Hekima na busara katika fikra za Imam Musa al Kadhim AS
Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika kipindi hiki maalumu tulichokuandalieni mnasaba wa kukumbuka siku aliyozaliwa Imam Mussa al Kadhim AS. Ni matumaini yangu utakuwa nami hadi mwisho wa makala hii.
Wapenzi wasikilizaji, Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema amewaneemesha waja Wake kwa kuwatumia Mitume na wajumbe Wake na kuwapa vitabu vitakatifu vya kuwaongoza wanadamu kwenye njia iliyonyooka. Mitume, Manabii na mawalii wa Mwenyezi Mungu ni hujja wa Allah katika ardhi na ni vigingi vya kuwaepusha wanadamu na ghadhabu za Mwenyezi Mungu. Katika sura ya 8 ya al Anfal ya Qur'ani Tukufu, aya ya 33, Mwenyezi Mungu anasema: "Na Mwenyezi Mungu hakuwa wa kuwaadhibu (hao wapotevu) wakati wewe upo pamoja nao." Mitume wa Mwenyezi Mungu ni waonyaji na waongozaji wa wanadamu kuelekea kwenye saada na ufanisi wa duniani na Akhera. Mitume na wajumbe hao wa Mwenyezi Mungu ni miongoni mwa vielelezo vya rehma na mapenzi ya Allah kwa waja Wake. Watu hao adhimu walibeba bendera ya kuwaongoza wanadamu katika kipindi chote cha historia na kuwalingania watu waliopetea njia ya uongofu na kuwaelekeza kwenye nuru na mwanga; na hakujaalia Mwenyezi Mungu ardhi ipitishe walau sekunde moja bila ya kuwa na mawalii na hujja Wake.Bwana Mtume Muhammad SAW na Ahlul Bait wake watoharifu nao pia walibeba bendera hiyo ya kuwaongoza wanadamu katika kipindi cha giza kubwa la dhulma, ujinga na ukandamizaji na walikabiliana na machungu mengi katika njia hiyo takatifu. Walikuwa manahodha mahiri walioongoza merikebu ya umma wa Kiislamu katika bahari yenye mawimbi makali na kuwafikisha ufukweni kwa amani na salama.Mwezi 7 Mfunguo Tano Safar, inasadifiana na siku ya kukumbuka alipozaliwa Imam Musa al Kadhim AS mmoja wa watu wa nyumba toharifu ya Bwana Mtume Muhammad SAW. Katika makala hii ya leo tutatupia jicho baadhi ya mafundisho yaliyojaa busara na hekima ya mtukufu huyo katika sira na maisha yake yaliyojaa ibra na mafunzo ambayo kama tutayazingatia na kuyafanyia kazi, basi tutapata saada na ufanisi hapa duniani na huko Akhera. Tab'an tutaanza na historia fupi ya kuzaliwa kwake.
Kama tulivyotangulia kusema, Imam Mussa al Kadhim AS alizaliwa mwezi 7 Mfunguo Tano Safar mwaka 128 Hijria katika eneo la al Abwaa nje kidogo ya mji mtakatifu wa Madina. Wakati wa kuzaliwa kwake, baba yake yaani Imam Jaafar Swadiq AS alisema: Mwenyezi Mungu SWT amenitunuku mwanadamu bora.Baada ya kuaga dunia baba yake, Imam Kadhim AS alishika hatamu za Uimamu na kuongoza umma wa Kiislamu kwa kipindi cha miaka 35. Kipindi cha uimamu wake kilijaa misukosuko na mashaka mengi na kiliambatana na kuchanua utawala wa wafalme wa Bani Abbas. Wafalme kama Haroun ar Rashid waliongoza dola ya Waislamu kwa kutumia hadaa na ujanja na kutenda dhulma kubwa dhidi ya Waislamu sambamba na kupotosha mafundisho sahihi ya dini hiyo tukufu ya Mwenyezi Mungu. Wakati wa kampeni za kuingia madarakani na kuwapindua wafalme wa Bani Ummaya, watawala wa Bani Abbas walijionesha kuwa ni wapenzi wa Watu wa Nyumba ya Mtume SAW na walidai kuwa wanaendesha kampeni hizo ili kurejesha utawala wa dola ya Waislamu kwa Ahlul Bayt wa Mtume AS baada ya kuporwa na ukoo wa Bani Umayya. Hata hivyo Bani Abbas walikwenda kinyume kabisa na Ahlul Bait AS na waliwaweka katika hali ngumu na mashaka makubwa. Hata hivyo hali hiyo haikumzuia Imam Musa al Kadhim AS kudumisha harakati yake ya kuleta marekebisho katika dini ya babu yake Bwana Mtume Muhammad SAW na katika fikra za umma wa Kiislamu hususan kati ya wasomi na kuwaondoa watu katika upotofu wa kifikra na kiitikadi uliokuwa ukienezwa na watawala wa wakati huo. Juhudi za kielimu za Imam AS ziliulinda na kuuwekea kinga Uislamu mbele ya wimbi kali la hujuma ya fikra potofu. Mtukufu huyo alifanya jitihada kubwa kuhakikisha kwamba, itikadi halisi za Uislamu zinalindwa vilivyo. Alikuwa akiwahimiza Waislamu kuhudhuria vikao vya kielimu na wasomi, na anasema katika moja ya nasaha zake kwa Waislamu kwamba: "Shirikini kwa wingi katika majlisi na vikao vya wasomi hata kama mtalazimika kusimama juu ya vidole vya mikono yenu, kwani Mwenyezi Mungu huhuisha nyoyo zilizokufa kwa nuru ya elimu na hekima, kama anavyohuisha ardhi iliyokufa kwa maji ya mvua."
