May 27, 2023 06:23 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 945 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 49 ya H'ujuraat. Tunaianza darsa yetu kwa aya yake ya sita ambayo inasema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِن جَاءَكُمْ فَاسِقٌ بِنَبَإٍ فَتَبَيَّنُوا أَن تُصِيبُوا قَوْمًا بِجَهَالَةٍ فَتُصْبِحُوا عَلَىٰ مَا فَعَلْتُمْ نَادِمِينَ

Enyi mlio amini! Akikujieni fasiki na khabari yoyote, ichunguzeni, msije mkawadhuru watu kwa kuto jua, na mkawa wenye kujuta kwa mliyo yatenda.

Habari zozote tunazozisikia kwa watu wengine huwa za namna mbili: Baadhi yao ni habari ambazo huwa hazina uhusiano wowote na kazi zetu au maisha yetu, bali huwa zinaakisi matukio yanayojiri katika jamii na mazingira yaliyotuzunguka. Lakini baadhi ya habari huwa zinahusiana na kazi zetu na maisha yetu. Kutokana na namna tunavyozipokea habari hizo ndivyo tunavyochukua uamuzi wa nini tufanye au tuonyeshe hisia na mtazamo gani juu yake! Aya hii tuliyosoma, inahusu aina ya pili ya habari na kueleza kwamba: katika habari kama hii, kabla ya kuchukua uamuzi au hatua yoyote ile, inapasa muhakiki na kuchunguza kama msimulizi wa habari hiyo ni mtu mkweli au muongo? Na habari anayosimulia inahusu matashi na makusudio ya mtu binafsi au inahusiana na tukio linalojiri kwenye mazingira tu ya nje? Kwa sababu kama hatutakuwa makini na kuitafakari habari tuliyosikia, tutaichukulia uamuzi usio sahihi, ambao athari na matokeo yake hayataweza kufidika. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, sharti la imani juu ya Mwenyezi Mungu ni kuwa makini na kutafakari katika mambo tunayofanya na tunayoyachukulia maamuzi, ili tusije tukachukua hatua kwa papara au kwa kuamini jambo kirahisi tu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, habari tunazosikia kwa watu wengine hata mafasiki na wafanya maasi tusizikatae wala kuzikubali moja kwa moja, bali tuchunguze na kuhakiki, kwa sababu wakati mwingine, hata mafasiki pia huwa wanasema kweli. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba, baadhi ya watu na vyombo vinavyopiga upatu wa habari hueneza uvumi na habari zisizo sahihi kwa watu ili kuitia jamii tafrani na mivutano. Kwa hiyo njia ya kuepukana na madhara hayo ya kijamii ni kwa waumini kuhakiki na kuchunguza yale wanayoyasikia. Halikadhalika aya hii inatutaka tujue kuwa, maamuzi na hatua zichukuliwazo bila nadhari huleta hasara na majuto. Na tab'an mara nyingi majuto hayo hayawi na faida yoyote kwa sababu hayawezi kufidiwa.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya saba na ya nane ambazo zinasema:

وَاعْلَمُوا أَنَّ فِيكُمْ رَسُولَ اللَّهِ ۚ لَوْ يُطِيعُكُمْ فِي كَثِيرٍ مِّنَ الْأَمْرِ لَعَنِتُّمْ وَلَٰكِنَّ اللَّهَ حَبَّبَ إِلَيْكُمُ الْإِيمَانَ وَزَيَّنَهُ فِي قُلُوبِكُمْ وَكَرَّهَ إِلَيْكُمُ الْكُفْرَ وَالْفُسُوقَ وَالْعِصْيَانَ ۚ أُولَٰئِكَ هُمُ الرَّاشِدُونَ

Na jueni kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu yuko pamoja nanyi. Lau angeli kut'iini katika mambo mengi, bila ya shaka mngeli taabika. Lakini Mwenyezi Mungu ameipendezesha kwenu Imani, na akaipamba katika nyoyo zenu, na akauchukiza kwenu ukafiri, na ufasiki, na uasi. Hao ndio walio ongoka,

فَضْلًا مِّنَ اللَّهِ وَنِعْمَةً ۚ وَاللَّهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ

Kwa fadhila za Mwenyezi Mungu na neema zake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye hikima. 

Aya hizi zinaashiria neema mbili kubwa za Allah SWT; ya kwanza ni kutuma Mitume wa kuwaongoza na kuwaelekeza watu kwenye uongofu; na ya pili ni fit'ra na maumbile safi ambayo Yeye Mola amewajaalia kuwa nayo wanadamu wote. Mitume wanawafikishia watu maneno ya mantiki na yenye ukweli wa wazi kabisa ili kuwaongoza na kuwaelekeza kwenye njia sahihi; na kwa upande wa hulka na tabia pia, wao ni ruwaza na vigezo vilivyokamilika vya kuigwa na kufuatwa na watu. Na ndio maana watu walio waumini wa kweli huwatii na kuwafuata Mitume. Kwa upande mwingine, Mwenyezi Mungu Azza wa Jalla, ameyaumba maumbile ya mwanadamu kwa kuyafanya yawe yanapenda mambo mema na kuchukia mambo mabaya. Kwa mfano, hata mwizi anayewaibia watu mali zao, kwa dhati ya nafsi yake anajua fika kwamba wizi ni kazi ovu na isiyopendeza. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kama tunataka tusije kupatwa na hasara na majuto, basi tufuate mafundisho ya Manabii wa Allah, na si kutarajia kwamba, wao Mitume wafuate matakwa yetu sisi; kwani matarajio hayo hayana mantiki wala maana yoyote. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kuvutiwa na dini, ambayo inamlingania mtu mema na kumweka mbali na mabaya, ni jambo la fit'ra na la kimaumbile, na ni hali ambayo Allah amemjaalia kila mtu kuwa nayo. Vilevile aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba, ukuaji na upevukaji wa kweli wa jamii unafungamana na kufuata mafunzo na mafundisho yaliyotukuka ya Mitume wa Mwenyezi Mungu na kujitakasa na uchafu wa kitabia na kimaadili. Aidha aya hizi zinatuelimisha kuwa pambo halisi la mwanadamu ni imani na ukamilifu wake wa kimaanawi na kiakhlaqi; si vivutio vya kidhahiri kama libasi na mavazi, majumba na makasri na vipando vya kifakhari.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya tisa ya sura yetu ya H'ujuraat ambayo inasema:

وَإِن طَائِفَتَانِ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ اقْتَتَلُوا فَأَصْلِحُوا بَيْنَهُمَا ۖ فَإِن بَغَتْ إِحْدَاهُمَا عَلَى الْأُخْرَىٰ فَقَاتِلُوا الَّتِي تَبْغِي حَتَّىٰ تَفِيءَ إِلَىٰ أَمْرِ اللَّهِ ۚ فَإِن فَاءَتْ فَأَصْلِحُوا بَيْنَهُمَا بِالْعَدْلِ وَأَقْسِطُوا ۖ إِنَّ اللَّهَ يُحِبُّ الْمُقْسِطِينَ

Na ikiwa makundi mawili katika Waumini yanapigana, basi yapatanisheni. Na likiwa moja la hayo linalidhulumu jingine, basi lipigeni linalo dhulumu mpaka lirejee kwenye amri ya Mwenyezi Mungu. Na likirejea basi yapatanisheni kwa uadilifu. Na hukumuni kwa haki. Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wanao hukumu kwa haki. 

Aya hii inagusia mfano mwingine wa madhara ya kijamii na kueleza kwamba: kuna wakati hutokea ugomvi na mapigano baina ya watu au makundi ya jamii na kila upande ukaomba msaada kwa marafiki na watu wao wa karibu ili uwawezeshe kupata ushindi katika ugomvi au mapigano hayo. Qur'ani inasisitiza katika suala hili kwamba, badala ya watu wengine katika jamii, nao pia kujiingiza kwenye mapigano, wawanasihi na kuwaasa wanaopigana wafikie suluhu na mapatano ili na wao wasije wakawa sababu ya kupamba moto na kupanuka ugomvi na mapigano hayo. Lakini kama moja kati ya pande hizo mbili itashikilia na kung'ang'ania kuendeleza vita na mapigano na kukataa katakata kufanya suluhu, Waislamu wote watakuwa na wajibu wa kukabiliana nalo na kulidhibiti kundi hilo linaloendeleza shari ili jamii isije ikatumbukia kwenye lindi la fitna na madhara makubwa zaidi. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba wanajamii wote wana jukumu na masuulia kuhusiana na usalama wa jamii yao. Kwa hivyo inapotokea mizozo na mapigano, haikubaliki watu kubaki kuwa watazamaji tu. Inapasa wawasuluhishe na kuwapatanisha wanajamii wenzao; lakini kama kundi moja kati ya mawili yanayopigana litaendeleza vita na uasi itapasa walidhibiti na kulichukulia hatua ili amani na usalama uendelee kuwepo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, haijuzu kumwachia na kumtazama tu mtu mwasi na mkorofi anayevuruga amani na usalama wa jamii. Mtu kama huyo, hata akiwa Muislamu, damu yake huwa haiheshimiki. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba, inapasa uadilifu uzingatiwe katika kuleta suluhu baina ya pande mbili zinazopigana vita, ili haki ya aliyedhulumiwa isije ikapotea. Itokeapo hivyo, suluhu na mapatano ya aina hiyo huwa ni ya madhila na udhalilishaji tu. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 945 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah, awajaalie Waislamu waishi kwa masikilizano baina yao, aziletee utulivu, usalama na amani ardhi zao na awaondolee fitna na mabalaa ya mizozo, vita na mapigano baina yao na mabalaa yanayotokana na uvamizi na shari za maadui zao. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/