May 27, 2023 05:36 UTC
  • Sura ya Fat-h, aya ya 17-21 (Darsa ya 941)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 941 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 48 ya Al Fat-h. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 17 ya sura hiyo ambayo inasema:

لَّيْسَ عَلَى الْأَعْمَىٰ حَرَجٌ وَلَا عَلَى الْأَعْرَجِ حَرَجٌ وَلَا عَلَى الْمَرِيضِ حَرَجٌ ۗ وَمَن يُطِعِ اللَّهَ وَرَسُولَهُ يُدْخِلْهُ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ ۖ وَمَن يَتَوَلَّ يُعَذِّبْهُ عَذَابًا أَلِيمً

Kipofu hana lawama, wala kiguru hana lawama, wala mgonjwa hana lawama. Na mwenye kumt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, atamuingiza katika Mabustani ambayo hupita mito chini yake. Na atakaye geuka upande atamuadhibu adhabu iumizayo.

Katika darsa iliyopita tuliona jinsi Allah SWT alivyowakemea waliokhalifu kwenda vitani na kuwaweka kwenye kundi la watakaofikwa na adhabu. Ni wazi kwamba miongoni mwao, walikuwemo watu walemavu na wagonjwa ambao hawakuwa na uwezo wa kuandamana na Waislamu wenzao kwenda vitani. Baadhi ya watu hao walikwenda kwa Bwana Mtume SAW na kutaka kujua nini itakuwa hukumu yao. Ndipo aya hii iliposhuka na kupambanua hukumu yao na wale walio wazima, lakini wakakhalifu na kuasi amri ya Mtume wa Mwenyezi Mungu. Mojawapo ya usuli na misingi mikuu ya Uislamu, ambao unatawala katika maamrisho na hukumu zote za dini ni ule uliobainishwa kama ifuatavyo katika sehemu ya mwanzo ya aya ya 286 ya Suratul-Baqarah, ya kwamba: "Mwenyezi Mungu haikalifishi nafsi yoyote ila kwa kadiri ya iwezavyo"… Kwa mfano katika Sala, ambayo moja ya masharti yake ni kusimama, watu wagonjwa na wasio na uwezo kimwili, inawajuzia kusali kwa kukaa au hata kulala. Faradhi ya funga imeondolewa wajibu wake, si kwa wagonjwa peke yao, lakini hata kwa watu wazima, ikiwa itawabainikia kwa yakini kwamba kufunga kutawasababishia maradhi, basi na wao pia wataondokewa na wajibu wa kufunga. Ili ibada ya Hija iwe ni wajibu kwa mtu, ni sharti awe na uwezo wa kimwili mbali na wa fedha; kwa hivyo watu wasio na uwezo wa kwenda Makka au kutekeleza hukumu za Hija, wao wanasameheka kutekeleza faradhi hiyo. Katika aya hii tuliyosoma pia, Qur'ani tukufu inasema: Jihadi ya kupambana na maadui ni wajibu kwa watu walio wazima kiafya, ambao wanao uwezo wa kupigana vita na kujihami nafsi zao; ama wale walio na ulemavu wa kimwili au walio wagonjwa, wao wanasameheka kwenda kwenye medani za vita na Jihadi. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, Mwenyezi Mungu anawapa mazingatio maalumu watu wagonjwa na walemavu kwa kuwaondolea wajibu wa kutekeleza baadhi ya faradhi za dini. Kwa hivyo viongozi na watungaji sheria katika jamii ya Waislamu, nao pia inawapasa waizingatie nukta hii wakati wanapopanga na kuweka sheria na kanuni za kijamii. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, suala muhimu na la msingi kwa Muislamu ni kutii na kujisalimisha kwa maamrisho ya Allah SWT ; japokuwa wajibu wa watu unatofautiana kulingana na mazingira na uwezo wa kila mmoja wao.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 18 na 19 ambazo zinasema:

لَّقَدْ رَضِيَ اللَّهُ عَنِ الْمُؤْمِنِينَ إِذْ يُبَايِعُونَكَ تَحْتَ الشَّجَرَةِ فَعَلِمَ مَا فِي قُلُوبِهِمْ فَأَنزَلَ السَّكِينَةَ عَلَيْهِمْ وَأَثَابَهُمْ فَتْحًا قَرِيبًا

Kwa hakika Mwenyezi Mungu amewaridhia Waumini walipokubai chini ya mti, na alijua yaliyomo nyoyoni mwao. Basi akateremsha utulivu juu yao, na akawalipa kwa Ushindi wa karibu.

وَمَغَانِمَ كَثِيرَةً يَأْخُذُونَهَا ۗ وَكَانَ اللَّهُ عَزِيزًا حَكِيمًا

Na ngawira nyingi watakazo zichukua. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima.