*******
Hapana shaka kuwa akili ni miongoni mwa atia na zawadi kubwa za Mwenyezi Mungu kwa mwanadamu. Mtume Muhammad SAW anasema: "Kudumu kwa uhai wa mwanadamu kunafungamana na akili yake, na hana dini mtu asiye na akili."Maana ya hadithi hiyo ya Mtume SAW ni kuwa akili ina umuhimu mkubwa katika mafundisho ya Kiislamu kwa kadiri kwamba, Bwana Mtume ameitaja kuwa ndio wenzo muhimu wa kutambua misingi na mafundisho ya Uislamu. Hadithi zilizopokewa kutoka kwa Mtume SAW na Ahlul Bait AS zinasisitiza kuwa, utukufu wa mwandamu na hadhi yake ya kuwa Khalifa wa Mwenyezi Mungu katika ardhi, una uhusiano wa moja kwa moja na ukamilifu wa akili yake. Uislamu na kitabu kitukufu cha Qur'ani vinasisitiza sana juu ya umuhimu wa kutumia akili na hekima. Aya za Qur'ani Tukufu daima zimetumia neno akili kwa sura ya kitendo na si kwa sura ya jina ili kusisitiza kwamba, suala muhimu zaidi ni kutumia akili na hikima na si kuwa na akili isiyotumiwa. Kuna aya nyingi sana za Qur'ani Tukufu zinazothibitisha hiyo. Katika Surat Muhammad aya ya 24 Mwenyezi Mungu anasema:
اَفَلا یَتَدَبَّرونَ القُرآنَ اَم عَلَی قُلوبٍ أَقفَالُهَا
Je! Hawaizingatii hii Qur'ani? Au kwenye nyoyo (zao) zipo kufuli?
Ikiwa na maana ya kwamba, kwa nini wanadamu hawa, hawatumii akili zao, wakazingatia yaliyomo ndani ya Qur'ani Tukufu, wakapata kuongoka, au kufuli zimefunga nyoyo zao na kuzifanya akili zishindwe kutumika inavyopasa? Maneno kama "afalaa yaaqilun," "afalaa yatadabarun," "afalaa yatadhakarun" n.k, yamejaa ndani ya Qur'ani Tukufu, yote yakiwahimiza watu kutumia akili zao vizuri.
******
Imam Kadhim AS kama walivyokuwa Maimamu wengine maasumu katika kizazi kitoharifu cha Bwana Mtume SAW, alifanya jitihada kubwa za kubainisha na kuweka wazi nafasi halisi ya akili na hekima katika mtazamo wa Uislamu na kwa sababu hiyo alimuhesabu mtu asiyetumia akili kuwa hana dini. Daima alikuwa akisema: "Tafuteni maarifa ya dini ya Mwenyezi Mungu, kwani kuelewa sheria za dini ya Mwenyezi Mungu ndio ufunguo wa kufikia daraja za juu za dini na dunia."Katika mafundisho matukufu ya Imam Musa al Kadhim AS kunaonekana suala jingine muhimu nalo ni kuwa dini inadhamini saada na ufanisi wa duniani na Akhera kwa sharti kwamba mwanadamu aifahamu na aielewe dini kwa njia sahihi. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana mtukufu huyo alisisitizia sana umuhimu wa kutumia akili na hekima. Alibainisha wazi nafasi na mchango wa akili na katika sehemu moja ya mafundisho yake, Imam Musa al Kadhim AS amenukuliwa akisema: Mwenyezi Mungu ana huja mbili, huja ya wazi na ya dhahiri, na huja ya batini na isiyo wazi. Huja ya wazi ni Mitume, Manabii na Maimamu, na huja ya batini ni akili." Ni kwa kutilia maanani hadithi kama hii ndiyo maana wanazuoni wa fiqhi ya Kiislamu wakaihesabu akili kuwa ni moja ya vyanzo vilivyo lazima kutumiwa katika kutolea ufafanuzi sheria za Kiislamu baada ya Qur'ani na Suna za Mtume SAW. Imam Musa al Kadhim AS alikuwa akisisitiza kwamba, dini na mafundisho ya Mwenyezi Mungu hayawezi kueleweka vyema bila ya kuwa na akili timamu na kwa sababu hiyo kutumia akili ipasavyo ni sharti la mtu kuwa na dini na hapana shaka kuwa dini haiwezi kufahamika isipokuwa kwa kutumia akili.Wapenzi