Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (70)
Assalaamu alaykum wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kujiunga nami tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu ili kwa pamoja tuweze kufungua ukurasa mwingine katika kurasa za historia ya Maulamaa na wanazuoni wa Kishia pamoja na mchango wao katika Uislamu bila kusahau athari na vitabu vyao mashuhuri.
Kipindi chetu kilichotangulia kilimzungumzia Jahangir Khan Ghashghaei. Tulieleza kwamba, alizaliwa 1243 Hijria mwafaka na 1828 Miladia katika moja ya viunga vya mji wa Isfahan nchini Iran. Jahangiri Khan Ghashghaei kama walivyokuwa watoto wengine wa eneo la Qashqai alijifunza mapema kupanda farasi na kulenga shabaha. Kutokana na kuonekana kuwa na kipaji, akili na maarifa ya hali ya juu, baba yake aliamuandalia mazingira ya kujifunza masomo ya msingi. Alimu huyu alikuwa na mchango mkubwa sana katika elimu ya falsafa. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 70 ya mfululizo huu kitamzungumzia mmoja wa shakhsia wakubwa wa ukoo wa Sadr wa Iraq katika karne ya 14 Hijria ni Sayyid Ismail Sadr. Karibuni.
Sayyid Ismail Sadr alizaliwa mwaka 1258 Hijria sawa na 1842 Miladia katika mji wa Isfahan Iran. Sayyid Ismail akiwa na umri wa miaka 6 alianza maisha ya uyatima baada ya baba yake kufariki dunia. Mpaka anafikisha umri wa miaka 14 alikuwa akisoma kwa kaka yake masomo kama fasihi ya lugha ya Kiarabu, fikihi na Usul. Akiwa na umri wa miaka 23 akiwa na hamu na shauku ya kwenda kumuona Shekhe Murtadha Ansari alifunga safari na kuelekea katika mji wa Najaf, Iraq.
Hata hivyo, Shekhe Murtadha Ansari aliaga dunia kabla Sayyid Ismail Sadr kuwasili katika mji huo na hivyo hakufanikiwa kukutana na mwanazuoni huyo. Pamoja na hayo, Sayyid Ismail alibakia katika mji wa Najaf huko Iraq na kushiriki katika masomo na darsa za Mahdi Kashif al-Ghitaa na Mirza Shirazi mkubwa. Alishiriki masomo ya walimu hao kwa takribani miaka 20 na ni miongoni mwa watu wachache ambao Mirza Shirazi Marjaa mkubwa wa Kishia aliwapa kiti chake cha mjadala na cha kufundishia katika kipindi cha miaka kumi ya mwisho wa umri wake na kumkabidhi kazi ya kufundisha na kulea wanafunzi. Baada ya Mirza Shirazi mkubwa, Sayyid Ismail Sadr akiwa na Maulamaa na Marajii wengine pamoja na shakhsia wakubwa wa Iraq alishiriki katika harakati za kijamii na kisiasa.
Mwaka 1316 Hijria (1899 Miladia) kuliasisiwa shirika kwa ajili ya kuwadhaminia Wairani bidhaa za vitambaa na nguo na kuwafanya wasiwe wahitaji wa madola ya kigeni. Sayyid Ismail Sadr akiwa pamoja na Maulamaa wengine wa Iran na Iraq alitoa taarifa ya kuunga mkono shirika hilo na akawashajiisha waliokuwa wakimkalidi kutumia bidhaa za shirika hilo.

Mwaka 1912 Russia iliishambulia kijeshi Iran huku Italia nayo ikipeleka vikosi katika moja ya ardhi za Kiislamu yaani Libya. Sayyid Ismail Sadr, Akhund Khorasani pamoja na Maulamaa na Marajii wengine wa Kishia wa Iran na Iraq walitoa hukumu ya jihadi na wakasema kwamba, ni wajibu kwa kila Mwislamu kutetea ardhi na milki za Kiislamu.
Wanazuoni waliotoa fatuwa walisema katika fatuwa zao hizo kwamba, kuendesha mapambano dhidi ya wavamizi wa ardhi za Kiislamu ni kupigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu na wanaopigana katika njia hiyo ni mithili ya wapiganaji na wanajihadi wa Vita vya Badr na Hunein.
Katika kipindi chote cha historia, daima Maulamaa wa Kiislamu walikuwa wakizingatia na kutoa kipaumbele mno kuhusianan na suala la umoja wa Waislamu na walikuwa wakilitambua hilo kuwa ni jambo muhimu mno. Kwa mtazamo wao ni kuwa, kutozingatia msingi huu, kunaweza kuwa chimbuko la Waislamu kushindwa na adui na hivyo kusambaratisha Uislamu.
Kwa muktadha huo, wakati kulipoanza vita vya kwanza vya Dunia na vikosi vya waitifaki kutangaza vita dhidi ya utawala wa Othmania, Maulamaa wa Kishia, licha ya matatizo yote uliokuwa nao utawala wa Othmania, lakini walitoa fatuwa za kupigana jihadi na kuwa upande wa utawala huo. Wanazuoni hao walieleza kwamba, ni wajibu kwa Waislamu kuendesha vita dhidi ya Uingereza na washirika wake kama ambavyo wao wenyewe na watoto wao walikuwa mstari mbele kabisa katika safu ya mujahidina.

Sayyid Ismail, Akhund Khorasani na Maulamaa wengine wa Kishia walitoa taarifa ya pamoja na kutangaza kuwa, hitilafu za kimadhehebu na kimakundi hazihusiani na misingi ya dini. Katika upande mwingine Aya ya 103 ya Surat al-Imran inasema:
Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane.
Kwa msingi huo Maulamaa wa Kishia wakiwa na lengo la kuhifadhi ardhi za Kiislamu waliungana na Maulamaa wa Kisuni katika fatuwa ya jihadi na wakatumia nguvu zao na ushawishi wao wote kwa ajili ya kulinda na kutetea ardhi za Waislamu. Kwao wao hakukuwa ana tofauti kwamba, ardhi hizo za Kiislamu ziko katika eneo gani la kijigorafia, iwe ni Iran, Libya au ardhi zilizo katika mamlaka ya utawala wa ufalme wa Othmania.
Sayyid Ismail ni babu mkuu wa familia na ukoo wa Sadr nchini Iraq, familia ambayo ilikuwa na taathira muhimu mno katika matukio ya kisiasa na kijamii ya nchi hiyo. Familia hiyo ilikuwa na wanazuoni na Maulamaa watajika na mahiri pia katika nchi za Lebanon na Iran, ambapo tutalizungumzia hilo katika vipindi vyetu vijavyo.
Mwishoni mwa umri wake Sayyid Sadr alihajiri na kuelekea katika mji wa Kadhmein Iraq. Aliishi katika mji huo mpaka alipoaga dunia akiwa na umri wa takribani miaka 80. Hakuna nukuu katika vitabu vya historia inayoeleza siku na tarehe hasa aliyoaga dunia mwanazuoni huyo.
Baadhi ya nukuu za historia zinasema, alifariki dunia 1919 Miladia huku vitabu vingine vikieleza kwamba, aliaga dunia mwaka 1921 Miladia. Kama ilivyo kwa Maulamaa wengine, shughuli ya mazishi ya Sayyid Ismail Sadr ilihudhuriwa na watu wengi wa matabaka mbalimbali ya wananchi na mwili wake umezikwa katika haram tukufu ya Kadhmein huko Iraq.
Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa leo umefikia tamati. Tukutane tena wiki ijayo katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu. Hadi tutakapokutana tena juma lijalo ninakuageni nikikutakieni kila la kheri.
Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh