Ufufuo na Marejeo ya Wanadamu -18
https://parstoday.ir/sw/radio/uncategorised-i20026-ufufuo_na_marejeo_ya_wanadamu_18
Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Ni wakati mwingine umewadia wa kuwa nanyi katika kipindi hiki kinachozungumzia kwa ufupi hatima na marejeo ya wanadamu baada ya dunia hii. Katika kipindi kilichopita tulizungumzia ulimwengu wa Barzakhi na kusema kuwa ndio nyumba ya kwanza baada ya mwanadamu kufariki dunia. Leo tutazungumzia ulimwengu wa kaburi.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Nov 23, 2016 07:59 UTC
  • Ufufuo na Marejeo ya Wanadamu -18

Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Ni wakati mwingine umewadia wa kuwa nanyi katika kipindi hiki kinachozungumzia kwa ufupi hatima na marejeo ya wanadamu baada ya dunia hii. Katika kipindi kilichopita tulizungumzia ulimwengu wa Barzakhi na kusema kuwa ndio nyumba ya kwanza baada ya mwanadamu kufariki dunia. Leo tutazungumzia ulimwengu wa kaburi.

Wakati mwanadamu anapofariki dunia na roho yake ikatengana na mwili na kuelekea ulimwengu wa roho, mwili wake huu wa kimaada huwekwa kaburini. Hata hivyo na licha ya kutengana huko, hubakia uhusiano dhaifu na mdogo sana baina ya mwili na roho ya mwanadamu aliyefariki dunia kutokana na viwili hivyo kuishi pamoja kwa muda mrefu na muungano uliokuwepo katika maisha ya dunia. Kwa hakika kuishi pamoja na mazoea yanayopatikana kutokana na kuwa pamoja kwa muda mrefu baina ya roho na mwili huifanya roho ya mwanadamu kuwa na aina fulani ya mahusiano na mwili wake walau dhaifu na mdogo. Ni kutokana na uhusiano huo ndiyo maana Uislamu ukaweka sheria makhsusi zinazohusiana na jinsi ya kusindikiza maiti, kukafini, kuzika, sheria zinazohusiana na kaburi, istihbabu na suna ya kuzuru makaburi, kuwaombea dua, rehma na maghufira waliotangulia kwa Mwenyezi Mungu makaburini na kadhalika. 

Ni vyema kukumbusha hapa kuwa, uhusiano huo baina ya roho na mwili huu wa kimaada katika ulimwengu wa Barzakhi huwa mkubwa zaidi katika nyakati za awali na siku za mwanzoni za baada ya kufariki dunia kutokana na uhusiano na mazoea ya kuishi pamoja kwa muda mrefu. Uhusiano huo hupungua taratibu kadiri mja aliyefariki dunia anavyozoea maisha ya ulimwengu wa Barzakhi na hubakia uhusiano hafifu na mdogo sana baina ya viwili hivyo. 

Roho ya mwanadamu kamwe huwa haibaki peke yake bali huandamana na mwili unaonasibiana na kuoana na ulimwengu ambako roho hiyo hupelekwa na inapokuwa. Kwa msingi huo katika ulimwengu wa Barzakhi pia roho ya mwanadamu huwa pamoja na mwili unaonasibiana na ulimwengu huo. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, mwili huu wa kimaada huwa haunasibiani na kuoana na ulimwengu wa Barzakhi. 

Baadhi ya watu wanadhani kuwa, Mwenyezi Mungu SW huumba mwili wa kibarzakhi unaooana na ulimwengu wa Barzakhi anapokuwa mwanadamu baada ya kufariki dunia. Wanaamini kwamba, roho ya mwanadamu huungana na mwili huo wa kibarzakhi. La hasha, bali mwili wa kibarzakhi hautofautiani na hakika ya mwanadamu mwenyewe. 

