Kumbukumbu ya kuuawa shahidi Imam Hassan Askary (as)
Assalaamu alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio kipindi hiki maalumu kinachokujieni kkwa mnasaba wa kukumbukak siku aliyouawa shahidi Imam Hassan Askary (as) mmoja wa Maimamu watoharifu kutoka katika kizazi cha Bwana Mtume (saw).
Katika dakika hizi chache tutajaribu kutupia jicho sehemu ya sira na maisha ya mtukufu huyu. Huku tukitoa mkkono wa pole kwa mnasaba huu mchungu tunakukaribisheni kusikiliza machache tuliyokuandalieni katika kipindi hiki maalaumu.
Karibuni.
Ghamu, majonzi na huzuni ilitanda katika milango, kuta na mitaa ya mji wa Samarra Iraq. Upepo ulikuwa ukivuma na kuzunguka katika matawi na majani ya mitende kana kwamba, kulikuwa kukitoka sauti ya huzuni na ya maombolezo. Mji ulikuwa umetilia kama vile hakkukuwa na watu. Anga nzima ya mji huo ilikkuwa ikiashiiria kwamba, mji wa Samarra umekumbwa na jambo lisilo la kawaida. Kimsingi ni kuwa, kwa miaka mingi mji wa Samarra ulikuwa umekumbwa na huzuni. Imam Hassan Askary alikuwa ameletwa katika mji huo kwa lengo la kudhibiti nyendo zake na ndio maana hakukuwa na mtu ambaye alikuwa akienda katika nyumba ya mtukufu huyu na asiwe ni mwenye kufuatiliwa na makachero wa utawala.
Imam Hassan Askari (as) aliuawa shahidi katika siku kama hizi kufuatia njama iliyofanywa na mmoja wa watawala dhalimu wa Bani Abbas.
Kati ya watawala wa Bani Abbas, Mu'tamid ndiye aliyewaudhi zaidi Imam Hassan Askary (as) na wafuasi wake, na kumfunga jela kwa muda fulani. Alikuwa mtawala mpenda madaraka na akitambua vyema kwamba, kama hangemdhibiti Imam Askary (as) kwa wakati na kumuacha aeneze mafundisho yake kwa uhuru kamilii miongoni mwa watu, basi muda si mrefu wangeweza kumuondoa madarakani kutokana na dhulma kubwa aliyokuwa akiwafanyia.
Katika upande wa pili, Mu'tamid na watawala wengine madhalimu wa Bani Abbas walikuwa wamesikia hadithi sahihi kutoka kwa Mtume (saw) kwamba Imam Askary (as) angeruzikiwa mtoto ambaye baadaye angeujaza ulimwengu kwa uadilifu na usawa na kuondoa kabisa utawala wa kidhalimu na uonevu.
Watawala hao walimbana na kumdhibiti Imam Askary (as) kwa kila njia waliyoweza na walitumia kila mbinu.
Kuhusiana na suala hilo, Imam (as) anasema: " Bani Ummayya na Bani Abbas walitulenga kwa mapanga yao kwa sababu kuu mbili. Ya kwanza ni kuwa walitambua vyema kwamba ukhalifa na uongozi wa Uislamu haikuwa haki yao na wala hawakuwa na hadhi yoyote kwenye haki hiyo. Walikumbwa na wasiwasi na hofu kubwa kuwa tusije tukaanzisha mapambano ya kusimamisha utawala adilifu na wa haki.
Sababu ya pili ni kwamba, walikuwa wamesikia hadithi za wazi na sahihi kwamba utawala wa madhalimu na waonevu ungeangushwa na Qaim wetu, na wao wakitambua vyema kwamba walikuwa ni watawala madhalimu na waonevu. Hivyo waliazimia kukata na kuuwa kizazi cha Mtume ili kutoruhusu kuzaliwa kwa Qaim wa Aali za Mtume (saw). Lakini Mwenyezi Mungu hakuruhusu wajue alikokuwa Mahdi (atfs) ili apate kudhihiri na kusimamisha utawala wake wa uadilifu hata kama makafiri watachukizwa na jambo hilo."
Licha ya uadui na njama zote hizo zilizofanywa na watawala wa Bani Abbas dhidi ya Ahlul Bait wa Mtume Mtukufu (saw), lakini njama na uadui huo haukumfanya Imam Hassan Askary (as) aache kuwatakia mema na kuwasaidia watawala hao katika utatuzi wa matatizo mengi yaliyoikumba serikali ya Kiislamu katika kipindi cha uhai wake. Imam (as) alikuwa kiongozi wa wanazuoni na wanamapambano wa kisiasa na kiitikadi katika zama zake. Katika zama hizo, wafuasi wa Imam Hassan Askary (as) walijishughulisha na uenezaji wa hadithi na mafundisho ya Ahlul Bait wa Mtume (saw) pamoja na sheria za Kiislamu.
