Kumbukumbu ya kuzaliwa Bibi Zaynab al-Kubra (as)
(last modified Sat, 18 Nov 2023 18:33:53 GMT )
Nov 18, 2023 18:33 UTC
  • Kumbukumbu ya kuzaliwa Bibi Zaynab al-Kubra (as)

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika kipindi hiki maalumu kinachokujieni kwa mnasaba wa kukumbuka siku aliyozaliwa Bibi Zaynab al-Kubra (a.s) binti ya Imam Ali bin Abi Talib (a.s); mwanamke ambaye aliondokea kuwa mashuhuri kutokana na kujipamba kwa sifa njema, fadhila, elimu, subira na ushujaa mkubwa aliokuwa nayo.

Nchini Iran Siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa Bibi Zaynab (a.s) inajuulikana kama "Siku ya Wauguzi", ambapo tabaka hili katika jamii huenziwa na kuthaminiwa mchango wao mkubwa walionao. Sambamba na kutoa mkono wa kheri, baraka na fanaka kwa mnasaba huu ninakukaribisheni muwe name katika dakika hizi chache ambapo tutaangazia japo kwa mukhtasari sehemu ya sira na mwenendo wa bibi mwema huyu. Kuweni name hadi mwisho wa kipindi hiki.

Bibi Zaynab al-Kubra (a.s) alizaliwa tarehe 5 Mfunguo Nane Jamadul Awwal mwaka wa 5 au wa 6 Hijria katika mji mtakatifu wa Madina. Bibi Zaynab (a.s) anayejulikana kama Shujaa wa Karbala na mbeba bendera ya harakati baada ya kuuawa shahidi ndugu yake yaani Imam Hussein bin Ali (a.s), alizaliwa na kulelewa katika nyumba iliyokuwa imejaa huba, fadhila na utukufu yaani nyumba ya Bibi Fatima Zahra na Imam Ali bin Abi Twalib (a.s). Bibi Zaynab (as) alirithi matukufu yote kutoka kwa baba yake yaani Imam Ali (a.s) na mama yake Bibi Fatima (a.s). Akiwa chini ya usimamizi na uangalizi wa malezi ya moja kwa moja ya wazazi wake hao watukufu, aliweza kukwea na kufikia daraja za juu za utukufu, ubora na ukamilifu.

Haram ya Bibi Zaynab (as) mjini Damascus Syria

 

Bibi Zaynab (a.s) alijifunza upole na uvumilivu kutoka kwa kaka yake Imam Hassan (as) huku akijifunza ushujaa kutoka kwa nduguye mwingine yaani Imam Hussein (as). Ni kutokana na sifa hizo bora ndipo ikadhihiri nuru na utukufu wa Kiislamu katika haiba ya mwanamke huyo mwema. Bi Zaynab AS aliondokea kuwa na taqwa, subira, kufungamana na maadili mema na sifa nyingine njema ambazo alijifunza kutoka kwa mama yake mwema ambaye ni mbora wa wanawake yaani Fatima Zahra AS. Bibi Zaynab (as) aliipitisha sehemu ya utoto wake kando ya babu yake yaani Mtume SAW na kupitisha moja ya vipindi vilivyojaa kumbukumbu nzuri. Hata hivyo kipindi hicho hakikudumu, kwani Bwana Mtume SAW aliaga dunia na kurejea kwa Mola wake. Aidha haukupita muda mrefu, mama yake naye akarejea kwa Mola wake.

Wapenzi wasikilizaji, licha ya kuwa Bibi Fatima Zahra (as) hakupitisha muda mrefu sana akiwa pamoja na watoto wake; lakini katika kipindi hicho hicho kifupi alichokuwa nao, aliwafunza watoto wake hao somo la juu kabisa la kumuabudu Mwenyezi Mungu na kutetea haki.

Sayyida Zaynab (as) alikuwa na akili ya hali ya juu, kiasi kwamba, katika kipindi hicho hicho cha utoto na kuinukia kwake aliweza kuhifadhi kwa moyo hotuba aali na iliyojaa madhumuni makubwa ya mama yake katika msikiti wa Mtume SAW yaani Masjdun Nabi. Hiyo ilikuwa ishara ya wazi ya upana wa fikra na hali ya kupevuka kifikra ya binti huyo aliyekulia katika malezi ya watu bora. Kielimu, Bibi Zaynab (as) alikuwa amebobea mno kiasi kwamba, umashuhuri wa elimu yake uliwafanya wanaume na wanawake wa Bani Hashim wampe lakabu ya "Mwanamke Mwenye Hekima."

