Kuwakirimu wazee ni wajibu wetu sote
Tarehe Mosi Oktoba dunia iliadhimisha Siku ya Wazee Duniani.
Kipindi cha uzeeni sawa kabisa na kipindi cha utotoni au ujana ni miongoni mwa awamu za maisha ya mwanadamu kwa tofauti kwamba, vipindi cha utotoni na ujana vimejaa nishati na utanashati lakini kipindi cha uzeeni kinaandamana na kunyong'onyea na kupungua harakati za kimwili. Mwaka 1982 Umoja wa Mataifa ulianzisha Baraza la Dunia la Wazee na mwaka huo huo uliwasilisha mpango wa kuainisha siku ya kimataifa kwa ajili ya wazee. Mwaka 1990 baraza hilo liliiainisha tarehe Mosi Oktoba kuwa Siku ya Wazee Duniani kwa shabaha ya kuwakirimu, kuwaenzi na kutafuta njia za kutatua na kukidhi mahitaji ya wazee.
Katika maadhimisho ya mwaka huu ya Siku ya Wazee Duniani Umoja wa Mataifa ulichagua maudhui ya kupambana na ubaguzi unaofanyika kwa mujibu wa umri ambako kumejadiliwa mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na mtazamo hasi na wa kibaguzi kuhusu wazee na madhara yake kwa watu wa tabaka hilo.
Ubaguzi wa kiumri au Ageism ni kumbagua mtu au kufanya ubaguzi dhidi ya kundi la watu kwa msingi wa umri wao. Sheria ya kupiga marufuku ubaguzi kwa msingi wa umri wa mtu katika nyanja za kazi na ajira inatekelezwa katika baadhi ya nchi duniani kama vile Uingereza, Marekani, Denmark, Ireland na Australia. Sheria hiyo inaambatana na zile za kupiga marufuku ubaguzi wa kijinsia na ubaguzi wa kimbari. Sheria hiyo ya marufuku ya ubaguzi kwa msingi wa umri wa mtu kwa hakika inazilazimisha serikali kudhamini ajira na kazi kwa ajili ya wazee na kuzuia ubaguzi unaofanywa na waajiri dhidi ya watu wa tabaka hilo katika masoko ya ajira na kazi.
Maana ya kuwabagua watu kwa msingi wa umri katika masuala ya kazi na ajira ni mwajiri kumbagua kibarua au mfanyakazi wake kutokana na umri na miaka yake. Ubaguzi huu una sura mbalimbali ambazo baadhi zinaonekana waziwazi, kama mtu kufukuzwa kazi kwa sababu ya uzee wake, na mara nyingine ubaguzi huo unafanyika kwa njia isiyo ya moja kwa moja kama kutoa maoni na tathmini ya wafanyakazi na waajiriwa kwa msingi wa umri wao. Mashirika ya wafanyakazi yanasema kuwa, ubaguzi unaofanyika kwa msingi wa umri (ageism) ndio unaoonekana zaidi katika maeneo ya kazi. Ubaguzi huo umekita mizizi na kuwa jambo la kawaida katika baadhi ya kazi kama za vyombo vya habari na matangazo kiasi kwamba, baada ya kupita miaka mingi sasa suala hilo linaonekana kukubalika na halipingwi na yeyote.
Msingi wa sheria nyingi ni kuzuia ubaguzi dhidi ya watu wenye umri wa chini ya miaka 65 katika mazingira ya kazi. Sheria ya kuzuia ubaguzi wa aina hii inahusu masuala kadhaa ambayo yote kwa pamoja yanaunda kanuni ya kuzuia ubaguzi kwa msingi wa umri wa mfanyakazi. Kwa mujibu wa sheria hiyo, mwajiri hapaswi kuainisha mpaka wa umri katika masharti ya kuajiriwa. Vilevile mwajiri anayemfukuza kazi mfanyakazi wake kutokana na hali ya umri wake au kumnyima fursa ya kupata elimu, hutambuliwa kuwa amekiuka sheria hiyo.
Katika upande wa kijamii pia wazee hukumbana na mambo mengi katika maisha yao ya kila siku. Baadhi ya mambo hayo ni kustaafu, kipindi cha kukatika hedhi, watoto kuwapelekwa wazazi wao kwenye vituo na nyumba za wazee badala ya kuishi nao wao wenyewe, kufariki dunia mke au mume na kadhalika. Ala kulli hal, tatizo kubwa zaidi la wazee ambalo pia husababisha usumbufu na matatizo kwa ndugu na jamaa zao ni kudhoofika kwa afya zao, kupoteza uhuru na hali ya kujitegemea, kuhisi upweke na hata kujihisi kwamba hawathaminiwi tena katika mahusiano yao na watu wengine.
Mwanzoni mwa uhai wake, mwanadamu huwa kiumbe ajizi ambaye huvuka vipindi mbalimbali vya kukua na kukomaa kimoja baada ya kingine. Katika kipindi cha ujana, mwanadamu hupata uwezo mkubwa wa kimwili na katika umri wa kati (baina ya miaka 40 na 60) hufikia kilele cha ukomavu na ukamilifu wa kiroho. Baada ya hapo huanza safari ya kuporomoka na kurejea katika kipindi cha udhaifu na kupoteza uwezo wa kimwili. Qur'ani tukufu inatupa picha ya mwenendo huu wa maisha ya mwanadamu katika aya ya 54 ya Suratu Rum inayosema: Mwenyezi Mungu ndiye aliyekuumbeni katika udhaifu, kisha akajaalia nguvu baada ya udhaifu, kisha akajaalia udhaifu na uzee baada ya nguvu. Anaumba atakavyo. Naye ndiye Mjuzi, Mwenye uweza.