wasikilizaji ni akili na hekima ndiyo inayoweza kupambanua baina ya jambo sahihi na lisilokuwa sahihi na hata kusadikisha au kukadhibisha yanayosemwa na Mitume wa Mwenyezi Mungu. Kutumia akili na hekima kumepewa umuhimu mkubwa sana katika maneno na mafundisho ya Imam Musa al Kadhim AS kwa kadiri kwamba, mtukufu huyo anaifungamanisha akili na saada ya dunia na Akhera. Mtukufu huyo anawausia wanadamu kumwomba Mwenyezi Mungu neema ya akili akisema: "Mtu anayetaka kujitosheleza bila ya kuwa na utajiri, kuwa na utulivu wa moyo bila ya kuhusudiwa na watu wengine na anayetaka usalama katika dini yake, anapaswa kumwomba Allah amkamilishie akili yake."
Wapenzi wasikilizaji, kutumia akili, kama ilivyo katika amali nyingine, kunahitaji mazoezi na juhudi kubwa. Ili kuweza kutayarisha uwanja mzuri wa kutumia akili na hekima, mwanadamu anapaswa kufanya mambo kadhaa maishani mwake ikiwa ni pamoja na kuketi na maulamaa na watu wenye hekima na na busara na kushauriana nao mara kwa mara. Imam Musa al Kadhim AS anasema kuhusu umuhimu wa suala hilo kwamba: "Kuketi na watu wenye dini humpa mtu sharafu na heshima ya dunia na Akhera na kushauriana na watu wenye busara na hekima huzidisha baraka, ustawi na taufiki ya Mwenyezi Mungu..."Vile vile Imam Mussa al Kadhim AS alikuwa akiwahimiza mno Waislamu kujiepusha kuketi na kusuhubiana na watu majahili na wajinga, akisisitiza kwamba suala hilo linamweka mtu mbali na njia ya haki na ufanisi. Anasema: Jiepushe kuketi na kusuhubiana na wajinga na wakimbie kama unavyokimbia mnyama mkali anayewinda wanadamu."Mpenzi msikilizaji, ibada na kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu kunamfanya mwanadamu kuwa mwingi wa hekima na busara. Humfanya mwanadamu kuwa tajiri kuliko matajiri wote kutokana nwa kwamba ibada humfanya amtegemee Mwenyezi Mungu katika kila kitu na kutosheka na anachoruzukiwa na Allah na kutokuwa na husda wala choyo kuhusu mali za wengine. Ni kwa sababu hiyo ndio maana watu watukufu wakawa wanawasisitizia sana wanadamu kujipinda kwa ibada na kujiweka karibu na Mwenyezi Mungu wakati wote. Hata mwanadamu anapokuwa anataka kutimiziwa haja zake, watuku hao wametuhimiza sana kupeleka maombi yetu kwa Mwenyezi Mungu na kukithirisha dua na kumsalia Mtume, yote haya ikiwa ni kutulea katika kuwa karibu na Mwenyezi Mungu na kutumia vyema akili zetu kwani akili inahukumu kuwa, mtu anapokuwa na haja hajisumbui kwenda kwa mtu ambaye ana uhakika hawezi kumkidhia haja yake. Katika kitabu cha Thawab al-A'maal kumenukuliwa hadithi kutoka kwa Imam Musa al Kadhim AS akitufundisha njia nzuri ya kuweza kukidhiwa haja zetu na Mwenyezi Mungu akisema: "Mtu anayesema baada ya swala ya Alfajiri na Magharibi na kabla ya kuketi kwenye miguu yake au kumzungumzisha mtu:
إِنَّ اللهَ وَ مَلائِکَتَهُ یُصَلُّونَ عَلَى النَّبِیِّ یا أَیُّهَا الَّذینَ آمَنُوا صَلُّوا عَلَیْهِ وَ سَلِّمُوا تَسْلیما
Hakika Mwenyezi Mungu na Malaika Wake wanamswalia Nabii. Enyi mlioamini! Mswalieni na mumsalimu kwa salamuNa akahitimisha kwa kusema:
الّلهُمَّ صَلِّ عَلی مُحَمَّد وَآلِ مُحَمَّد
Ewe Mola Wangu mshushie rehema Muhammad na Aali Muhammad - Mwenyezi Mungu humtimizia haja zake mia moja, sabini humu duniani na thelathini huko Akhera."
*******
Kama walivyokuwa Maimamu wengine wa nyumba toharifu ya Bwana Mtume Muhammad SAW, Imam Musa al Kadhim AS alikamilika katika sifa bora za kibinadamu ikiwa ni pamoja na hekima nyingi katika kila alilolitamka. Mbali na umuhimu wa kutumia akili na busara, kumenukuliwa hadithi nyingi pia kutoka kwa Imam Musa al Kadhim AS kuhusiana na wajibu wa kulinda haki za viumbe wengine hata wale ambao Mwenyezi Mungu hakuwapa uwezo wa kuzungumza na sisi wanadamu wa kawaida tukaweza kuwaelewa kama vile wanyama. Miongoni mwa haki za wanyama kwa mwanadamu ni kukidhi mahitaji yao ya kimsingi kama kuwapa chakula na maji, kwa sababu wanyama hawawezi kueleza matakwa na mahitaji yao. Hivyo basi kumfungia mnyama nyumbani na kumnyima neema hizo za Allah ni dhulma. Imam Musa al Kadhim amenukuliwa akisema: Mcheni Mwenyezi Mungu kuhusu viumbe wasiosema." Na bila ya shaka yoyote hayo ni katika mafundisho matukufu ya Bwana Mtume Muhammad SAW. Imam Ali bin Abi Twalib AS amesema: Siku moja Mtume SAW alipokuwa akitawadha, paka alimsogelea mtukufu huyo. Mtume SAW alitambua kwamba mnyama huyo ana kiu. Mtukufu huyo alimsogezea chombo kilichokuwa na maji na paka akanywa maji hayo. Kisha Mtume SAW akaendelea kutawadha."
Imam Musa al Kadhim AS alikuwa akihimiza mno wajibu wa kulindwa haki ya kimsingi kabisa ya wanyama yaani haki ya kuishi ikiwa ni pamoja kumtayarishia chakula, maji ya kunywa, makazi yanayofaa na kumdhaminia usalama. Sheria za Kiislamu pia zinawahimiza Waislamu kumlinda mnyama na maudhi na kutodhuru mwili wake. Wakati Imam Mussa al Kadhim AS aliposema: Mcheni Mwenyezi Mungu kuhusu viumbe wasiosema, aliulizwa na hadhirina: Ni viumbe gani hao wasiosema? Alijibu kwa kusema: Ni mbuzi, paka, njiwa na mithili yao."Wapenzi wasikilizaji, miongoni mwa mambo yaliyokuwa yakisisitizwa mno na Imam Musa al Kadhim AS ni ihsani. Tunaweza kusema kuwa, sifa hii ya ihsani na kutenda wema hata kwa viumbe wasiosema, haipatikana isipokuwa kwa wanadamu wenye imani thabiti ya Mwenyezi Mungu na Siku ya Malipo au watu ambao wao wenyewe walishawahi kukumbana na mashaka na tabu na wanajua vyema uchungu na maumivu ya watu wenye haja na matatizo ya kimaisha. Hii ni kwa sababu watu ambao hawaelewi vyema uchungu na matatizo hawawezi kuumizwa na matatizo ya wanadamu wenzao wala hawawezi kuwafikiria viumbe wengine. Katika kitabu cha Biharul Anwar kumenukuliwa hadithi kutoka kwa Imam Mussa al Kadhim AS akithibitisha moja ya sababu za watu kufanya ihsani na wema akisema: "Kufanya ihsani na kutenda wema hakuna thamani wala nafasi kwa mtu ambaye hajawahi kuonja shida na matatizo."
*******
Wapenzi wasikilizaji hayo ndiyo tuliyoweza kukuandalieni kwenye makala yetu ya leo kwa mnasaba wa kuadhimisha siku ya kuzaliwa Imam Musa al Kadhim AS, mmoja wa watu wa nyumba toharifu ya Bwana Mtume Muhammad SAW. Tumegusia historia fupi ya kuzaliwa kwake na tumejikita zaidi kwenye mafundisho yake yaliyojaa hekima. Amma na muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi chetu umeisha. Kwa mara nyingine tena tunatoa mkono wa kheri na baraka kwenu nyinyi nyote kwa mnasaba wa kukumbuka siku ya kuzaliwa Imam Mussa al Kadhim AS tukimuomba Allah aturuzuku shufaa ya mjukuu huyo wa Mtume wetu Muhamamd SAW. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.