Ukweli ni kuwa, amali zetu nzuri na mbaya ndizo zinazounda na kutengeneza miili yetu katika ulimwemgu wa Barzakhi na huko Akhera. Kwa maana kwamba, katika kipindi chote cha maisha yake hapa duniani, mwanadamu hujenga na kutengeneza mwili wake wa baadaye katika ulimwengu wa Barzakhi na huko Akhera. Matendo, mienendo, maneno na hata fikra na mitazamo yetu vyote huchangia katika kuunda na kutengeneza batini na hakika yetu, au kwa lugha nyingine, miili yetu katika ulimwengu wa Barzakhi na huko Akhera. Miili hiyo ya Kibarzakhi ipo hivi sasa lakini haionekani kwa viungo vya kimaada kutokana na pazia na hijabu ya maada inayozuia kuona na kuelewa ipasavyo masuala yasiyo ya kimaada. Naam, wapo baadhi ya watu ambao kutokana na ibada, uchamungu na kutakasa nafsi wanaweza kupasua pazia na hijabu hiyo na kushuhudia kwa jicho la roho zao safi batini na miili ya ulimwengu wa Barzakhi. Imepokewa kutoka kwa Imam Ja'far Swadiq (as) kwamba amesema: "Roho za waumini katika ulimwengu wa Barzakhi zitakuwa katika miili inayoshabihiana na miili yao hapa duniani". (Biharul Anwar 6:119) 

Hadithi zilizopokewa kutoka kwa Mtume Muhammad (saw) na Aali zake watoharifu zinaonesha kuwa, nafasi ya mwanadamu katika ulimwengu wa Barzakhi italingana na amali na matendo mema na maovu aliyotenda hapa duniani. Hadithi ya Mtume (saw) iliyopokewa kutoka kwa mjukuu wake, Imam Sajjad Zainul Abidin (as) inasema: "Kaburi huwa ama bustani kati ya mabustani ya peponi au moja kati ya mashimo ya moto wa Jahannam". (Tafsiri ya al Burhan 3:120)

Hivyo basi kaburi ambalo ndio ulimwengu wa Barzakhi, huwa sehemu ya kudhihiri matokeo ya amali na matendo ya mja kabla ya kuwadia Siku ya Kiyama. Imam Swadiq (as) aliulizwa kwamba: Barzakhi ni nini? Alisema: "Ni kaburi tangu mwanadamu anapofariki dunia hadi Siku ya Kiyama". (Usul Kafi-3) Kwa utaratibu huo kaburi lina maana mbili. Kwanza ni shimo hili linalochimbwa makaburini wanakozikwa wafu na kuwekwa miili ya kimaada ya wanadamu. Maana nyingine ya kaburi ni ulimwengu wa Barzakhi. Hivyo basi linapozungumziwa suala la mbinyo wa kaburi, maswali ya kaburini, wahka na fazaa ya kipindi hicho maana yake si kaburi hili la udongo bali ni ulimwengu wa Barzakhi. Kwa maana hiyo ya kaburi pia watu ambao hawana kaburi kama wale walioghiriki baharini na miili yao haikupatikana kabisa, waliochomwa moto na miili yao ikawa majivu na kadhalika wanakumbana na maswali ya kaburini, misukosuko na wahka wa kipindi hicho cha kaburi kwa maana ya ulimwengu wa Barzakhi. Aya ya 25 ya Suratu Nuh inahadithia hatima ya kaumu ya Nabii Nuh (as) waliogharikishwa baharini na kusema: "Basi kwa ajili ya makosa yao waligharikishwa, wakaingizwa Motoni.."

Ni wazi kuwa, moto unaozungumziwa hapo ni moto wa ulimwengu wa Barzakhi na si katika kaburi la udongo la dunia hii. 