Katika dini ya Uislamu wazee wamepewa heshima makhsusi, na watu wote wa jamii wamefaradhishiwa kuwalinda na kuwashughulikia watu wa tabaka hilo. Kwa sababu hiyo Uislamu umeweka sheria zinazohusiana na wazee ili watu wa jamii waliangalie tabaka hilo kwa jicho la heshima na taadhima. Utukufu wa wazee unatokana na kwamba, wametekeleza ipasavyo risala yao katika panda shuka na misukosuko ya maisha na sasa wamestaafu na kuwa kandokando ya watu wa jamii na familia wakiwa na uzoefu na tajiriba kubwa ya maisha.
Dini tukufu ya Uislamu imehimzia sana kuwakirimu na kuwaheshimu wazee kwa kadiri kwamba, Mtume Muhammad (saw) anasema kuwa: Kuwaheshimu wazee Waislamu ni kumheshimu Mwenyezi Mungu. (Usulul Kafi:3-240). Vilevile anasema katika hadithi nyingine kwamba: Mtu anayemkirimu na kumuheshimu mzee, Mwenyezi Mungu atampa amani mbele ya mashaka na matatizo ya Siku ya Kiyama. (al Kafi: 2-658) Katika hadithi nyingine Mtume Muhammad (saw) anasema: Waheshimuni wazee ili mpate kuheshimiwa na watoto wenu. (Ghurarul Hikam).
Uislamu wapenzi wasikilizaji, umewahimiza wanadamu kuwaheshimu na kuwakirimu wazee na kuwa na huruma na upole kwa wadogo. Suala hili huzidisha upendo na baraka ndani ya familia. Si hayo tu bali Mtume wa rehma, Muhammad (saw) anakutaja kuwaheshimu na kuwakirimu wazee kuwa ni sifa inayompa mwanadamu ustahiki wa kuwa rafiki wa mtukufu huyo ambayo hapana shaka ni daraja kubwa sana. Anasema katika hadithi iliyopokewa katika kitabu cha Usulul Kafi kwamba: Warehemuni watoto na wakirimuni na kuwaheshimu wazee ili mupate kuwa marafiki zangu. (al Kafi: 2-316)
Miongoni mwa vielelezo vya kuwaheshimu wazee ni kutowaita kwa majina yao, kusimama wanapoingia, kutowatangulia wakati unapotembea nao, kutozungumza nao kwa sauti kubwa na ya juu, kukidhi mahitaji yao, kuwahudumia na kuwaangalia katika kipindi hicho cha uzee na udhaifu.
Imam Zainul Abidin Ali Sajjad (as) ambaye ni miongoni mwa wajukuu watukufu wa Mtume (saw) anasema: Miongoni mwa haki za mzee ni kumthamini na kumheshimu, kama atakuwa na fadhili katika dini umkirimu na kumuenzi, mtangulize mbele yako, usikabiliane naye kwa maneno ya uhasama wakati unapohitilafiana naye, usimtangulie wakati wa kutembea, usimuone kuwa ni mjinga na kama ataamiliana na wewe isivyo basi stahamili mabaya yake….
Kwa ufupi ni kuwa, wazee kwa ujumla wanastahiki kupewa heshima na taadhima, na pale mzee anapokuwa baba au mama basi jukumu hilo huwa kubwa na zito zaidi. Baba na mama huhitaji upendo na mazingatio makubwa zaidi katika kipindi cha uzeeni kuliko watu wengine. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana Qur'ani tukufu inatukataza hata kuwaudhi jambo na neno dogo tu kama kuwaambia "ah!".
Mwenyezi Mungu SW anasema katika aya ya 23 ya Suratu Israa kwamba: Na Mola wako Mlezi ameamrisha kuwa, msimuabudu yeyote ila Yeye tu, na wazazi wawili muwatendee wema. Mmoja wao akifikia uzee, naye yuko kwako, au wote wawili, basi usimwambie hata: Ah! Wala usiwakemee, na sema nao kwa msemo wa hishima.
Tofauti na utamaduni wa Kimagharibi ambao unakuona kuwepo wazee ndani ya familia kuwa ni mzigo na usumbufu na wanafanya kila wawezalo kuhakikisha kwamba wazee hawabani uhuru wao binafsi na wanachukua hatua ya kuwatupilia mbali kwa kuwapeleka kwenye vituo na nyumba za wazee, Uislamu umewakirimu, kuwaenzi na kuwathamini na kuwasisitiza wafuasi wake kuchunga haki zao na kutumia tajiriba na uzoefu wao.
Nafasi na makazi ya wazee katika mtazamo wa Uislamu si nyumba za wazee bali ni ndani ya familia yenye upendo, mshikamano na utanashati. Wazee wanapaswa kuwa taa na nuru ya nyumba zetu na inatupasa daima kunufaika na fikra na uzoefu wao wa muda mrefu na kuwafanya washauri wetu wakati wa kutaka kuchukua maamuzi.