْتُكُمْ صَاعِقَةً مِّثْلَ صَاعِقَةِ عَادٍ وَثَمُودَ
Basi wakipuuza wewe sema: Nakuhadharisheni adhabu mfano wa adhabu ya A'di na Thamudi,
إِذْ جَاءَتْهُمُ الرُّسُلُ مِن بَيْنِ أَيْدِيهِمْ وَمِنْ خَلْفِهِمْ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا اللَّهَ ۖ قَالُوا لَوْ شَاءَ رَبُّنَا لَأَنزَلَ مَلَائِكَةً فَإِنَّا بِمَا أُرْسِلْتُم بِهِ كَافِرُونَ
Walipo wajia Mitume mbele yao na nyuma yao wakawaambia: Msimuabudu ila Mwenyezi Mungu! Wakasema: Angeli taka Mola wetu Mlezi bila ya shaka angeli wateremsha Malaika. Basi sisi hakika tunayakataa hayo mliyo tumwa.
Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizozungumzia baadhi ya ishara za ujuzi na uwezo wa Mwenyezi Mungu mbinguni na ardhini. Aya hizi zinawahutubu wanaomkanusha Allah ya kwamba: inadi na ukaidi wa kuikataa haki hauna mwisho mwingine isipokuwa kufikwa na adhabu ya Mola. Ni kama zilivyokuwa baadhi ya kaumu zilizopita, ambazo licha ya kuusikia wito wa Mitume wa Allah na kuishuhudia miujiza yao kwa macho yao lakini ziliamua kukufuru. Katika kuhalalisha upingaji wao, watu hao walikuwa wakimwambia Mtume wao: Kama unataka tukuamini, itabidi utuonyeshe na sisi pia tuwaone hao malaika wanaokuteremkia na kukuletea wahyi. Lakini kwa kuwa huwezi kulifanya hilo hatutakuamini wewe mwenyewe, wala wito unaolingania, kwa hivyo tutabaki kwenye ukafiri wetu. Ni wazi kwamba, upinzani huo wa kiinadi hupelekea watu kushukiwa na adhabu ya Mwenyezi Mungu; na vitu vya kimaumbile, ambavyo ni dhihirisho la urehemevu wa Allah hugeuka kuwa sababu ya maangamizi kwa watu kama hao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, moja ya majukumu ya Mitume ni kuwapa maonyo na indhari watu kuhusu mwisho mbaya wa matendo yao maovu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, si adhabu zote zimewekwa kwa ajili ya akhera peke yake. Baadhi ya adhabu huteremshwa papa hapa duniani. Kwa hivyo tujihadhari matendo yetu maovu na machafu yasije yakatufanya tuhasirike duniani na akhera. Vile vile tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, Mwenyezi Mungu anatimiza dhima yake kwa watu kupitia Mitume wake ili wasije wakatafuta udhuru na kisingizio cha kutetea shirki na ukafiri wao. Utaratibu alioweka Allah ni kutowaadhibu wapinzani na wakanushaji kabla ya kuwatimizia dhima ya kuwafikishia wito wa uongofu. Halikadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa, ujumbe mkuu wa wito wa Mitume ulikuwa ni kuwalingania watu tauhidi na kumwabudu Mola pekee wa haki. Kwa hivyo hakuna Mtume yeyote aliyewalingania watu kumwabudu na kumtii yeye.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 15 na 16 ambazo zinasema:
فَأَمَّا عَادٌ فَاسْتَكْبَرُوا فِي الْأَرْضِ بِغَيْرِ الْحَقِّ وَقَالُوا مَنْ أَشَدُّ مِنَّا قُوَّةً ۖ أَوَلَمْ يَرَوْا أَنَّ اللَّهَ الَّذِي خَلَقَهُمْ هُوَ أَشَدُّ مِنْهُمْ قُوَّةً ۖ وَكَانُوا بِآيَاتِنَا يَجْحَدُونَ
Ama kina A'di walitakabari katika ardhi bila ya haki, na wakasema: Nani aliye na nguvu kushinda sisi? Kwani wao hawakuona kwamba Mwenyezi Mungu aliye waumba ni Mwenye nguvu kushinda wao? Na wao wakawa wanazikataa Ishara zetu!
