Kipindi maalumu kwa mnasaba wa kukumbuka alipofariki dunia Mtume (saw) + Kasida
Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu, Muhammad (saw) aliaga dunia tarehe 28 Swafar mwaka wa 11 Hijiria katika mji mtakatifu wa Madina akiwa na umri wa miaka 63 na kuzikwa katika mji huohuo.
Kwa mujibu wa riwaya nyingi zilizopo, yapata miongo minne baada ya kifo cha Mtume (saw), yaani tarehe 28 Swafar mwaka 50 Hijiria, mjukuu wake mpendwa Imam, Hassan Mujtaba (as) naye aliuawa shahidi na vibaraka wa mtawala dhalimu, Muawiyya. Vifo hivyo vya Mtume na mjukuu wake viliiachia huzuni kubwa jamii ya Kiislamu. Tunatoa mkono wa pole kwa Waislamu wote duniani kwa mnasaba huu mchungu wa kukumbuka vifo vya watukufu hawa wawili.
Katika Aya zake, Qur'ani Tukufu inamtaja Mtume kama taa inayoangaza katika njia ya wokovu wa Mwenyezi Mungu na kwamba ni rehema kwa walimwengu na ruwaza njema kwa wale wanaotaka kuwa na maisha mema humu duniani na huko Akhera. Aya hizo pia zinakumbusha kwamba hata kama Mtume (saw) ni mjumbe wa Mwenyezi Mungu anayewasiliana moja kwa moja na nguvu za mbinguni, lakini wakati huohuo ni mwanadamu kama wanadamu wengine, ambaye anahitajia chakula, mavazi, ndoa, huwa mgonjwa na pia kuzeeka. Hivyo wakati wake ulipowadia, aliitikia wito wa Mwenyezi Mungu kama wanavyofanya wanadamu wengine wote. Katika Hija yake ya mwisho na alipokuwa akimpiga shetani mawe, Mtume Mtukufu (saw) aliwaambia Waislamu: 'Jifundisheni amali za Hija kutoka kwangu kwa sababu baada ya mwaka huu huenda nisifanikiwe tena kuja Hija na huenda hamtaniona tena nikiwa katika nafasi hii.' Mtume (saw) alikuwa mgonjwa katika siku za mwisho za maisha yake humu duniani. Akiwa katika hali hiyo ya kuumwa alienda msikitini na baada ya kuswali alisema: 'Enyi watu! Moto mkali wa fitina umewashwa na fitina kuenea kama yanavyoenea mawimbi ya usiku mkubwa. Mimi nitakutangulieni katika siku ya Ufufuo na nyinyi mtafika mbele yangu kwenye Hodhi ya Kauthar. Fahamuni kwamba nitakuulizeni kuhusu Thaqalain (Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Ahlu Beit wangu). Hivyo tazameni mtaamiliana vipi na viwili hivi baada yangu. Hii ni kwa sababu Mwenyezi Mungu Mrehemevu na anayejua mambo yote amenijulisha ya kwamba viwili hivi havitatengana hadi vitakaponifikia. Jueni kwamba nimekuachieni viwili hivi, hivyo msivitangulie msije mkasambaratika na kugawanyika wala msivipuuze mkaja kuhiliki.' Baada ya hapo Mtume (saw) akaanza safari ya kuelekea kwa Muumba wake kwa usumbufu.
Watu wakaanza kumuaga Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu huku macho yao yakiwa yamejaa machozi. Hata akiwa katika hali ya maumivu makubwa ya ugonjwa, Mtume aliwausia sana watu wa pembeni yake kuhusu umuhimu wa kushughulikia matatizo na mahitaji ya watu na kuzingatia haki zao. Kisha aliwaambia hadhirina: 'Niitieni ndugu na rafiki yangu.' Ummu Salama, mkewe Mtume (saw) akasema: 'Muiteni Ali kwa sababu Mtume hamkusudii mtu mwingine isipokuwa Ali.' Ali alipofika, Mtume alimuashiria amkaribie. Kisha alimkumbatia kwa muda mrefu huku akimnong'oneza na kumwambia siri zake hadi akazimia. Baada ya kuona hali hiyo wajukuu wa Mtume (saw) Hassan na Hussein (as) walilia sana na kuuangukia mwili wake. Imam Ali (as) alitaka kuwatoa juu ya mwili wa Mtume (saw) lakini akazinduka ghafla na kusema: 'Eeh Ali! Waache wawili hao nipate kunusa harufu yao nao wanuse harufu yangu, ili wanufaike nami na mimi ninufaike nao.'
Hapo Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu akaaga dunia. Aliaga dunia akiwa mikononi mwa Ali bin Abi Talib (as) ambaye aliwatangazia watu waliokuwa karibu kuhusu kifo cha mtukufu huyo (saw). Kifo cha Mtume (saw) kilikuwa kichungu na chenye huzini kubwa kwa serikali na umma wa Kiislamu. Katika kipindi kifupi, Mtume Mtukufu (saw) alifanikiwa kuanzisha mazingira mazuri ya upendo, udugu na urafiki kati ya watu na kuasisi serikali iliyoeneza uadilifu na uzingatiaji sheria katika jamii, ambapo kila mtu na hasa tabaka la watu wa kawaida walinufaika sana kutokana na hali hiyo.
