Sura ya Fuss’ilat, aya ya 24-28 (Darsa ya 878)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 878 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 41 ya Fuss’ilat. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 24 na 25 za sura hiyo ambazo zinasema:
فَإِن يَصْبِرُوا فَالنَّارُ مَثْوًى لَّهُمْ ۖ وَإِن يَسْتَعْتِبُوا فَمَا هُم مِّنَ الْمُعْتَبِينَ
Basi wakisubiri Moto ndio maskani yao. Na wakiomba radhi hawakubaliwi.
وَقَيَّضْنَا لَهُمْ قُرَنَاءَ فَزَيَّنُوا لَهُم مَّا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ وَحَقَّ عَلَيْهِمُ الْقَوْلُ فِي أُمَمٍ قَدْ خَلَتْ مِن قَبْلِهِم مِّنَ الْجِنِّ وَالْإِنسِ ۖ إِنَّهُمْ كَانُوا خَاسِرِينَ
Na tukawawekea marafiki, na wakawapambia yaliyo mbele yao na nyuma yao. Basi ikawathibitikia kauli wawe pamoja na umma zilizopita kabla yao, miongoni mwa majini na watu. Hakika hao wamekuwa ni wenye kukhasirika.
Aya hizi zinaendeleza yale tuliyozungumzia katika darsa iliyopita kwa kuashiria jinsi rafiki mbaya na mwenza muovu anavyochangia kumfanya mtu ahasirike na kuwa na mwisho mbaya huko akhera. Aya ya 24 inasema, Siku ya Kiyama, si siku ya kupokelewa udhuru na uombaji msamaha wa wafanyamadhambi, kwa sababu uombaji radhi huo utakuwa umetokana na kuuona moto wa Jahanamu na wa hali ya kulazimika si kwa hiari ya mtu. Kwa hivyo hakutakuwa na tofauti katika hali za watu hao kama wataistahamili na kuivumilia adhabu; na hata kama watatoa udhuru na kuomba msamaha, hautawafalia kitu na makazi yao yatakuwa ni motoni tu. Kisha aya zinaendelea kueleza kwamba, chanzo cha kufikwa na adhabu hiyo kali ni kuchagua rafiki na wenza wenye fikra chafu na mienendo miovu wakati walipokuwa duniani. Hao ni marafiki na wenza ambao, wakati mtu anapofanya mambo maovu, badala ya kumnasihi na kumpa ukumbusho wa kumtaka ayawache wanamshajiisha na kumhamasisha aendelee kufanya matendo na mambo hayo; na kiukweli ni kwamba, wanayapamba maovu hayo yaonekane mazuri na ya kupendeza. Marafiki hao laghai na waovu wanawazunguka watu kila upande na kuzihodhi fikra zao, kiasi cha kuwafanya wasiwe na uwezo hata wa kupambanua kati ya zuri na baya. Waliwapindulia hakika ya mambo juu chini na kuyafanya maovu yaonekane mazuri mbele ya macho yao. Kwa hiyo matokeo ya kuchagua rafiki mbaya ni mtu kutumbukia kwenye dimbwi la ufisadi. Kutokana na kuwa na mtazamo huo potofu, si tu mtu anajijengea msingi mbovu wa maisha yake ya hapa duniani, lakini kwa kuendelea kufuata njia hiyo, anauharibu pia mustakabali wake wa huko akhera na kujifungia mwenyewe mlango wa uokovu. Njia hiyo tab’an waliifuata pia watu wengine wengi kabla yao, na haikuwafikisha kwenye hatima nyingine isipokuwa kuishia kwenye moto wa Jahanamu.
Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, madamu tungaliko duniani, tujue kwamba tungali nayo fursa ya kutubia kwa Mola wetu, lakini tutakapofika akhera hakutakuwa na njia tena ya kutubia, kuomba radhi au kuweza kurudi tena duniani. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, tujihadhari tusije tukatekwa na marafiki wabaya na waovu, kwa sababu wataziathiri fikra na shakhsia zetu na mwisho wake tutaishia kuwa pamoja nao kwenye adhabu ya moto. Halikadhalika aya hizi zinatuelimisha kwamba, mtu anayesifia maovu tunayofanya si rafiki wa kweli, bali ni shetani aliye katika sura ya binadamu, kwa sababu yeye ni mithili ya shetani anayeyafanya maovu yaonekane mazuri mbele ya macho ya watu. Vilevile aya hizi zinatutaka tujue kwamba, kuporomoka kwa mtu hufanyika taratibu na hatua kwa hatua. Katika hatua ya kwanza, rafiki wabaya humpambia maovu yakaonekana mazuri mbele ya macho yake. Matokeo yake ni mtu kushughulishwa na maovu hayo, akaendelea kuyaogelea mpaka hatimaye akahasirika na kuwa na hatima na mwisho mbaya. Wa aidha aya hizi zinatuelimisha kwamba, rafiki mbaya hamuongezei mtu chochote, bali huwa sababu ya kupotoka na kuhasirika duniani na akhera.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 26 hadi 28 za sura yetu hii ya Fuss’ilat ambazo zinasema:
وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا لَا تَسْمَعُوا لِهَٰذَا الْقُرْآنِ وَالْغَوْا فِيهِ لَعَلَّكُمْ تَغْلِبُونَ
Na walio kufuru walisema: Msiisikilize Qur'ani hii, na timueni zogo, huenda mkashinda.
فَلَنُذِيقَنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا عَذَابًا شَدِيدًا وَلَنَجْزِيَنَّهُمْ أَسْوَأَ الَّذِي كَانُوا يَعْمَلُونَ
Basi hapana shaka tutawaonjesha hao walio kufuru adhabu kali, na hapana shaka tutawalipa malipo mabaya ya yale waliyo kuwa wakiyafanya.
ذَٰلِكَ جَزَاءُ أَعْدَاءِ اللَّهِ النَّارُ ۖ لَهُمْ فِيهَا دَارُ الْخُلْدِ ۖ جَزَاءً بِمَا كَانُوا بِآيَاتِنَا يَجْحَدُونَ
Hayo ndiyo malipo ya Maadui wa Mwenyezi Mungu - Moto! Humo watakuwa na maskani ya kudumu, ndiyo malipo yao kwa sababu walikuwa wakizikataa Ishara zetu.
Aya hizi zinaashiria moja ya maovu ambayo washirikina wa Makka walikuwa wakimfanyia Bwana Mtume Muhammad SAW na kueleza kwamba kila pale Bwana Mtume alipokuwa akiwasomea watu aya zenye kuvutia na kusisimua nyoyo za Qur’ani, baadhi ya washirikina walikuwa wakipiga vikorombwe au kusoma mashairi kwa sauti kubwa ili kisomo cha Qur’ani cha mtukufu huyo kisiwafikie watu wakaiamini haki. Leo hii pia mwenendo huo unaendelezwa kwa njia na sura tofauti. Sababu ni kwamba maadui wa haki wanatambua kuwa, endapo watu wataujua ukweli wa mafundisho matukufu ya Qur’ani, wengi wao watauamini na kuufuata. Kwa hivyo hutumia vyombo vyao vikubwa vya habari na uenezi walivyonavyo na kueneza sumu ya makelele na propaganda ili hakika na ukweli wa Qur’ani na Uislamu usiwafikie walimwengu. Ili kufikia lengo hilo, huwa wanatumia njia za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja. Hutumia nyenzo kama filamu, tamthilia, uchoraji, katuni pamoja na uandishi wa vitabu vya hadithi na riwaya ili kuzifanyia shere na stihzai thamani za kidini. Maadui hao wa haki hueneza pia taarifa potofu na zisizo na ukweli kuhusu dini pamoja na kuzusha tuhuma na mambo yenye utata kwa lengo la kuchafua sura ya Uislamu ili kuwazuilia walimwengu kuikubali dini hiyo ya haki. Hata hivyo, hiyo ni dhana hewa waliyonayo maadui hao, ya kudhani na kutaraji kwamba kwa kufanya hivyo wataweza kuuzuia Uislamu usienee ulimwenguni. Hapana shaka, sifa maalumu iliyonayo haki ni kuviondoa vizuizi inavyowekewa kimoja baada ya kingine na kufungua njia ya kutangaza ukweli wake. Na ndiyo maana ukweli wa Qur’ani unazidi kuwadhihirikia walimwengu siku baada ya siku. Ni wazi pia kwamba, adhabu kali ya Allah inawaongejea watu wanaowazuilia watu wengine wasizisikie aya za Mwenyezi Mungu na kutaka watu wengine pia wabaki kwenye upotofu kama walivyo wao. Watu wanaozikanusha kila mara aya za wito wa haki, kwa hakika ni maadui wa Allah na dini yake. Bila ya shaka adhabu ya watu hao kulingana na amali hizo mbaya sana walizofanya, itakuwa kali na ya kuumiza mno na hawatapata njia ya kuwaepusha na moto wa Jahanamu. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kwa kawaida, watu wasio na maneno ya mantiki na yenye hoja, hutumia visingizio mbalimbali ili kuwazuia watu wasisikilize maneno ya mantiki yasemwayo na wengine. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, Qur’ani ina mvuto na taathira maalumu, kiasi kwamba hata kuzisikia tu aya zake kunaweza kuzivuta nyoyo na kuzielekeza kwa Allah. Ndiyo maana maadui wanawazuilia watu kuyasikia maneno hayo ya wahyi. Halikadhalika aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba, maadui hutumia nyenzo na suhula tofauti na kuendesha kampeni za propaganda chafu ili kuzuia ukweli wa Qur’ani na Uislamu usiweze kuwafikia walimwengu. Wa aidha aya hizi zinatuelimisha kuwa, adhabu ya milele ya moto imeandaliwa kwa watu wanaoamua kwa makusudi na kwa uelewa kamili kuipiga vita haki; na hiyo ndiyo adhabu ya uadilifu kwa watu kama hao. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 878 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuwezeshe kuufikisha wito wa haki kwa walimwengu wote na autawalishe Uislamu duniani kote ili heri na saada ipatikane kwa wanadamu wote. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/