فَأَرْسَلْنَا عَلَيْهِمْ رِيحًا صَرْصَرًا فِي أَيَّامٍ نَّحِسَاتٍ لِّنُذِيقَهُمْ عَذَابَ الْخِزْيِ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ۖ وَلَعَذَابُ الْآخِرَةِ أَخْزَىٰ ۖ وَهُمْ لَا يُنصَرُونَ
Basi tuliwapelekea upepo wa kimbunga katika siku za nuhusi, ili tuwaonjeshe adhabu ya kuwahizi katika uhai wa duniani, na bila ya shaka adhabu ya Akhera ina hizaya zaidi, na wala wao hawatanusuriwa.
Aya hizi zinaendeleza maudhui iliyozungumziwa katika aya zilizotangulia zilizozitaja kaumu za A'di na Thamudi kwa kuashiria kukufuru kwao na aina ya adhabu iliyowafika. Watu wa kaumu ya A'di walikuwa wakiishi kusini mwa Saudi Arabia ya leo. Wao walikuwa wapiganaji vita hodari na walikuwa na nguvu na utajiri mwingi. Walijenga majengo ya makazi yao kwenye sehemu za miinuko na walikuwa na ngome madhubuti na makasri mazuri na ya kupendeza. Watu wa kaumu ya A'di walijiona bora kuliko watu wote na wakadhani hakuna yeyote wa kuwashinda wao. Dhana hiyo iliwatia uasi na ghururi. Kwa hivyo wakati Mtume wao Hud (as) alipowalingania wito wa Allah walimjibu kwa ghururi na kiburi: "Wewe ni nani hata utuonye sisi kwamba tutashukiwa na adhabu kwa kukaidi amri za Mwenyezi Mungu? Hivi yupo yeyote mwenye nguvu za kutushinda au kutuangamiza sisi?" Kwa kweli mvinyo wa nguvu na wingi wa watu wao ulikuwa umeilevya kaumu ya A'di mpaka wakawa hawajali kumwasi, kumpinga na kumkadhibisha Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Lakini walichokuwa wameghafilika nacho ni kwamba Mola aliyewaumba ana nguvu na uwezo mkubwa zaidi ya walionao wao. Yeye si Muumba wao tu, bali pia ni Muumba wa mbingu na ardhi; na kimsingi ni kwamba nguvu za wanadamu haziwezi kulinganishwa na Yeye Allah SWT. Alla kulli hal, adhabu ya hizaya na ya kudhalilisha iliwashukia watu wa kaumu hiyo kutokana na uasi na ukaidi wao. Kwa muda wa wiki nzima upepo mkali na wa kutisha uliwavumia katika siku za ukorofi ukaziteketeza na kuziangamiza nyumba, mashamba na kila kitu cha watu hao waliokuwa wakijiona na kujivuna. Mwisho wake hakukuwa na kilichosalia zaidi ya magofu na mabaki ya makasri yao ya fahari, maisha yao ya starehe na mali zao zilizokithiri. Na hiyo ilikuwa adhabu ya duniani tu; bila shaka adhabu ya akhera itakuwa ya hizaya na ya kufedhehesha zaidi, na wala hakutakuwa na yeyote wa kuweza kuwasaidia watu hao. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, ukafiri na ukanushaji unaofanywa kwa sababu ya kiburi na ghururi una adhabu ya duniani pia. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kuwa na ghururi kwa sababu ya nguvu na madaraka ni hatari inayomnyemelea kila mtu na kila jamii; na matokeo yake ni kufikwa na hizaya na madhila papa hapa duniani. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, katika hali zote mbili, vitu vyote vya ulimwengu wa maumbile ni watekelezaji wa amri za Mwenyezi Mungu kwa kufanya lile atakalo Yeye Mola; iwe ni katika kuteremshiwa watu neema za Allah au kushukiwa na adhabu yake. Halikadhalika aya hizi zinatutaka tujue kwamba, nyakati zinapoteremka rehma za Mwenyezi Mungu ni za heri na baraka, na nyakati yanaposhuka mabalaa na adhabu ya Mola ni za nuhusi na ukorofi.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 17 na 18 ambazo zinasema:
وَأَمَّا ثَمُودُ فَهَدَيْنَاهُمْ فَاسْتَحَبُّوا الْعَمَىٰ عَلَى الْهُدَىٰ فَأَخَذَتْهُمْ صَاعِقَةُ الْعَذَابِ الْهُونِ بِمَا كَانُوا يَكْسِبُونَ
Na ama Thamudi tuliwaongoza, lakini walistahabu upofu kuliko uwongofu. Basi uliwachukua moto wa adhabu ya kuwafedhehi kwa sababu ya yale waliyo kuwa wakiyachuma.
وَنَجَّيْنَا الَّذِينَ آمَنُوا وَكَانُوا يَتَّقُونَ
Na tukawaokoa walio amini na wakawa wanamcha-mngu.
Baada ya kaumu ya A'di, aya tulizosoma zinazungumzia ulivyokuwa mwisho wa kaumu ya Thamudi. Watu wa kaumu hiyo walikuwa wakiishi kaskazini ya Saudi Arabia; na wao pia walikuwa wakijenga katikakati ya milima majengo imara na madhubuti; na walikuwa na ardhi zenye rutuba, zilizootesha mimea na miti ya kijani kibichi na konde na bustani zilizonawiri. Kuhusu kaumu ya Thamudi, Mwenyezi Mungu SWT anasema: Kaumu hiyo pia tuliifikishia uongofu kama tulivyozifanyia kaumu zingine na tukamtuma Saleh kwa ajili ya kuufikisha uongofu huo kwa watu hao. Nabii Saleh aliwaendea watu wake na mantiki na hoja za wazi pamoja na muujiza utokao kwetu. Lakini badala ya watu wake kuyakubali maneno ya Mtume wao waliyapinga na kuyakadhibisha wakafadhalisha kuzitia upofu nyoyo zao badala ya kuutambua ukweli na wakakataa kuikubali haki. Kwa kuwa upinzani wa watu wa kaumu hiyo ulitokana na ghururi iliyosababishwa na inadi na ukaidi; na si kwa sababu ya ujinga na kutoelewa ukweli, walifikwa na adhabu kali na ya kudhalilisha papa hapa duniani. Radi ya kutisha iliunguza na kuangamiza mji na maskani yao. Radi hiyo haikuwa ngurumo na umweso tu wa kutisha bali iliandamana na tetemeko kubwa la ardhi lililobirua kila kitu juu chini na kukiangamiza. Lakini wale walioamini na kutenda mema hawakujumuishwa kwenye adhabu hiyo iliyowashukia makafiri. Mwenyezi Mungu aliwaokoa waja wake hao na adhabu hiyo kali na ya kutisha. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, ukafiri ni ishara ya moyo uliopofuka; na kung’ang’ania ukafiri na upotofu kuna mwisho mbaya kwa mtu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, rehma au adhabu ya Mwenyezi Mungu inafuata kanuni na utaratibu; na ukweli ni kwamba ni natija na matunda ya amali za mtu mwenyewe. Imani na usafi wa nafsi ndio siri ya uokovu; na dhambi na ukafiri ndio sababu ya maangamizi. Wapenzi wasikilizaji darsa ya 876 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atupe mema duniani na akatupe mema akhera na atulinde na adhabu ya moto. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/