Baadhi ya watu wanauliza kwamba, adhabu na neema za kaburini zilizotajwa katika Qur'ani na hadithi za Mtume na Aali zake watoharifu huwa vipi? Hii ni kwa sababu, mwili wa mwanadamu unapowekwa kaburini na kufukiwa na udongo, tunapolifukua kaburi hilo baada ya muda hatuoni lolote kati ya yanayosemwa kama moto au kuchomwa na moto na neema zinazotajwa katika mafundisho ya dini? Kitu pekee tunachokiona ni mwili ule ule tulioweka na kuulaza kaburini. Sasa adhabu na neema za kaburini huwa vipi?

Swali hili linaweza kujibiwa kwa kutoa mfano wa ndoto ya mwanadamu. Mtu anayeona ndoto ya kutisha, watu walioko kandokando yake huona mwili wake uliotulizana na katika hali ya usingizi tu. Hata hivyo kama mwenye kuona ndoto hiyo ya kutisha hatawaeleza hali aliyokumbana nayo katika ndoto na adhabu na wahka aliokuwa nao wakati alipokuwa amelalala, kamwe wasingeweza kujua yaliyomkuta. 

Tumesema kuwa, katika dakika na saa za awali za baada ya kufariki dunia na roho kutengana na mwili wa kimaada, roho hubakia kandokando ya mwili wake kutokana na uhusiano mkubwa uliojengeka baina ya viwili hivyo kwa miaka au muda mrefu. Roho hiyo huufuata mwili wake wakati watu na jamaa wa karibu wanapokuwa wanaugeuza, kuuosha na kuusafirisha. Roho hiyo ambayo huwa tayari imepata habari za ulimwengu wa Barzakhi, huwa inazungumza na wenzake katika ulimwengu huo bila ya watu wanaosindikiza mwili kujua lolote. Wakati mwili wa maiti unapokaribia kuwekwa kaburini, roho ambayo inakuwa ikishuhudia hali hiyo, hupatwa na wasiwasi na woga mkubwa. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana mafundisho ya Kiislamu yanawataka wanadamu wasipeleke moja kwa moja mwili wa maiti na kuuingiza kaburini, bali uwekwe juu ya ardhi kabla ya kuingizwa kaburini ili mwanadamu ajitayarishe kuingia huko. Kisha upelekwe mbele kidogo na kuwekwa tena chini na kisha ubebwe kwa mara ya tatu na kupelekwa hadi pembeni ya kaburi, na katika mara ya nne uingizwe kaburini taratibu. 

Uhusiano wa kiwango fulani baina ya mwili wa Barzakhi na maisha ya kimaada huendelea kuwepo hata baada ya kuzikwa mwanadamu. Roho za waliofariki dunia huendelea kuwatembelea na kuwatazama jamaa na familia zao. Hali hii hutokea wakati wowote na kwa mtu yeyote lakini hutokea zaidi katika siku za Ijumaa. 

Bwana mmoja aliyejulikana kwa jina la Is'haq bin Ammar alimuuliza Imam Mussa al Kadhim (as) ambaye ni miongoni mwa maimamu watoharifu katika kizazi cha Mtume wetu Muhammad (saw) kwamba: Je, Muumini aliyefariki dunia huitembelea familia yake? Imam alisema: Ndiyo, Nilimuuliza: Kwa muda gani? Imam Kadhim (as) alisema: Kadiri ya utukufu wao. Baadhi yao hutembelea familia zao kila siku na wengine kila baada ya siku tatu na wa chini kabisa hutembelea familia zao kila siku ya Ijumaa. 

Is'haq bin Ammar aliuliza tena kwamba: Waumini hao hutembelea familia zao wakati gani siku ya Ijumaa? 

Imam Kadhim (as) alisema: Adhuhuri wakati wa kupinduka jua, wakati huo Mwenyezi Mungu SW huituma roho ya maiti akiwa pamoja na Malaika ili amuoneshe mambo yanayomfurahisha na kufunika mambo yanayotia huzuni na kusikitisha. (Usulul Kafi 3).