Licha ya kukabiliwa na hali ngumu ya kisiasa katika zama zake, Lakini Imam Hassan Askary (as) alitumia uwezo wake wote kutetea sheria za Kiislamu na kupambana na bida' na uzushi katika Uislamu. Juhudi kubwa za kielimu, kubainisha mitazamo na fikra safi na sahihi za Uislamu, kuanizsha mawasiliano na Mashia walioishi katika sehemu za mbali zaidi duniani na kuwatayarisha kwa ajili ya kipindi cha ghaiba (kutoonekana katika upeo wa macho) ya Imam wa kumi na mbili, ni miongoni mwa majukumu muhimu aliyokuwa nayo Imam Hassan Askary (as).
Imam Hassan Askari (as) alikuwa mja bora na wa kupigiwa mfano kuhusiana na suala la ibada na ucha-Mungu. Abu Hisham Ja'ffari mmoja wa wafuasi wa Imam Hassan Askary (as) anasema: 'Wakati wa swala ulipofika, aliacha shughuli aliyokuwa akiifanya na hakutanguliza kazi yoyote mbele ya swala. Uwepo mtukufu wa Imam (as) lilikuwa dhihirisho la kuvutia la ibada na kunyenyekea mbele ya Mwenyezi Mungu.'
Imam Hassan (askari (as) alikuwa mwenye huruma kubwa zaidi miongoni mwa watu na aliteua mawakili katika maeneo mengi ya Kiislamu ili wapate kutatua matatizo yaliyokuwa yakiwakabili wakazi wa maeneo hayo na kuwatengea watu masikini na wasiojiweza kiwango maalumu cha msaada wa fedha. Aliwataka mawakili hao kutumia fedha hizo katika kutatua matatizo ya watu, masuala ya heri, kuondoa hitilafu miongoni mwa Waislamu na mambo mengine yenye manufaa kwa umma wa Kiislamu.
Wapenzi wasikilizaji katika nasaha zake, Imam (as) aliwaomba watu wawe na subira na kulinda heshima zao katika kukabiliana na matatizo na changamoto tofauti za maisha. Anasema katika moja ya nasaha zake hizo za busara kwa mmoja wa wafuasi wake: "Kadiri unavyoweza kujizuia, usimuombe mtu. Hii ni kwa sababu, kila siku ina riziki yake mpya, na fahamu kwamba kuombaomba humuondolea mtu heshima na thamani yake. Hivyo kuwa na subira hadi Mwenyezi Mungu atakapokufungulia mlango. Fursa na neema kila moja ina wakati wake, hivyo usilifanyie pupa tunda ambalo halijaiva bado, bali muda wake ukifika utanufaika.
Katika sehemu nyingine ya miongozo yake, Imam Hassan Askary anasema: Mambo mawili ni miongoni mwa sifa mbili kuu. Imani na itikadi ya Mwenyezi Mungu Mmoja na kuwanufaisha ndugu katika imani. Kwa mujibu wa hadithi hii ya Imam Askary, kuwahudumia watu kuna umuhimu mkubwa kiasi kwamba, kumetajwa baada ya suala la imani ya itikadi ya Mwenyezi Mungu Mmoja.
Kama unavyojua mpenzi msikilizaji katika Aya nyingi za Qur'ani Tukufu Mwenyezi Mungu SW ametaja "amali njema" baada ya imani na kumuamini Yeye. Kwa msingi huo katika hadithi hii Imam Askary (as) anakutaja kuwahudumia watu kuwa ni miongoni mwa vielelezo vya amali njema.
Moja ya mambo yenye umuhimu mkubwa katika akhlaki na maadili ya Kiislamu ni kuwajali watu, kuwa na moyo wa ushirikiano, kutenda wema na kuwahudumia watu kwa njia mbalimbali hususan waumini na watu watenda mema. Tunapotazama Aya za Qur'ani Tukufu na hadithi nyingi na vilevile sira na mwenendo wa Mitume wa Mwenyezi Mungu na mawalii wake tunaona kuwa, hakuna jambo linalomkurubisha zaidi mja kwa Mola Muumba baada ya kutenda amali za wajibu kama kutenda wema na kuwahudumia waja wake. Ni kwa sababu hiyohoyo ndiyo maana Manabii na mawalii wa Mwenyezi Mungu daima walikuwa wakitanguliza mbele kazi ya kuwahudumia watu na kukidhi haja zao.
Kabla ya kufa shahidi, Imamu Hassan Askary (as) aliwaita takribani shakhsia 40 wa Kishia kutoka miji mbalimbali na akawaonyesha mtoto wake ili baada yakke watu wawe na utambuzi kuhusiana na Imamu wa zama zao na hivyo wasikumbwe na utata na kuchanganyikiwa.
Kwa mara nyingine tena tunatoa mkono wa pole kwa Waislamu wote na hasa wafuasi wakweli wa Ahlul-Bayt (as) kwa mnasaba huu wa kukumbuka siku aliyokufa shahidi Imam Hassan Askary (as).
Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabakaatuh