Filamu "Barbie" na marufuku yake katika nchi za Kiislamu
https://parstoday.ir/sw/radio/uncategorised-i102442-filamu_barbie_na_marufuku_yake_katika_nchi_za_kiislamu
Barbie ndie mwanasesere anayeuzwa sana ambaye alianza kutengenezwa nchini Marekani zaidi ya miaka 60 iliyopita, na umaarufu wake miongoni mwa wasichana wadogo ulimwenguni kote umekuwa sababu ya kutengenezwa filamu nyingi zinazohusiana na mwanasesere huyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 20, 2023 02:18 UTC
  • Filamu

Barbie ndie mwanasesere anayeuzwa sana ambaye alianza kutengenezwa nchini Marekani zaidi ya miaka 60 iliyopita, na umaarufu wake miongoni mwa wasichana wadogo ulimwenguni kote umekuwa sababu ya kutengenezwa filamu nyingi zinazohusiana na mwanasesere huyo.

Katika miaka hii yote, wanasaikolojia wamekuwa wakikosoa shakshia ya mwanasesere huyo kutokana na madhara na uharibifu wa mdoli huyo kwenye maisha ya watoto, bali hata kwa watu wazima.

Tovuti za habari zimeripoti kuwa, filamu ya "Barbie" imepigwa marufuku nchini Algeria kutokana na kuenenza "propaganda za ushoga na uhalifu mwingine unaokiuka maadili ya kidini na kitamaduni ya nchi hiyo". Shirika la habari la Reuters limenukulu duru rasmi za Algeria zikisema kwamba, filamu hiyo "inatangaza liwati, ushoga na upotovu mwingine wa Magharibi," ambao "hauambatani na imani za kidini na kitamaduni za Algeria." Kupigwa marufuku filamu hiyo huko Algeria kunafuatia hatua sawa zilizochukuliwa katika nchi kadhaa za Asia Magharibi zikiwemo Kuwait na Lebanon, ambazo zimepiga marufuku filamu hiyo. Barbie imeonyeshwa Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu na Bahrain, baada ya kuchujwa na kuondolewa baadhi ya sehemu zake.

Saudi Arabia, ambayo hapo awali ilitangaza kuwa filamu hiyo ya Barbie haitaonyeshwa katika majumba ya sinema ya nchi hiyo, hatimaye ilitoa idhini ya kuonyeshwa nchini humo, suala mbalo limeibua hisia tofauti baina ya watazamaji wa Kisaudi. Kwa mfano, mwandishi wa habari wa Saudia, Turki Al-Shalhoub, amesema: "Filamu ya Barbie ina vipengee vinavyomtambua mwanamke kuwa ni sawa na bidhaa ya kuuzwa na kununuliwa, kueneza na kupigia debe ushoga, kuwadhihirisha mashoga na watu wanaofanya liwati kuwa ni mashujaa na kuhubiri ufeministi uliopindukia."

Nchini Lebanon, Waziri wa Utamaduni wa nchi hiyo ametangaza kwamba filamu ya "Barbie" inatangaza ushoga, kufifiza umuhimu wa familia na inakinzana na thamani za kidini na kimaadili. Mohammed Wissam Al-Murtadha amesisitiza kuwa, filamu hiyo inapingana na maadili ya kidini nchini Lebanon, kwa sababu inahimiza upotovu wa kubadilisha jinsia, na wakati huo huo inapinga mfumo dume na kukejeli nafasi ya mama. 

Msemaji wa Wizara ya Habari ya Kuwait pia alisema kuwa filamu hiyo inahuburi "mawazo na imani ambazo ni ngeni kwa jamii ya Kuwait." Kuonyeshwa kwa filamu Barbie katika jimbo la Punjab huko Pakistani pia kumeahirishwa kutokana na "maudhui yasiyofaa".

Ikumbukwe kwamba kuonyeshwa filamu "Barbie" hakukupigwa marufuku katika nchi za Kiislamu pekee, bali nchi kama Vietnam pia imepiga marufuku filamu hiyo kutokana na kuonyesha ramani ya uongo kuhusu madai ya China katika Bahari ya Kusini ya China. Ufilipino pia imeruhusu kuonyeshwa filamu hiyo baada ya kuchujwa na kufanyiwa marekebisho.   

Kama tulivyosema katika kipindi cha Makala ya Wiki iliyopita, filamu "Barbie" iliyoongozwa na Greta Gerwig ni komedi ya fantasia ambayo ilizinduliwa nchini Marekani mwezi Julai 2023. Filamu hiyo imevutia hisia za watumiaji wa mitandao ya kijamii kutokana na kutolewa kwa wakati mmoja na filamu "Oppenheimer". 

Filamu hiyo imetengenezwa kwa mujibu wa mtindo wa maisha wa wanasesere Barbie. Katika filamu hiyo hakuna falsafa yoyote isipokuwa ufeministi wa kibinafsi, na jambo hili liko wazi sana kiasi kwamba, mwandishi wa "Daily Mail", ambaye yeye mwenyewe ni mwanamke, anaandika kuhusu uwakilishi wa wanaume kwenye filamu hiyo kwamba: "Hii ni filamu iliyo dhidi kabisa mwanaume. Kila mhusika wa kiume katika filamu Barbie ama ni mpumbavu, au mtu mwenye fikra mgando, au mtu aliyefeli, mwenye huzuni na wa kusikitisha kwa kiasi fulani." Mwandishi huyo wa Daily Mail anaendelea kusema: Filamu "Barbie" inakera sana na ni ya kijinsia, na inahalalisha kuwanyonya wanawake kwa kutumia jina la kutetea haki zao.    

Shakhsia ya Barbie katika sinema ilizaliwa katika enzi ambayo sinema ililenga zaidi watazamaji wa kiume na kwa sababu hiyo, wanawake nusu uchi walionekana mara nyingi kwenye filamu za kipindi hicho. Katika zama hizo, wanaume wengi walitazama filamu kwenye majumba ya sinema, na wanawake walitazama tamthilia wakiwa nyumbani. Katika hali hii, Barbie aliingia katika utamaduni wa watu kama kitu ambacho kinapaswa kupatwa na kumilikiwa na wanaume, na kitu bora ambacho wanawake wanapaswa kufanana nacho. Tunaweza kusema kuwa, Barbie alikuwa waraka mwanasesere ulioakisi utamaduni wa watu, na sio kitu kilichoanzisha mwenendo na mtindo mpya. Mwanasesere huyu alikuwa sehemu ya tamasha kubwa na la kudumu ambalo lilionyeshwa katika sinema sambamba na watu kama Marilyn Monroe, na katika tasnia ya katuni sambamba na Malikia wa Walt Disney (Disney Princesses).

Wanawake wenye miili myembamba na nywele za dhahabu, zilizopinda na zenye mawimbi, wenye umaridadi na uzuri wa mdoli, walizingatiwa kuwa mali bora ya mwanaume. Wanasesere hao wenye nywele za blondi, wa kupendeza na kuvutia na wanaoonekana wapumbavu, walieneza na kuhubiri kilichojulikana kama mtindo wa maisha wa Kimarekani; yaani mwanamke mrembo, anayekubali kila kitu, mtiifu na mwenye mavazi maridadi, asiyejihusisha na siasa wala masuala ya jamii, na kwa ujumla, asiye na itikadi, maoni na matendo.

Tangu wakati huo na kutokana na matangazo mengi yaliyokuwa yakihuburi na kupigia debe shakhsia hiyo ya Barbie, watu wengi walijitokeza kupinga fikra hizo na kutangaza kuwa, kuwepo kwa Barbie na kugeuzwa kwake kuwa mizani na kigezo cha uanamke ni tusi na kuwadhalilisha wanawake. Wakati huo wanasaikolojia walitahadharisha kuhusu matokeo hatari ya kupigia debe mwanasesere huyo kwa watoto, na wadau wa vyombo vya habari walimuona Barbie kama kitu kilicho dhidi ya utamaduni.

Lakini sasa tuko katika wakati na zama tofauti, na Barbie anataka kujitangaza kama muenezaji wa sera mpya katika zama na enzi mpya. Barbie amekuja kuwa nembo ya mambo kama ushoga na maingiliano ya watu wenye jinsia moja, chuki dhidi ya mwanaume na kuhubiri ufeministi. 

Filamu "Barbie" inaanza kwa picha zinazoonyesha wasichana wadogo wakicheza michezo ya kimama na wanasesere wanaofanana na watoto, kisha sauti ya msimulizi inasema: "Tangu mwanzo wa wakati, tangu alipodhihiri msichana mdogo wa kwanza, kumekuwa na wanasesere. Lakini madoli yalikuwa daima "madoli watoto", na wasichana ambao walicheza nao waliweza tu kuwa mama zao…" Wasichana wadogo wanaomuona Barbie, wanawagonga na kuwabamiza wanasesere wao kwenye milango na kuta za nyumba…. Hivi ndivyo filamu Barbie inavyoanza.

Filamu Barbie 2023 imekuja kuwasilisha fikra kwamba, kuwa mama ni aina fulani ya utaahira na ni kikwazo kwa maendeleo ya wanawake. Si hayo tu, bali msimulizi katika filamu hiyo anasikika akisema kwamba, kuwa mama yumkini kukaonekana kuwa ni jambo zuri, lakini suala hilo ni la muda tu.

Kadiri filamu hiyo inavyoendelea mbele, tunaona zaidi na zaidi ubaridi usio na mwisho wa Barbie kuhusu mpenzi wake aliyetambulishwa kama Ken. Hii haina maana kwamba, Barbie hampendi Ken tu, bali ni kwamba, kimsingi hapendi mwanaume yeyote. Filamu hiyo inasonga mbele kwa mtindo huo huo unaowata wanawake kujitenga na fikra ya kuwa mama, kuwa mke na kuwa na uhusiano wa aina yoyote ambao upande wake wa pili ni mwanaume. Kwa maneno mengine ni kwamba, watengenezaji wa filamu Barbie wanataka kuwafanya wanawake waamini kuwa, ni jambo la aibu kuwa na hamu ya kuwa mama au mke, na badala yake kuwaelekeza wanawake upande wa kuwa na mahusiano ya kimwili na kingono na wanawake wenzao.

Tunapaswa kusema hapa kuwa, suala hilo haliishii katika filamu Barbie, na leo hii inashuhudiwa kuwa, huko Hollywood, tunakabiliwa na matangazo mengi ya kupigia debe ushoga na liwati na juhudi kubwa za kubadilisha mitazamo ya jamii kuhusu ufuska huo, na hatimaye kulifanya jambo hilo kuwa kitu cha kawaida. Harakati hii imeanzishwa ili kudhalilisha na kudhoofisha taasisi ya familia, kwa sababu tunapochunguza historia tunaona kwamba, liwati na maingiliano ya kingono baina ya watu wenye jinsia moja yamekuwepo katika vipindi vingi na idadi ndogo sana ya watu imehusika katika upotovu huu. Hata hivyo tunapoangalia vizuri medani ya utamaduni ya ulimwengu wa Magharibi tunaona kuwa, propaganda za kueneza na kupigia debe ufuska huo zimeshika kasi zaidi na zaidi.

Kwa mfano, Kampuni ya Walt Disney, mojawapo ya makampuni makubwa zaidi ya burudani duniani, imeweka wazi kuwa, imejitolea kuongeza kwa kiasi kikubwa wahusika wa ushoga, liwati na usagaji (LGBTQIA) katika bidhaa zake. Kwa miaka kadhaa sasa, Disney imekuwa ikionyesha shakhsia za waofanya liwati na wasagaji katika filamu zake za katuni, na mifano maarufu zaidi ya ukweli huo ni katuni za Frozen 2 na Toy Story 4.

Katika kipindi cha miongo miwili au mitatu iliyopita, vipindi vya televisheni vimesaidia sana njama za kuhalalisha mahusiano ya watu wenye jinsia moja, na mitandao ya kijamii pia imekuwa jukwaa la makundi ya watu wanaofanya liwati na wasagaji. Vilevile tasnia ya filamu imejiunga na mtindo huu hatua kwa hatua. Vyombo hivyo vya upashaji habari na burudani vinajaribu kuunda kazi nyingi za sanaa katika nyanja mbalimbali kwa kutumia mwavuli wa kutetea haki za wasagaji na watu wanaojihusisha na liwati au kwa anwani ya kuwaonea huruma.

Inatupasa hapa pia kuashiria kwamba, suala la kutotambua rasmi jinsia ya watu tangu wanapozaliwa ni mbinu mpya ambayo inatekelezwa kisheria katika baadhi ya nchi za Magharibi, na kwa sababu hiyo, kwa miaka mingi sasa Hollywood imekuwa ikifanya kazi ya kuzalisha filamu na katuni za kuhalalisha mtazamo huo. Mbali na sinema na filamu, mfumo wa elimu katika nchi za Magharibi pia unafanya kazi kubwa ya kueneza fikra hiyo na kutotambua rasmi jinsia ya mtoto tangu anapozaliwa. Pamoja na hayo inatupasa kukiri kwamba, sinema imekuwa mstari wa mbele katika mchakato huu, na utengenezaji wa filamu kama "Barbie" umefanyika katika mkondo huo huo wa kuhalalisha ufuska na utovu huo wa maadili, kudhoofisha na hatimaye kuharibu kabisa taasisi ya familia.