Hija na Visa Vyenye Ibra
(last modified Sun, 19 Aug 2018 12:14:34 GMT )
Aug 19, 2018 12:14 UTC
  • Hija na Visa Vyenye Ibra

Assalamu Alaykum wasikilizaji wapenzi popote pale mlipo. Tuko kwenye msimu wa ibada tukufu ya Hija. Kwa mnasaba huo Radio Tehran imekuandalieni kipindi hiki maalumu cha Hija na Visa Vyenye Ibra. Kisa chetu cha kwanza kitahusu Hija ya Kudumu Daima Dawamu.

Abduljabar Mustawfi alikuwa anakwenda Makka kuhiji, mfukoni mwake akiwa na dinari elfu moja za dhahabu za kugharimia safari yake. Moyoni alijawa na shauku kubwa ya kuizuru Nyumba tukufu ya Allah; na mawazo aliyokuwa akilini mwake yaliufanya mwili wake mzima usisimke kwa furaha. Muda wote alikuwa akiwaza juu ya lahadha atakapoiona Nyumba ya Mwenyezi Mungu na kufanya munajati na kunong'ona na Mola wake Mwenye huruma na Mrehemevu. Akiwa njiani katika safari yake, alifika mjini Kufa. Alikata kichochoro kimoja baada ya chengine cha mji huo huku amezama kwenye fikra hizo. Mara akafika mahali palipokuwa na magofu, akamkuta hapo mwanamke anafukua fukua kutafuta kitu kwenye magofu yale. Mara mwanamke yule akauona mzoga wa kuku kwenye kona moja ya magofu. Aliunyakua na kuuficha haraka kwenye nguo yake kisha akashika njia kwenda zake. Abduljabar akajiuliza nafsini mwake: mwanamke huyu ndo anafanya nini, kwani hajui kama kula nyamafu ni haramu?

Aya ya 173 ya Suratul Baqarah:

إِنَّمَا حَرَّمَ عَلَیْکُمُ الْمَیْتَةَ وَالدَّمَ وَلَحْمَ الْخِنْزِیرِ وَمَا أُهِلَّ بِهِ لِغَیْرِ اللَّهِ ۖ فَمَنِ اضْطُرَّ غَیْرَ بَاغٍ وَلَا عَادٍ فَلَا إِثْمَ عَلَیْهِ ۚ إِنَّ اللَّهَ غَفُورٌ رَحِیمٌ

Yeye amekuharimishieni mzoga tu na damu na nyama ya nguruwe na kilicho tajiwa, katika kuchinjwa kwake, jina la asiye kuwa Mwenyezi Mungu. Lakini aliye fikiwa na dharura bila ya kutamani wala kupita kiasi, yeye hana dhambi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.

Abduljabar aliamua kumfuata mwanamke yule. Akajisemea mwenyewe; bila shaka huyu mwanamke ana hali ngumu kimaisha. Lazima nimfuate nikaone hali aliyonayo.

Mwanamke yule alichepuka huku akipenya kwa kasi kichochoro kimoja na kutokea chengine. Mara akaingia ndani ya nyumba moja. Watoto wake walimkimbilia na kumzunguka. Wakamwambia: mama tuhoi kwa njaa, umetuletea kitu gani? Mama yule alijibu kwa aibu: Nimeleta kuku ili nikufanyieni kuku wa masalo.

Abduljabar alikuwa amejibanza kipembeni. Machozi yalimbubujika aliposikia maneno yale. Aliwaendea majirani kuwauliza hali ya mama yule. Wakamwambia: Huyu ni mke wa Abdullah bin Zayd Alawi. Mumewe ameuliwa na Hajjaj akawafanya wanawe mayatima. Staha aliyonayo mama huyu inamfanya ashindwe kumwomba mtu kitu.

Abduljabar Mustawfi alijisemea moyoni mwake: kama unataka kutekeleza Hija, Hija yako wewe ni hii. Palepale akakifungua kiunoni kifuko chake cha sarafu za dhahabu, akagonga mlango wa nyumba ya mama yule. Akamkabidhi kifuko kile na kwenda zake.

Mwaka ule Abduljabar alibakia mjini Kufa na kufanya kazi ya kuteka na kuuza maji. Wakati mahujaji walipokamilisha Hija na kurudi makwao, walipokaribia mjini Kufa, watu mbalimbali, akiwemo na yeye Abduljabar Mustawfi, walitoka nje ya mji kwenda kuwalaki. Walipoukaribia msafara wa mahujaji, mara mpanda ngamia mmoja akachomoza mbele, akamsalimia Abduljabar na kumwambia: "Ee bwana Abduljabar, nimekuwa nikikutafuta tangu siku ile uliponikabidhi dinari elfu moja Arafa. Pokea kifuko cha sarafu zako za dhahabu." Mpanda ngamia yule akamkabidhi Abduljabar kifuko chenye dinari elfu kumi na kutoweka.

Wakati uleule Abduljabar Mustawfi akasikia sauti inamsemeza: "Ewe Abduljabar, kwa dinari elfu moja ulizotoa katika njia yetu, tumekuletea dinari elfu kumi; na tumewaumba malaika kwa sura yako, ambao kwa muda wote wa uhai wako watakuwa kila mwaka wanakwenda kuhiji kwa ajili yako, ili waja wangu wajue kwamba, hakuna wema wowote unaopotea kwangu Mimi."

Aya ya 56 ya Suratu Yusuf:

Mwenyezi Mungu anasema akatika aya hiyo ya 56 ya Suratu Yusuf ya kwamba:

نُصِیبُ بِرَحْمَتِنَا مَنْ نَشَاءُ ۖ وَلَا نُضِیعُ أَجْرَ الْمُحْسِنِینَ

Tunamfikishia rehema zetu tumtakaye, wala hatupuuzi malipo ya wafanyao mema.

Wapenzi wasikilizaji, kisa chetu cha pili katika kipindi chetu cha leo kinahusu sifa za Hujaji wa kweli.

Bwana mmoja aliyetoka mji wa mbali aliweza baada ya tabu na mashaka mengi kufika mji mtukufu wa Makka kwa ajili ya kuhiji na kuizuru Nyumba ya Allah ya Al-Kaaba. Mapenzi makubwa na hamu na shauku isiyo na kifani aliyokuwa nayo ya kuizuru Al-Kaaba na kaburi la Bwana Mtume Muhammad SAW vilikufanya kuvumilia tabu na mashaka yote yaliyomfika liwe jambo jepesi kwake. Alitekeleza amali za Hija kwa uzuri ulioje huku akiwa na matumaini makubwa moyoni mwake ya kutakabaliwa amali zake na Allah. Aliandamana na mahujaji wenzake hadi ardhi ya Mina kutekeleza amali zilizopasa kufanywa huko. Usiku alipokuwa amelala huko Mina aliwaona usingizini malaika wawili wamemteremkia kutoka kwa Allah wakausimamia umma wa mahujaji waliokuwepo pale. Wakawa wanamwashiria hujaji mmoja mmoja na kusema: Huyu ni hujaji; ikiwa na maana Hija yake imekubaliwa na Allah. Lakini kuhusu mahujaji wengine wakawa wanasema: Huyu si hujaji na huyu si hujaji. Wakati malaika walipomfikia yeye, yule bwana aliwasikia wakisema: Mtu huyu si hujaji. Yule bwana alizinduka kutoka ndotoni akiwa amejawa na hofu na wasiwasi. Alitupa jicho huku na kule. Majonzi makubwa yalimjaa moyoni. Alinong'ona taratibu na kwa unyonge na Mola wake: Ee Mola wangu, nimevumilia tabu na mashaka yote haya kwa ajili ya kuja kukuzuru. Nimekuja kutekeleza amri yako ya Hija. Imekuwaje basi hija yangu haijatakabaliwa? Aliwaza nafsini mwake huku akifikiria amali na matendo aliyofanya huko nyuma. Atakuwa amefanya nini mpaka akabaidishwa na rehma za Allah namna ile. Mahali ambapo mahujaji hufutiwa na kusamehewa madhambi yao, yeye atakuwa amefanya dhambi gani iliyoshinidikana kusamehewa!

Akafikiri kwamba huenda atakuwa hajakamilisha ipasavyo malipo ya Zaka na Khumsi ya mali zake.  Akawaandikia barua wanawe na kuwaambia: Mimi mwaka huu nitabaki Makka. Zihesabuni mali zangu zote. Kama kuna fungu lolote la Khumsi au Zaka linaloniwajibikia nilipieni.

Barua ilipowafikia watoto wake, walitekeleza amri ya baba yao kama alivyowaelekeza. Mwaka uliofuatia, bwana yule akatekeleza tena ibada tukufu ya Hija. Wakati alipokuwa katika ardhi ya Mina, usiku akiwa amelala aliota tena ndoto ileile. Na mara hii pia malaika wawili walipomfikia yeye walisema: Huyu si hujaji. Alizinduka ghafla usingizini huku akiwa na tahayuri na huzuni kubwa. Ilimpasa ajue, kwa nini Hija yake haitakabaliwi. Ndipo akakumbuka kuwa ana jirani yake masikini mwenye nyumba ndogo na ya kinyonge. Wakati bwana yule alipotaka kujenga nyumba yake ya ghorofa, jirani yake huyo alimwomba asijenge jengo refu sana kwa sababu litaizuia nyumba yake ndogo kupata mwanga wa jua. Lakini yule bwana hakuyajali maneno yake akaamua kujenga nyumba ya ghorofa kadhaa. Hivyo akajisemea mwenyewe: Huenda ni kwa sababu hii Mwenyezi Mungu haikubali Hija yangu. Bwana yule akashika tena kalamu na karatasi kuwaandikia watu wake barua na kuwaambia: Mwaka huu pia mimi nitabaki Makka. Nyinyi nendeni mkazungumze na jirani yetu fulani, mumtake akuuzieni nyumba yake; kama atakataa, basi zibomoeni ghorofa mbili za nyumba yangu ili nyumba ya jirani isikose mwanga wa jua. Wanawe wakamfuata jirani yao, lakini hakuwa tayari kuuza nyumba yake. Kwa hivyo wakawa hawana njia nyingine isipokuwa kuibomoa nyumba yao ili jirani yao awe radhi nao. Kwa mara nyingine msimu wa Hija ukawadia na wakati yule bwana alipokuwa katika ardhi ya Mina aliota tena ndoto ileile, lakini mara hii hali ilikuwa tofauti na mara zilizopita. Malaika wawili walipomsimamia mbele yake walisema: Mtu huyu ni hujaji, mtu huyu ni hujaji...

Wapenzi wasikilizaji, Bwana Mtume Muhammad SAW amesema: Watu wawili, hawatotizamwa na Allah kwa jicho la rehma Siku ya Kiyama; mwenye kukata udugu na mwenye kumtendea ubaya jirani yake. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../