Sura ya Al-Jaathiya, aya ya 26-32 (Darsa ya 919)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 919 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 45 ya Al-Jaathiya. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 26 na 27 za sura hiyo ambazo zinasema:
قُلِ اللَّهُ يُحْيِيكُمْ ثُمَّ يُمِيتُكُمْ ثُمَّ يَجْمَعُكُمْ إِلَىٰ يَوْمِ الْقِيَامَةِ لَا رَيْبَ فِيهِ وَلَٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ
Sema: Mwenyezi Mungu anakuhuisheni, kisha anakufisheni, kisha atakukusanyeni Siku ya Kiyama isiyo na shaka. Lakini watu wengi hawajui.
وَلِلَّهِ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ وَيَوْمَ تَقُومُ السَّاعَةُ يَوْمَئِذٍ يَخْسَرُ الْمُبْطِلُونَ
Na ni wa Mwenyezi Mungu ufalme wa mbingu na ardhi. Na siku kitakapotokea Kiyama, siku hiyo washikao batili watahasirika.
Katika darsa iliyopita tuliwazungumzia wakanushaji wa maadi, yaani kufufuliwa kwa viumbe, ambao walimtaka Bwana Mtume SAW na waumini wawafufue wazee wao waliopita ndipo wao waamini Kiyama. Aya ya 26 tuliyosoma inawajibu watu hao kwa kuwaambia: Nyinyi wenyewe ambao mko hai sasa hivi, amekuumbeni nani na akakupeni uhai? Kwa hiyo mnamkanusha hata Muumba wenu pia? Kama mnaamini kwamba yuko aliyekuumbeni, kwa nini hamkubali kuwa huyohuyo Muumba wenu anao uwezo wa kukufufueni tena? Kwa nini badala ya kutaamali na kutumia akili, mnataka kila jambo mlione kwa macho tu? Kisha aya inayofuatia inatilia mkazo nukta ya kwamba, ikiwa mna shaka juu ya uwezo wa Mwenyezi Mungu wa kuumba tena, hebu angalieni tu adhama ya mbingu na ardhi ili muweze kujua, ni jambo la hakika kabisa, kwamba mwenye uwezo wa kuumba ulimwengu huu wenye adhama, na ambaye ndiye mmiliki na mtawala wa ulimwengu wote wa uumbaji, katu hatoweza kushindwa kukuumbeni nyinyi tena. Basi jihadharini, msifuate batili badala ya haki, kwa sababu mtakuja kujuta na kuhasirika Siku ya Kiyama. Sababu ni kuwa mtapoiharibu rasilimali yenu ya umri, hamtaambulia kingine chochote zaidi ya majonzi na majuto. Bila ya shaka umri anaojaaliwa mtu, pamoja na akili, kipaji na ufahamu wa mambo ndio mtaji na rasilimali yake ya hapa duniani, lakini wanaofuata batili wanaziacha rasilimali hizo kwa vitu vya kupita. Kwa hivyo Siku ya Kiyama, ambapo haitamfalia mtu isipokuwa imani sahihi na amali njema, watakuja kubaini watu watakavyohasirika kutokana na waliyoyafanya. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, maisha ya mara ya kwanza ya mwanadamu ni hoja ya kuthibitisha uwezekano wa kupewa uhai tena kiumbe huyo Siku ya Kiyama. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, akthari ya watu, badala ya kutafakari juu ya ishara za uumbaji, hutarajia kuona kila kitu kwa macho yao, ndipo waukubali ukweli na haki. Halikadhalika aya hizi zinatutaka tujue kwamba, wale wanaokadhibisha Kiyama na kuitakidi kuwa ni batili, siku kitakaposimama, watabaini kuwa wamehasirika na kupata hasara kubwa iliyoje!
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 28 na 29 ambazo zinasema:
وَتَرَىٰ كُلَّ أُمَّةٍ جَاثِيَةً ۚ كُلُّ أُمَّةٍ تُدْعَىٰ إِلَىٰ كِتَابِهَا الْيَوْمَ تُجْزَوْنَ مَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ
Na utauona kila umma umepiga magoti, na kila umma utaitwa (kwenda kusoma) kitabu chake (waambiwe): Leo mtalipwa yale mliyo kuwa mkiyatenda.
