Imam Ridha AS na risala yake iliyojaa siri za afya
Leo mji mtakatifu wa Mashhad umetanda huzuni na majonzi katika haram ya Ali bin Musa Ridha AS. Idadi kubwa ya waombolezaji wamefika katika haram hiyo kwa ajili ya kuombleza. Leo ni siku ya kukumbuka kuuawa shahidi Imam Ali bin Musa Ridha AS ambaye ni kutoka katika kizazi kilichotakasika cha Mtume Muhammad SAW.
Imamu huyo mkarimu ambaye alikuwa mbeba bendera ya Wilaya, katika kipindi chote cha maisha yake yaliyojaa baraka aliufungulia Umma milango ya hekima na maarifa na hivyo akawa kigezo cha ucha Mungu na ubora kwa lengo la kufikia saada. Tunachukua fursa hii kutoa salamu zetu za rambi rambi kwa mnasaba wa kukumbuka kuuawa shahidi Imamu huyu mkubwa na kuwakaribisha kusikiliza machache tuliyowaandalia kumhusu.
Imam Ridha AS aliishi sehemu ya maisha yake katika zama za utawala wa Ma'amun, khalifa wa silisili ya Bani Abbas. Ma'amun alikuwa mtu mwenye ujanja wa kisiasa na hila na alijiarifisha kama mtu apendaye elimu.
Mara kwa mara alikuwa akiandaa vikao vya kielimu vilivyohudhuriwa na Imam Ridha AS na wasomi wengine wa kidini na kimadhehebu ili wafanye midahalo.
Lengo la Ma’amun lilikuwa ni kutia dosari shakhsia ya kielimu ya Imam. Lakini kinyume na alivyotarajia Ma’amun, vikao hivyo vilipelekea shakhsia iliyojaa fadhila na elimu ya Imam Ridha AS kubainika wazi kwa wote. Hii ni kwa sababu Imam Ridha AS alijibu kikamilifu maswali yote aliyoulizwa katika nyanja mbali mbali za kielimu. Ujuzi mkubwa na elimu ya hali ya juu ya Imam ni jambo ambalo lilipelekea Ma’amun kukiri kuwa: “Hakuna mtu mwenye ujuzi mkubwa duniani kumliko Hadhrat Ridha.”
Imam Ridha AS alibainisha moja ya sifa muhimu za Imamu kwa kusema Imamu anatakiwa kuwa na elimu na uono wa mbali au hekima. Imam Ridha AS amenukuliwa akisema: “Elimu na ujuzi wa Imam daima huwa unastawi, huwa ni mpole, mwenye kufahamu kikamilifu masuala ya kisiasa na huwa ni mwenye kustahiki uongozi. Imam ni mlinzi wa dini ya Mwenyezi Mungu na kuwalingania watu kwa hekima, mawaidha, uzuri na hoja za wazi ili waelekee katika njia ya Mwenyezi Mungu.”
Imam Ridha AS kwa kuzingatia kikamilifu matukio ya kielimu na kisiasa ya zama, alitekeleza ipasavyo risala yake kwa lengo la kuhuisha Uislamu wa kweli na kuwaongoza wanaadamu katika njia ya haki. Kwa kutumia fikra zake za Uislamu halisi, mtukufu huyo aliwaondoa wanaadamu kutoka njia potofu na kuwaongoza katika njia iliyonyooka. Kwa hakika Imam Ridha AS alikuwa mfano wa daraja la mawasiliano baina ya waja na Allah SWT na hivyo kuwafanya waweze kufahamu kwa kina mafundisho yenye thamani ya Kiislamu. Daima mtukufu huyo alikuwa akitoa wito kwa watu kutafakari na kuwa na tadbiri katika dini kwa kusema: “Ibada si kufunga na kuswali kwa wingi bali ibada (ya kweli) ni kutafakari sana kumhusu Allah SWT.”
Miongoni mwa Maimamu waliotakasika, Imam Ridha AS alipata lakabu ya “Alim Aali Mohammad” yaani ‘Msomi wa Kizazi cha Mohammad.'
Hali bora zaidi kwa mwanaadamu ni kunyenyekea na kuwa na khushuu mbele ya Allah SWT. Kuhusu hili Imam Ridha AS alisema: “Hali ya kuwa karibu zaidi mja na Allah SWT ni katika hali ya kusujudu na hili linaenda sambamba na ile kauli ya Allah Tabaraka wa Ta’ala aliposema: ‘Sujudu ili ukaribie.”
Ali bin Musa Ridha AS katika hadithi anasema hivi: “Hakuna mja anayefikia uhakika wa imani isipokuwa awe na sifa tatu: Maarifa na ufahamu katika dini, msimamo wa wastani katika maisha na subira katika misiba.”
Kimsingi ni kuwa mwanaadamu hufikia imani kamili anapokuwa na maarifa kamili, khushuu na kutekeleza faradhi za kidini kwa uono wa mbali. Katika utumizi wa fedha katika maisha vile vile hapaswi kuwa na misimamo ya kufurutu mipaka na katika matatizo ya maisha Mwislamu anapaswa kuwa mstahamilivu na kukubali takdiri ya Mwenyezi Mungu.
Katika zama za khalifa wa Bani Abbas, Ma’amun baadhi ya wakati alikuwa akiwaita wasomi wa taaluma ya tiba kutoka maeneo mbali mbali kwa lengo la kufanya midahalo ya kisayansi ili kwa njia hiyo aweze kupata itibari.
Katika moja ya vikao hivyo vya kisayansi alihudhuria Imam Ridha AS na Ma’amun ambapo kundi la matabibu na wanafalsafa maarufu wa Nishabur walihudhuria. Walitoa hotuba nyingi kuhusu masuala ya kitiba. Imam Ridha AS alikaa kimya na kutosema chochote. Ma’amun alumwambia hivi Imam Ridha AS: "Ya Abal Hassan! Una nini cha kusema kuhusu maudhui hizi?"
Imam alisema: “Nina maoni ambayo usahihi wake nimeupata kupitia tajriba ya muda mrefu. Zaidi ya hayo nina elimu ambayo waliotangulia waliniachia na kuna mambo ambayo kila mwanaadamu anapaswa kuyajua. Nitakusanya nadharia hizi na tajriba pamoja na yote yanayohitajika katika uga huu.”
Imam alitayarisha risala yake na kumkabidhi Ma’amun. Ili kuonyesha umuhimu wa risala hiyo, Ma’amun aliamuru iandikwe kwa wino wa dhahabu na ihifadhiwe katika hazina ya serikali. Ni kwa sababu hii ndio ikapewa jinal la “Risalatul Dhahabiyya.” Hivi ndivyo mjumuiko huu wa maelezo ya kitiba ya Imam Ridha AS kuhusu afya ya mwili ulikusanywa katika risala hiyo iliyopewa jina la Dhahabiyya. Katika risala hii Imam amesherehesha faida za vyakula mbali mbali, mbinu za kitiba na kiafya pamoja na namna ya kukabiliana na maradhi ya kiroho na kinafasi.
Risala hii imejaa siri nyingi. Katika risala hii Imam ameandika hivi: “Mwenyezi Mungu hajaufanya mwili uwe na ugonjwa isipokuwa ameujaalia uwe na dawa ya kutibu…”
Katika sehemu ya kitabu hicho chenye thamani ambacho pia ni maarufu kama ‘Tibb Ar Ridha’, Imam Ridha AS amesema: “Iwapo watu wataridhika kula chakula kichache, miili yao itakuwa na mlingano.”
Risala hii ya tiba iliyojaa balagha ni kati ya vitabu vyenye thamani kubwa vya Kiislamu katika uga wa tiba. Kitabu hicho kimebainisha maudhui mbali mbali za kitiba kama vile biolojia, fiziolojia, kemia, lishe n.k. Kitabu hiki kinamuongoza mwanaadamu katika maisha bora yenye afya ambayo ni neema kubwa ya Allah SWT.
Naam, Imam Ridha AS alikuwa shakhsia adhimu na alim mwenye fadhila. Alikuwa na ubora wote wa kimaanawi na kimaadili. Alichukua jukumu la Uimamu na kuuongoza Umma wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 35. Mtukufu huyo alikuwa kipenzi cha Umma. Lakini Ma’amun, Khalifa wa Kiabbasi hakuweza kustahamili mahaba makubwa ya watu kwa Imamu Ridha AS pamoja na karama zake nyingi. Katika upande mwingine hakuweza kuzuia ushawishi wa kimaanawi wa Imam Ridha na hivyo akawa anamtazama kama kizingiti katika malengo yake machafu. Kwa hivyo Ma’amun alitumia kila njama kuhakikisha anamuondoa Imam katika njia yake. Alitekeleza njama yake hiyo chafu katika siku ya mwisho ya mwezi wa Safar mwaka 203 Hijria na hatimaye kumuua shahidhi Imam Ridha AS.
Leo tunakumbuka tukio hilo chungu la kuuawa Imamu huyu mkubwa wa Umma. Hivi sasa nchini Iran katika mji mtakatifu wa Mashhad, maelfu ya watu kutoka kila pembe ya dunia wamekusanyika kwa ajili ya ziyara katika Haram Takatifu na iliyojaa nuru ya Imam Ridha AS huku wakimtumia salamu na kupata karama zake. Tunamuomba Mwenyezi Mungu atujaalie nasi tupate taufiki ya kumzuru Imamu huyu mkubwa na tupate kunufaika na nuru ya muongozo wake.
Salamu ziwe juu yako ewe Ali Bin Musa Ridha! Salamu ziwe juu yako ewe Imamu uliyejitahidi kwa ajili ya ukweli na uadilifu katika njia ya haki!