 

Katika tukio la Karbala, Bi Zaynab (as) alisimama kidete na kukabiliana barabara na dhulma za watawala madhalimu na majahili wa zama hizo ili kutimiza malengo matukufu ya kaka yake, Imam Hussein (as). Bibi huyu alikuwa amebobea kielimu ambapo wanawake na mabinti wa Madina walikuwa wakienda katika nyumba ya Bibi Zaynab kwa ajili ya kujifunza elimu na maarifa. Zaynab kwa upande wake alikuwa akiitumia fursa hiyo kuwabainisha masuala mbalimbali ya kidini, kijamii na kisiasa. Darsa hizo za elimu ziliendelea pia wakati Bi Zaynab alipokuwa mjini Kufa baada ya baba yake kuelekea katika mji huo. Katika zama hizo wanawake na mabinti waliokuwa na hamu, shauku na raghba ya elimu walimtumia ujumbe Imam Ali AS na kumueleza kwamba, tumesikia kwamba, binti yako Zaynab kama alivyokuwa mtukufu mama yake, ni chemchemi ya elimu na maarifa na ana elimu na ukamilifu; hivyo turuhusu tuje kwake na kunufaina na elimu yake.

Bi Zaynab kama walivyo watu wengine wa nyumba tukufu ya Bwana Mtume SAW hakuwa nyuma katika masuala ya kiibada, dua na kunong'ona na Mwenyezi Mungu. Alitambulika kuwa mchaji Mungu na mtu aliyezama katika ibada na uchaji Mungu. Alikuwa akiamka nyakati za usiku na kuacha usingizi na kisha kusimama akifanya ibada na kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu.

 

Mbali na Swala za usiku alikuwa akisoma mno kitabu cha Mwenyezi Mungu yaani Qur'ani Tukufu. Baada ya tukio la Karbala licha ya masaibu, machovu, mateso na taabu alizokabiliana nazo yeye pamoja na watu wengine wa familia ya kaka yake yaani Imam Hussein (as), katu hakusahau au kughafilika kusali Swala za usiku. Imam Sajjad (as) anasimulia akisema: Shangazi yangu Zaynab (as) alikuwa akisali Swala zake zote za wajibu na mustahabu tukiwa njiani kutoka Kufa tukipelekwa Sham; na baadhi ya wakati alikuwa akitekeleza taklifu hizo za kidini akiwa amekaa kutokana na njaa kali na kudhoofika mwili."

Sifa nyingine kubwa ya Bi Zaynab AS ni uvumilivu na subira isiyo ya kawaida aliyokuwa nayo. Aidha aliondokea kuwa mashuhuri kutokana na kuwasaidia wahitaji na wasiojiweza na inaelezwa kwamba, nyumba yake mjini Madina ilikuwa kimbilio la wasio na uwezo na waliokwama katika mambo yao. Mmoja wa watafiti anaandika kuhusiana na hali hiyo kwa kusema: "Muamala na radiamali ya Bibi Zaynab (as) dhidi ya maadui, ilikuwa ya kushangaza na kustaajabisha. Aliweza kuwahutubu kwa maneno makali mno viongozi jeuri, licha ya wao kuwa na madaraka na uwezo mkubwa.

Kwa sauti ya juu, aliweza kuitikisa kasri ya kidhalimu na ghasibu ya Bani Umayya, sanjari na kuifedhehesha majlisi ya Yazid kwa maovu yake kupitia hotuba aliyoitoa mbele yake na watu wake wa karibu." Aidha miongoni mwa sifa nyingine adimu za Bibi Zaynab (as) ni ushujaa wa hali ya juu aliokuwa nao. Mtukufu huyo alisimama kwa nguvu zake zote na kupambana na madhalimu na hata kufikia kupewa lakabu ya "Simba wa Bani Hashim."

Wapenzi wasikilizaji muda wa kuipindi hiki maalumu umefikia tamati. "Kwa mara nyingine tena tunatoa mkono wa kheri, baraka na fanaka kwa mnsaba wa kukumbuka siku aliyozaliwa Sayyida Zaynab AS binti wa Imam Ali bin Abi Talib AS, siku ambayo kama tulivyaoshiria mwanzoni mwa kipindi hiki maalumu huadhimishwa pia hapa nchini kama "Siku ya Wauguzi".

Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh