Sura ya Muhammad, aya ya 1-6 (Darsa ya 928)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 928. Baada ya kukamilisha tarjumi na maelezo ya sura ya 46 ya Al-Ah'qaaf, katika darsa hii tutaanza kutoa tarjumi na maelezo kwa muhtasari ya sura ya 47 ya Muhammad. Sura hii ambayo imepewa jina la Nabii Muhammad SAW, inahusu mlinganisho baina ya makundi mawili ya waumini na makafiri; makundi ambayo yalikuwepo huko nyuma na yataendelea kuwepo kwa muda wote wa historia. Ni wazi kuwa jukumu la waumini ni kuwalingania na kuwaita watu kwenye dini ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake, lakini hawana haki ya kuwalazimisha wasilimu na kuukubali Uislamu. Makafiri, ambao wameshika njia ya batili, daima huwa wanajaribu kutumia kila njia ili kuwazuia waumini wasifuate njia ya Allah. Si ajabu kuwaona wakati mwingine wakitumia mabavu au nguvu za kijeshi kufikia lengo lao hilo. Katika hali kama hiyo ndipo huzuka ugomvi na mapigano kati yao na waumini. Sura hii ya Muhammad, inabainisha kwa uwazi kabisa amri za Allah SWT vinapotokea vita kati ya imani na ukafiri. Baada ya maelezo hayo mafupi tunaianza sasa darsa yetu ya leo kwa aya ya kwanza hadi ya tatu ya sura hiyo ambazo zinasema:
الَّذِينَ كَفَرُوا وَصَدُّوا عَن سَبِيلِ اللَّهِ أَضَلَّ أَعْمَالَهُمْ
Wale walio kufuru na wakazuilia njia ya Mwenyezi Mungu, Yeye atavipotoa vitendo vyao.
وَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَآمَنُوا بِمَا نُزِّلَ عَلَىٰ مُحَمَّدٍ وَهُوَ الْحَقُّ مِن رَّبِّهِمْ ۙ كَفَّرَ عَنْهُمْ سَيِّئَاتِهِمْ وَأَصْلَحَ بَالَهُمْ
Na wale walio amini, na wakatenda mema, na wakaamini aliyo teremshiwa Muhammad - nayo ni Haki iliyo toka kwa Mola wao Mlezi - atawafutia makosa yao na ataitengeneza hali yao.
ذَٰلِكَ بِأَنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا اتَّبَعُوا الْبَاطِلَ وَأَنَّ الَّذِينَ آمَنُوا اتَّبَعُوا الْحَقَّ مِن رَّبِّهِمْ ۚ كَذَٰلِكَ يَضْرِبُ اللَّهُ لِلنَّاسِ أَمْثَالَهُمْ
Hayo ni kwa sababu wale walio kufuru wamefuata upotovu, na walio amini wamefuata Haki iliyo toka kwa Mola wao Mlezi. Namna hivi Mwenyezi Mungu anawapigia watu mifano yao.
Vinara wa ukafiri na shirki huwa daima wanatumia kila njia ili kuongeza idadi ya makafiri wenzao kwa ajili ya kulinda na kuimarisha nafasi yao. Hujaribu kutumia mbinu tofauti ili kuwavuta watu katika njia yao; na si hasha wala si ajabu kuwaona wakitumia mbinu hata ya kutoa misaada ya pesa kuwasaidia wanyonge na wahitaji na kufanya mambo mbalimbali ya utoaji huduma kwa umma, lakini ukweli ni kwamba lengo la kufanya hayo ni kuhifadhi idadi ya wale wenye imani kama yao na kuwavuta watu wengine kwenye imani yao potofu na ya batili. Bila shaka wao hawafaidiki na wanayoyafanya; na Mwenyezi Mungu hayapokei wala hawatakabalii mambo yao mema na ya kheri wanayofanya, kwa sababu hawayafanyi kwa lengo takatifu. Ni sawa kabisa na mtu ajengaye hospitali ili iwahudumie watu wasio na uwezo, lakini akawa amefanya hilo kwa ajili ya kujipatia umaarufu tu na hadhi ya kijamii. Hata kama watu wanyonge na wahitaji watanufaika na jema hilo, lakini mjengaji wake hafaidiki na alichokifanya. Mkabala wake ni watu walioitambua haki wakaiamini; na wakamwamini pia mletaji wake, yaani Bwana Mtume Muhammad SAW. Mema ya watu hao yatakubaliwa na Allah SWT. Anawaghufiria madhambi yao kwa rehma zake na kuwatengezea mambo yao. Kisha aya zinaendelea kueleza kwa msisitizo nukta ya kwamba, tofauti ya kuamini na kukufuru inatokana na tofauti ya baina ya haki na batili. Kundi moja linajitahidi kuijua haki na kuifuata, lakini kundi jengine, ambalo nalo pia limeitambua haki linakataa kuifuata, bali si hasha likasimama kukabiliana nayo. Watu duniani hawatoki kwenye moja ya makundi haya mawili. Ama wanaoikubali haki au wanaoipiga vita. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, maadui wa Uislamu wana mpango maalumu wa kukabiliana na dini hiyo ya haki, na wanafanya kila njia kufanikisha mpango wao huo. Hata hivyo yote wayafanyayo hayatafika popote; kwani Uislamu utaendelea kuenea siku baada ya siku. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kumwamini Allah peke yake hakutoshi; inalazimu kumwamini pia Mtume wake wa mwisho ili tuweze kuifuata ipasavyo njia yake Mola kupitia mafunzo na mafundisho ya Nabii wake huyo wa rehma. Halikadhalika aya hizi zinatutaka tujue kwamba, kama tutajitahidi kufanya mambo mema na ya kheri kwa kadiri ya uwezo wetu, Mwenyezi Mungu Mtukufu atatusamehe madhambi na makosa yetu na tutatengenekewa katika mambo yetu. Vilevile aya hizi zinatuelimisha kuwa, kumwamini tu Mwenyezi Mungu, Mtume wake na Kitabu chake cha Qur'ani hakutoshi; inalazimu pia kufanya amali njema na za kheri.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya nne hadi ya sita ya sura yetu ya Muhammad ambazo zinasema:
فَإِذَا لَقِيتُمُ الَّذِينَ كَفَرُوا فَضَرْبَ الرِّقَابِ حَتَّىٰ إِذَا أَثْخَنتُمُوهُمْ فَشُدُّوا الْوَثَاقَ فَإِمَّا مَنًّا بَعْدُ وَإِمَّا فِدَاءً حَتَّىٰ تَضَعَ الْحَرْبُ أَوْزَارَهَا ۚ ذَٰلِكَ وَلَوْ يَشَاءُ اللَّهُ لَانتَصَرَ مِنْهُمْ وَلَٰكِن لِّيَبْلُوَ بَعْضَكُم بِبَعْضٍ ۗ وَالَّذِينَ قُتِلُوا فِي سَبِيلِ اللَّهِ فَلَن يُضِلَّ أَعْمَالَهُمْ
Basi mnapokutana (vitani) na walio kufuru wapigeni shingoni mwao, mpaka mkiwadhoofisha wafungeni pingu. Tena waachilieni kwa hisani au wajikomboe, mpaka vita vipoe. Ndivyo hivyo! Na lau angeli taka Mwenyezi Mungu angeli washinda mwenyewe, lakini haya ni kwa sababu akutieni mitihani nyinyi kwa nyinyi. Na walio uliwa katika njia ya Mwenyezi Mungu hatazipuuza a'mali zao.
سَيَهْدِيهِمْ وَيُصْلِحُ بَالَهُمْ
Atawaongoza na awatengezee hali yao.
وَيُدْخِلُهُمُ الْجَنَّةَ عَرَّفَهَا لَهُمْ
Na atawaingiza katika Pepo aliyo wajulisha.
Kama tulivyoeleza katika aya zilizopita, maadui wa Uislamu wanatumia njia na mbinu tofauti ili kukabiliana na Uislamu na kuwadhoofisha Waislamu; na moja ya mbinu zao hizo ni kuanzisha vita na mapigano. Katika aya hizi tulizosoma, Allah SWT anaeleza bayana na kwa msisitizo kamili kwamba: katika medani ya Jihadi na vita na maadui, kuweni imara na thabiti, piganeni kwa ushujaa na msambaratisheni adui. Lakini yeyote kati yao atakayejisalimisha kwenu, msimuue, bali mkamateni mateka; na baada ya kumalizika vita mwachieni huru kwa ihsani au kwa kupokea malipo ya fidia. Kupambana kwenu na adui inapasa kuwe kwa namna itakayomfanya ashindwe, na kumpigisha magoti asalimu amri; na hii inapasa iwe ndiyo mbinu ya kivita ya kuitumia hadi kuhakikisha mumemdhibiti adui. Ni wazi pia kuwa, katika vita na mapigano hayo, baadhi ya watu huuawa. Ikiwa waliouawa watakuwa katika njia ya haki, Allah SWT atazinunua nafsi zao na kuwapa jaza yao Akhera; na ikiwa waliouawa watakuwa katika njia ya batili, hao watakuwa wamepoteza bure roho zao, na adhabu kali inawangojea pia Siku ya Kiyama. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, inatupasa tuamiliane kwa amani na masikilizano; na makafiri ambao hawajaanzisha vita kupigana na Waislamu. Lakini tuchukue hatua kali kabisa na madhubuti kukabiliana na waliotangaza vita dhidi yetu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kama inavyosisitizwa kupambana kwa ujasiri na ushujaa na adui kwenye medani ya vita na mapigano, ndivyo linavyotiliwa mkazo pia suala la kutoa msamaha kwa mateka wa vita. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, vita na Jihadi ni moja ya nyuga na medani za kutahiniwa waumini na Allah SWT, ili ibainike ni nani aliye tayari kupigana Jihadi; na nani anayekimbia medani ya vita na mapambano. Vilevile aya hizi zinatuelimisha kwamba, japokuwa kidhahiri mashahidi wameuawa na wameondoka duniani, lakini kwa kuwa wamefanya muamala na Mwenyezi Mungu, juhudi zao hazipotei bure; na Yeye Mola atawapa jaza na malipo ya malengo yao mema na ya kheri. Kwa maana hiyo, mashahidi ndio washindi halisi katika medani ya vita na jihadi. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 928 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azifanye thabiti imani zetu, atughufirie madhambi yetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../