Sura ya Al-Ah'qaaf, aya ya 1-5 (Darsa ya 921)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 921. Baada ya kukamilisha tarjumi na maelezo ya sura ya 45 ya Al-Jaathiya, katika darsa hii tutaanza kutoa tarjumi na maelezo kwa muhtasari ya sura ya 46 ya Al-Ah'qaaf. Ardhi ya watu wa kaumu ya Aad ilikuwa ikiitwa Ah'qaaf kwa sababu ilikuwa ya mchanga wa changarawe. In shaa Allah tutakuja kuzungumzia habari za kaumu ya Aad katika aya ya 21 ya sura hii. Tunaianza basi darsa yetu hii kwa aya ya kwanza hadi ya tatu ya sura yetu ya Ah'qaaf ambazo zinasema:
حم
H'A MIM
تَنزِيلُ الْكِتَابِ مِنَ اللَّهِ الْعَزِيزِ الْحَكِيمِ
Uteremsho wa Kitabu umetoka kwa Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
مَا خَلَقْنَا السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا إِلَّا بِالْحَقِّ وَأَجَلٍ مُّسَمًّى ۚ وَالَّذِينَ كَفَرُوا عَمَّا أُنذِرُوا مُعْرِضُونَ
Hatukuziumba mbingu na ardhi wala yaliyomo baina ya viwili hivyo ila kwa haki na kwa muda maalumu. Na wale walio kufuru wanayapuuza yale wanayo onywa.
Sura hii, nayo pia kama zilivyo sura zingine 28 za Qur'ani tukufu imeanza kwa herufi za mkato; na kama zilivyo sura hizo, baada ya kutajwa herufi hizo, umezungumziwa umuhimu na adhama ya Qur'ani tukufu. Ni kama kwamba Allah SWT anataka kutuambia: Mimi nimeteremsha kitabu kutokana na herufi hizi hizi za alfabeti mnazotumia nyinyi pia; kitabu ambacho nyinyi hamna uwezo wa kuleta mfano wake; na hii ni hoja madhubuti zaidi ya kuthibitisha kuwa Qur'ani ni muujiza. Sisitizo kwamba Qur'ani imeteremshwa na Mwenyezi Mungu mwenye izza na hekima, ambalo limebainishwa katika aya kadhaa za Qur'ani, linadhihirisha hadhi na nafasi ya kitabu hiki cha mbinguni, kitabu ambacho, kutekeleza mafundisho yake kunampa mtu nguvu na izza. Kwa sababu, mafunzo na mafundisho yote ya Qur'ani yanatokana na elimu na hekima, na halipatikani ndani ya kitabu hicho neno, amri au katazo lolote la porojo na upuuzi. Na si upande wake wa hukumu na sharia pekee, bali mfumo mzima wa maumbile umeumbwa juu ya msingi wa haki na unaendeshwa kwa kufuata mpango na muda maalumu; na kila kitu katika mfumo huo kina nafasi yake makhsusi. Hapana shaka, si ndani ya kitabu hicho cha mbinguni linaweza kupatikana neno hata moja linalokinzana na haki, wala si katika majimui yote ya ulimwengu wa uumbaji wa Allah kinaweza kuonekana kitu chochote kisicho na mlingano au kinachopingana na haki. Vyote hivyo vina mlingano na uwiyano na vinaendana na haki. Lakini kama uumbaji huo ulivyokuwa na mwanzo wake, umewekewa pia hatima na mwisho wake, ambao utakapowadia, dunia yote itatoweka. Bila shaka watu wanaokanusha kuwepo Mwenyezi Mungu na kutumwa Mitume, wanazipuuza aya za Mwenyezi Mungu ndani ya Qur'ani, mfumo wa uumbaji na maonyo yatokanayo na akili na wahyi. Wao wanajiweka mbali na haki na kuipa mgongo; matokeo yake, ni wao wenyewe kujinyima na kujikosesha uongofu wa Mwenyezi Mungu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, Qur'ani ni maneno ya Mwenyezi Mungu yaliyoteremshwa kwenye moyo wa Bwana Mtume Muhammad SAW na kutamkwa kupitia kinywa cha mtukufu huyo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, mfumo wa maumbile na hukumu na sharia za dini, vyote viwili vinatokana na haki na hikma, kwa sababu vyote viwili chimbuko na asili yao ni Mwenyezi Mungu Mjuzi na Mwenye Hikima. Aidha, aya hizi zinatutaka tujue kwamba hakuna lolote pogo, la upotofu au la upuuzi katika mfumo wa uumbaji. Vilevile aya hizi zinatuelimisha kuwa mbingu na ardhi na vingine vyote vilivyopo vimewekewa muda maalumu na wenye makadirio na hakuna jambo lolote linalotokea kwa sadfa na bahati tu. Halikadhalika aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba, ulimwengu wote wa uumbaji uko katika mwendo unaopita kwenye njia na mkondo wa haki. Ni mwanadamu peke yake, ambaye kwa kuchagua njia isiyo sahihi, ndiye anayeamua kukengeuka mkondo huo wa haki na kufuata upotofu.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya nne na ya tano za sura yetu ya Ah'qaaf ambazo zinasema:
قُلْ أَرَأَيْتُم مَّا تَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّهِ أَرُونِي مَاذَا خَلَقُوا مِنَ الْأَرْضِ أَمْ لَهُمْ شِرْكٌ فِي السَّمَاوَاتِ ۖ ائْتُونِي بِكِتَابٍ مِّن قَبْلِ هَٰذَا أَوْ أَثَارَةٍ مِّنْ عِلْمٍ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ
Sema: Je! Mnawaona wale mnao waomba badala ya Mwenyezi Mungu? Nionyesheni wameumba nini katika ardhi; au hao wanayo shirika katika mbingu? Nileteeni Kitabu kilicho kuwa kabla ya hiki, au athari yoyote ya ilimu, ikiwa mnasema kweli.
وَمَنْ أَضَلُّ مِمَّن يَدْعُو مِن دُونِ اللَّهِ مَن لَّا يَسْتَجِيبُ لَهُ إِلَىٰ يَوْمِ الْقِيَامَةِ وَهُمْ عَن دُعَائِهِمْ غَافِلُونَ
Na ni nani mpotofu mkubwa kuliko yule anayeomba badala ya Mwenyezi Mungu, ambaye hatamwitikia mpaka Siku ya Kiyama, na wala hawatambui maombi yao.
Katika aya hizi tulizosoma, Bwana Mtume Muhammad SAW anatakiwa awaambie na kuwauliza washirikiana wa Makka ya kwamba: haya masanamu mnayoyaabudu yana mchango gani na yameshiriki kwa kiwango gani katika uumbaji na uendeshaji wa mbingu na ardhi? Ikiwa nyinyi wenyewe mnakiri na kukubali kuwa Allah SWT ndiye aliyeumba ardhi na mbingu, jua na mwezi pamoja na nyote zote, ni kwa nini na inakuwaje tena mnayaabudu haya masanamu na kuamua kuviomba vitu hivi visivyo na akili, thamani, wala hisia yoyote, kwa ajili ya kutatuliwa matatizo yenu? Kwani kabla ya Qur'ani, kimekujieni kitabu chochote ambacho kimekupeni idhini ya kuabudu masanamu? Au mumeletewa hoja za kielimu na watu wajuzi na weledi ambazo zimekufanyeni muwaabudu wengineo ghairi ya Mwenyezi Mungu? Kuabudu kwenu masanamu inapasa kutokane na ama hoja ya akili au ya maandiko, wakati nyinyi hamna hoja yoyote kati ya hizo mnayoitegemea. Hivyo ni wazi kwamba imani na itikadi yenu inatokana na dhana hewa na batili. Kisha aya zinaendelea kuwaeleza washirikina ya kwamba, pasi na kuwa na hoja yoyote ya kimantiki na ya kimaandiko, nyinyi mnayaomba masanamu au waabudiwa wengine badala ya Mwenyezi Mungu, ilhali mnajua kwamba wao hawana uwezo wa kuitika maombi yenu wala wa kukidhi na kutekeleza matakwa yenu. Ukweli ni kuwa, nyinyi mumekengeuka njia ya haki na mko kwenye dhalala na upotofu mkubwa. Na sababu ni kwamba mnaviabudu na kuviomba vitu ambavyo hata haviyasikii muyasemayo, wala havina habari au ufahamu wa chochote kile katika mnavyoviomba. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kuchagua kufuata njia nyingine yoyote ile ghairi ya njia ya Muumba wa ulimwengu ni kupotea na kufuata upotofu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, wakati mwingine hulazimu kuwatupia wapinzani masuali ya kichangamoto ili kuwatafakarisha na kuwafanya wabaini na kuelewa udhaifu na kutokuwa na mashiko njia wanayofuata. Halikadhalika aya hizi zinatuelimisha kwamba, si masanamu ya miti na mawe tu, bali hata wanadamu wenye uwezo na ujuzi hawawezi kujitimizia wao wenyewe wala kuwatimizia watu wengine matakwa na mahitaji yao mengi; na haiwezekani kuwaelekea na kuwategemea wao badala ya Mwenyezi Mungu Mola Muumba wa kila kitu. Wa aidha aya hizi zinatutaka tuelewe kuwa, jambo lolote alifanyalo mtu inapasa liwe na hoja ya kiakili au kielimu, au hoja itokanayo na maneno ya Allah SWT au Mtume wake na makhalifa wake maasumu na watoharifu. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 921 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuepushe na kila aina ya shirki, kubwa na ndogo, ya dhahiri na iliyofichika. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/