Katika darsa kadhaa nyuma tulieleza kwamba Bwana Mtume Muhammad SAW na masahaba zake waliondoka Madina na kuelekea Makka kwa madhumuni ya kwenda kufanya Umra; na kwamba Mtume wa Allah alimtuma mmoja wa masahaba zake kwa wakubwa wa Makureishi akawajulishe kwamba Waislamu hawaendi huko kwa nia ya kupigana vita, bali lengo lao ni kuzuru Nyumba ya Mwenyezi Mungu; lakini Makureishi walimkamata na kumweka kizuizini mjumbe huyo wa Bwana Mtume. Kufuatia hatu hiyo ya Makureishi, Mtume wa Mwenyezi Mungu aliwakusanya masahaba zake chini ya mti uliokuwepo katika eneo liitwalo Hudaibiya; na hapo akachukua baia' ya utiifu kwao, kwamba hakuna yeyote kati yao atakayerudi nyuma katika medani ya vita wala kuzembea katika kupambana na washirikina. Wakati habari ya baia' hiyo ilipowafikia washirikina waliingiwa na hofu wakaamua kumwachia huru mjumbe wa Mtume. Kwa kufungwa mkataba wa Hudaibiya, njia ikafunguliwa kwa Waislamu kwenda kufanya Umra katika miaka iliyofuatia. Na baada ya hapo pia, Waislamu wakashinda na kuikomboa ngome ya Khaybar na kujipatia ngawira chungu nzima. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kuwa muumini hakuishii katika ufanyaji baadhi ya amali za kiroho tu za Uislamu kama Sala na Funga, lakini kujitokeza na kushiriki katika nyuga za kijamii na kisiasa, kuwa bega kwa bega na kuwasaidia viongozi wa dini, ni miongoni mwa vielelezo pia vya kuwa muumini wa kweli. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, tusihadaiwe na dhahiri ya amali zetu. Allah SWT ana ujuzi kamili wa nia halisi na yaliyomo ndani ya nafsi zetu na atatulipa thawabu kulingana na nia hizo. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, kupata radhi na ridhaa ya Mwenyezi Mungu Azza wa Jalla, ambalo ni jambo la kimaanawi, hakuna mgongano na kuchuma ngawira za vitani na neema za hapa duniani. Halikadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, kuwa na utiifu na uaminifu kwa Mtume wa Allah na kumsaidia katika kukabiliana na maadui ndiyo siri ya kupata rehma na fadhila za Mwenyezi Mungu duniani na akhera.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 20 na 21 za sura yetu ya al Fat-h ambazo zinasema:

وَعَدَكُمُ اللَّهُ مَغَانِمَ كَثِيرَةً تَأْخُذُونَهَا فَعَجَّلَ لَكُمْ هَٰذِهِ وَكَفَّ أَيْدِيَ النَّاسِ عَنكُمْ وَلِتَكُونَ آيَةً لِّلْمُؤْمِنِينَ وَيَهْدِيَكُمْ صِرَاطًا مُّسْتَقِيمًا

 Mwenyezi Mungu anakuahidini ngawira nyingi mtakazo zichukua, basi amekutangulizieni hizi kwanza, na akaizuia mikono ya watu isikufikieni, na ili hayo yawe Ishara kwa Waumini, na akakuongozeni Njia Iliyo Nyooka.

وَأُخْرَىٰ لَمْ تَقْدِرُوا عَلَيْهَا قَدْ أَحَاطَ اللَّهُ بِهَا ۚ وَكَانَ اللَّهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرً

Na mengine hamjaweza kuyapata bado, Mwenyezi Mungu amekwisha yazingira. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.

Aya hizi zinaendeleza maudhui iliyozungumziwa katika aya zilizotangulia kwa kueleza kwamba, rehma na fadhila za Allah kwa waumini haziishii kwenye Sulhu ya Hudaibiya na ukombozi wa ngome ya Khaybar pekee, bali kuna ushindi mwingine kadhaa ambao watapata Waislamu katika siku za usoni, ushindi ambao wao wenyewe hawaufikirii wala kuuwaza na wala hakuna uwezekano kwa wao na uwezo wa kuupata. Na sababu ni kuwa, mbali na Mwenyezi Mungu Mtukufu kuteremsha sakina na utulivu ndani ya nyoyo za waumini, anazitia woga na hofu pia nyoyo za makafiri ili waache kuanzisha uchokozi na uvamizi dhidi ya Waislamu. Ni wazi kwamba, misaada hiyo ya ghaibu ya Allah inaimarisha imani za waumini juu ya ukweli wa Mtume wa Mwenyezi Mungu na kuwafanya wawe thabiti katika njia ya uongofu wanayoifuata. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, katika kanuni za vita inajuzu kuchukua mali za adui kwa sura ya ngawira; na kanuni hii imethibitishwa na kukubaliwa na Allah SWT. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, Mwenyezi Mungu Mtukufu ametupa ahadi kwamba kama tutafanya juhudi za kweli na za ikhlasi za kuinusuru dini yake, atatuteremshia baraka za kimaada pia za neema za hapa duniani. Vilevile aya hizi zinatutaka tujue kwamba, kuvunjwa nguvu maadui na kuzimwa uchokozi wao, na kupatikana amani na usalama katika jamii ya Waislamu ni miongoni mwa neema na ihsani kubwa ambayo Allah SWT anawafanyia waumini. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 941 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah aunusuru Uislamu na Waislamu na shari za maadui zao na awape nguvu na uwezo wa kuzishinda hila na njama zao. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/