هَٰذَا كِتَابُنَا يَنطِقُ عَلَيْكُم بِالْحَقِّ ۚ إِنَّا كُنَّا نَسْتَنسِخُ مَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ
Hiki kitabu chetu kinasema juu yenu kwa haki. Hakika Sisi tulikuwa tukiyaandika mliyo kuwa mkiyatenda.
Aya hizi zinatoa taswira ya mahakama ya Siku ya Kiyama, ambapo kutokana na hofu, woga na wasiwasi watakaokuwa nao watu, watapiga magoti siku hiyo wakingojea kuona nini itakuwa hatima yao. Katika kubainisha jinsi hali itakavyokuwa, aya zinasema, kila umma utaitwa kwenda kusoma kitabu chake. Daftari la amali za kila mtu litakuwa limeshawekwa tayari; kwa sababu, kwa muda wote wa uhai wa kila mtu, Malaika wa Mwenyezi Mungu walikuwa wakifanya kazi ya kuhifadhi kila jema na baya alilokuwa akilifanya, pasi na kupitwa na chochote; kwa hivyo siku hiyo katika mahakama ya Kiyama, kila mtu atakabidhiwa nakala ya daftari hilo la amali zake, ili asije akadhani analipwa thawabu au anapewa adhabu, bila sababu yoyote. Kisha baada ya hapo, Allah SWT atawahutubu waja wake ya kwamba: hiki ni kitabu chetu kinachoeleza kwa haki juu yenu na kuweka wazi amali na matendo yenu. Wakati wa uhai wenu mlifanya kila mlichotaka na hamkuwa mkiamini abadani kwamba, kuna mahali amali zenu zinasajiliwa na kuhifadhiwa; lakini Sisi tulikuwa tumewaamuru malaika wetu wazisajili na kuzihifadhi amali zenu zote mnazofanya. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, mfumo wa maumbile unaendeshwa kwa msingi wa haki na uadilifu na unafanya kazi kwa nidhamu na mahesabu maalumu; na amali na matendo yote ya mtu yanarekodiwa na kuhifadhiwa. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, msingi wa malipo ya thawabu au adhabu watakayolipwa watu Siku ya Kiyama utakuwa ni amali zao njema au mbaya walizofanya hapa duniani. Vilevile aya hizi zinatutaka tufahamu kwamba, kila mtu ana faili ambalo ndani yake yanahifadhiwa kwa umakini na kulingana na uhalisia, amali na matendo yake yote. Hapana shaka, kuamini mtu kwamba kila afanyalo huwa halipotei bali linahifadhiwa kama lilivyo, ni chachu kubwa ya kumzuia kufanya maasi na madhambi.
Ifuatayo sasa ni aya ya 30 na 31 za sura yetu ya Al Jaathiya ambazo zinasema:
فَأَمَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ فَيُدْخِلُهُمْ رَبُّهُمْ فِي رَحْمَتِهِ ۚ ذَٰلِكَ هُوَ الْفَوْزُ الْمُبِينُ
Ama wale walio amini na wakatenda mema, Mola wao Mlezi atawaingiza katika rehema yake. Huko ndiko kufuzu kuliko dhahiri.
وَأَمَّا الَّذِينَ كَفَرُوا أَفَلَمْ تَكُنْ آيَاتِي تُتْلَىٰ عَلَيْكُمْ فَاسْتَكْبَرْتُمْ وَكُنتُمْ قَوْمًا مُّجْرِمِينَ
Na ama wale walio kufuru, (wataambiwa): Kwani hamkuwa mkisomewa Aya zangu nanyi mkawa na kiburi, na mkawa watu waovu?
Baada ya kukamilishwa kazi ya mahakama ya Kiyama, watu wote watagawanyika katika makundi mawili; na kila kundi litalipwa malipo ya amali zake. Kundi la kwanza ni la waumini wafanya mema; na kundi la pili ni la makafiri wafanya maovu. Waliokuwa waumini, watapata rehma maalumu za Allah SWT, ambazo ni saada na fanaka ya duniani na akhera; na huko ni kufuzu kuliko dhahiri kabisa. Bila ya shaka, baada ya kuhesabiwa amali za watu, watakaopata rehma hizo za Mola Mwenyezi na neema zisizo na kifani, ni wale ambao, mbali na kuamini, watakuwa na rasilimali ya amali njema pia. Ama kwa upande wa makafiri, wao wataulizwa, kwani nyinyi hamkuwa mkisomewa aya zangu, lakini mkatakabari na kuasi? Kwa hivyo watu hao watakosa rehma za Mwenyezi Mungu na wataishia kwenye hilaki na maangamizi. Sababu ni kwamba, badala ya kuitafuta na kuikubali haki, walisimama kuyapinga maneno ya Mwenyezi Mungu na kuyapa mgongo; na katika matendo yao pia waliamua kufanya kila aina ya maasi na madhambi. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, imani na amali njema hazitenganishiki, wala kila kimoja peke yake hakiwezi kumfanya mtu apate saada na kufuzu akhera. Ni imani inayoambatana na amali njema, ndiyo inayomletea saada na fanaka mtu na jamii kwa ujumla. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, chimbuko la ukafiri ni kuasi na kutakabari mbele ya haki. Wa aidha tunabainikiwa kutokana na aya hizi kwamba, chanzo cha mtu kufanya maovu na madhambi ni kumkanusha Mwenyezi Mungu na kukaidi kutekeleza amri zake.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 32 ambayo inasema:
وَإِذَا قِيلَ إِنَّ وَعْدَ اللَّهِ حَقٌّ وَالسَّاعَةُ لَا رَيْبَ فِيهَا قُلْتُم مَّا نَدْرِي مَا السَّاعَةُ إِن نَّظُنُّ إِلَّا ظَنًّا وَمَا نَحْنُ بِمُسْتَيْقِنِينَ
Na iliposemwa: Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni kweli, na Kiyama hakina shaka, nyinyi mkisema: Hatujui Kiyama ni nini, hatudhani ila dhana tupu , wala hatuna yakini.
Baada ya aya zilizotangulia kuzungumzia kiburi, ukaidi na inadi ya makafiri mbele ya aya za Mwenyezi Mungu, aya hii tuliyosoma inasema: alama ya kutakabari kwenu ni kwamba kila pale waumini walipokuwa wakizungumzia kuthibiti kwa Kiyama na kuku kumbusheni juu ya tukio hilo, badala ya kutafakari na kulizingatia hilo mlikuwa mkisema: Ndo kitu gani hicho Kiyama? Nani aliyekiona au kusimulia hata sisi tuamini? Maneno mnayosema nyinyi mlioamini pia hayana thamani yoyote kwetu, zaidi ya kuwa ni mawazo na dhana tu; na sisi hatuna ujuzi wa yakini kuhusu Kiyama. Ajabu ni kuwa, kama watu haohao wataambiwa: kuna hatari kama ya moto ambayo inaweza kusababisha nyumba zenu kuungua, hapohapo watakuwa tayari kuchukua hatua haraka za tahadhari ili kuzuia hatari hiyo isitokee, lakini kuhusiana na Kiyama, hawakuwa tayari kutilia maanani hata uwezekano tu wa kwamba, kunaweza kukawa na ukweli juu ya hilo. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, waumini inawapasa wawafikishie watu wote neno la haki, ili wawe wametimiza dhima kwao, hata kama akthari ya watu hawataamini. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, si lazima mtu awe na yakini juu ya Kiyama; hata dhana na kuchukulia tu kwamba kinaweza kuthibiti, kunapasa kuwe chachu ya kuizuia nafsi yake kufanya maovu na madhambi, kwa sababu hatari na madhara yake ni makubwa mno. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 919 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azifanye thabiti imani zetu, atughufirie madhambi yetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/