Hatua alizozichukua Mtume Muhammad katika kipindi cha miaka 23 ya Utume wake, zinachukuliwa kuwa hatua na harakati muhimu zaidi za kihistoria kuwahi kuchukuliwa katika jamii ya mwanadamu. Alianzisha jamii mpya, kuunganisha Bara Arabu katika mfumo wa kisiasa na kijamii juu ya msingi wa Qur'ani na kujaza imani kwenye nyoyo na fikra za wafuasi wake. Wafuasi wake hao walieneza ujumbe huo katika pembe na maeneo ya mbali zaidi duniani. Kwa msingi huo tunaweza kusema kuwa taathira ya Mtume Muhammad (saw) katika historia ni kubwa zaidi kuliko taathira za watu wengine wote katika historia ya mwanadamu. Sifa muhimu ya ustaarabu ulioanzishwa na Mtume (saw) ni ya upole na huruma mkabala wa taasubi za kikabila na kidini zilizotawala katika zama hizo. Mtume (saw) alichangia na kuimarisha pakubwa elimu, taaluma na sanaa za mwanadamu kwa kuwasilisha njia za wastani na za kati kwa kati katika mienendo na miamala ya watu. Hatua za Mtume (saw) katika kuasisi jamii iliyostaarabika na iliyo na serikali kuu yenye taasisi na idara za kisiasa na kisheria zinazoendeshwa kwa msingi wa taratibu zilizo wazi, zilipelekea kubadilishwa mifumo ya jamii za kijahilia. Jambo hilo pia lilipelekea kuanzishwa ustaarabu halisi uliosimama juu ya misingi ya ubunifu na uvumbuzi kwa kadiri kwamba jamii za Kiislamu na zisizo za Kiislamu zingali zinanufaika na matunda ya kimaada na kimaanawi ya uvumbuzi huo hadi leo. Kuhusu ukweli huo, Will Durat, mwanahistoria na mwandishi mashuhuri wa Kimarekani anasema katika kitabu chake cha Historia ya Ustaarabu: "Muhammad aliyaunganisha makabila ya waabudu-masanamu na yaliyokuwa yametawanyika jangwani. Alianzisha dini nyepesi, ya kawaida, ya wazi na yenye nguvu kuliko dini za Uyahudi, Ukristo na za kale za Bara Arabu. Dini hiyo inayozingatia masuala ya kimaanawi imesimama juu ya msingi wa ushujaa wa kikabila ambapo katika kipindi cha kizazi kimoja ilipigana na kushinda vita 100 vya kijeshi na katika kipindi cha karne moja kuweza kuasisi ufalme mkubwa na mpana ambapo katika zama zetu hizi umeweza kuwa na nguvu kubwa ambayo inadhibiti nusu ya ulimwengu."
Pierre-Simon Laplace, mnajibu na mwanahesabati mashuhuri wa Ufaransa anasema: "Hata kama sisi hatuziamini dini za mbinguni, lakini dini ya Mtukufu Muhammad na mafundisho yake ni mifano miwili ya kijamii kwa ajili ya maisha ya wanadamu. Kwa msingi huo, tunakiri kwamba kudhihiri dini na sheria zake za hekima, ni jambo kubwa na lenye thamani, hivyo tunahitaji kukubali mafundisho ya Mtukufu Muhammad."
Hata kama Mtume Mtukufu (saw) hayuko tena pamoja nasi, lakini ni wazi kwamba ujumbe wake ni uleule ujumbe wa Tauhidi ambao ndio unaoangaza ulimwengu na kuufanya uvutie wanadamu. Huu ndio ujumbe wa kwanza wa Mitume wote wa Mwenyezi Mungu, kwa maana ya kutotogemea nguvu nyingine yoyote isipokuwa ya Mwenyezi Mungu na vilevile kutokubali aina yoyote ya dhulma na uonevu. Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 25 ya Surat al-Anbiyaa: Na hatukumtuma kabla yako Mtume yeyote ila tulimpa Wahyi ya kwamba hapana mungu isipokuwa Mimi. Basi niabuduni Mimi tu.
Mtume alipokabiliana na jamii ya kijahili, katili na isiyokuwa na huruma alitumia upendo, subira na sheria zilizo wazi kuirekebisha jamii hiyo. Leo pia ulimwengu unahitajia maadili na upendo ili kuunda jamii iliyojitenga na vitendo vya utumiaji mabavu na ukiukaji mipaka. Jambo hilo litawezekana tu kwa kunufaika na mafundisho ya Mtume Mtukufu (saw), Mtume ambaye uwepo wake umejaa rehema, upendo, subira, wema na msamaha na ni kutokana na akhlaki yake hiyo njema ndipo akafanikiwa kupenya na kuzivutia nyoyo za mamilioni ya watu ulimwenguni.
Kwa mara nyingine tena tunatoa mkono wa pole kwa Waislamu wote duniani kwa mnasaba huu mchungu wa kukumbuka kifo cha Mtume Mtukufu (saw) na mjukuu wake mwema Imam Hassan (as).