Jan 02, 2021 08:59 UTC
  • Katika Maktaba ya Qassim Suleimani (mwaka mmoja tangu kuuawa  kwake shahidi)

Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo.

 

Karibuni kutegea sikio kipindi hiki maalumu kinachokujieni kwa mnasaba wa kukumbuka kutimia mwaka mmoja tangu alipouawa kidhulma Luteni Jenerali Qassim Suleimani ambaye jina lake ni mashuhuri mno katika ulimwengu wa Kiislamu kutokana na kusimama kidete dhidi ya makundi ya kigaidi. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

 

Luteni Jenerali Qassem Suleimani, Kamanda wa zamani wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, aliuawa shahidi alfajiri ya kuamkia Ijumaa ya tarehe 3 Januari 2020 pamoja na Abu Mahdi al Muhandis, aliyekuwa Naibu Mkuu wa Al-Hashdu-Sha'abi pamoja na wenzao wengine wanane katika shambulio la anga lililofanywa na jeshi vamizi na la kigaidi la Marekani karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad nchini Iraq. Shahidi Qassim Suleimani alizaliwa tarehe 20 Isfand 1335 Hijria Shamsia katika mji wa Kerman.  Wakati wa utoto na kuinukia kwake aliupitisha akiwa pamoja na baba yake. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuundwa Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH alijiunga na kikosi hicho.

Wakati wa kuanza vita vya kulazimishwa vya miaka minane vya Iraq dhidi ya Iran, Qassim Suleimani akawa akitoa mafunzo kwa brigedi za kijeshi mjini Kerman na kuzituma katika medani ya vita. Mwaka 1360 Qassim Suleimani akateuliwa kuwa kamanda wa kikosi cha 41 cha Tharallah. Kikosi hicho chini ya uongozi wa Qassim Suleimani kilitekeleza operesheni nyingi wakati wa vita vya kujihami kutakatifu kama Walfajr 8, Karbala 4, Karbala 5 na kadhalika. Mwaka 1389 Qassim Suleimani aliteuliwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH. Baada ya kuibuka kundi la kigaidi la Daesh nchini Iraq na Syria, Luteni Jenerali Qassim Suleimani alihudhuria katika medani za vita za mataifa hayo akiitikia wito wa viongozi wa nchi hizo na kuwa na nafasi kubwa katika kuliangamiza kundi hilo la kigaidi. 

Luteni Jenerali Qassem Suleimani, na Abu Mahdi al Muhandis, aliyekuwa Naibu Mkuu wa Al-Hashdu-Sha'abi

 

Shahidi Qassim Suleimani anatambulika na wananchi wa mataifa ya Kiislamu na yasiyo ya Kiislamu katika eneo la Asia Magharibi kama kamanda shujaa wa Kiislamu. Wananchi wa asia Magharibi hususan wa Iraq bila shaka ni wadaiwa wa shahidi huyu kutokana na kuwa na mchango mkubwa katika kulinda roho, mali, usalama na utulivu wao na wakati alipouawa alikuwa ameelekea Baghdad kwa mwaliko rasmi wa serikali ya nchi hiyo.

 

Umepita mwaka mmoja sasa tangu lilipotokea tukio hilo chungu ambalo lilitikisha nyoyo za wapenda haki na wapigania uhuru duniani, ambapo kumbukumbu kubwa ya Haj Qassim ambayo ni chimbuko la miongozo ya shahidi huyu katu haiwezi kusahaulika. Sura yake iliyojaa nuru na haiba yake yenye utulivu usio na kifani ni mambo ambayo watu wote hawawezi kuyasahau. Familia za mashahidi katu haziwezi kusahau mkono wa shahidi Qassim Suleimani uliokuwa ukigusa na kupangusha pangusa vichwa vya watoto wa mashahidi mara alipokuwa akizitembelea familia hizo, mtu ambaye daima alikuwa akihisi kuwa na majukumu mbele ya familia hizo za mashahidi ambapo alikuwa akiwaunga mkono kama baba wa familia mwenye huruma na huba kubwa kwa familia yake. Kwa hakika shahidi Qassim Suleimani ni misadqi na mfano wa wazi wa Aya ya Qurani Tukufu isemayo: Wana nguvu (na wakali) mbele ya makafiri, na wanahurumiana wao kwa wao. Hilo tunalishuhudia wazi ambapo maadui walikuwa wakitetemeka kwa kusikia jina lake, huku nyoyo za watoto wa mashahidi zikipata utulivu kwa kutajwa jina lake.

 

Tukio la Januari 3 mwaka jana ghafla moja lilimdhihirisha mtu na shakhsia ambaye mpaka wakati huo hakuna mtu aliyekuwa akifahamu ni kwa kiwango ana nafasi katika nyoyo za watu.

Uamuzi wa kumuua shahidi Qassim Suleimani lilikuwa kosa la kistratejia lililofanywa na Marekani ambapo kwa mauaji haya ya kidhulma, shahidi huyu amegeuka na kuwa shujaa anayetoa ilhamu kwa wote wanaoipenda Iran na wanaowachukia mabeberu na waistikbari. Tukio hilo lilitia ari na roho mpya katika mwili wa makundi ya muqawama na mapambano kieneo, na kuongeza hisia ya mfungamano wa kitaifa katika jamii ya Wairani. Na hii ndio sifa maalumu ya shahidi na athari ya kuuawa shahidi ambayo madola ya kibeberu hayawezi kuidiriki.

Hakuna maktaba ya kimaada ambayo inaweza kuwalingania wafuasi wake suala la kujitolea kwani kwao wao maslahi ya mtu binafsi ndio kigezo. Katika ustaarabu wa Kiislamu, shahidi ni mtu ambaye ameuawa katika njia ya haki na ukweli na ni kama ilivyo kwa mshumaa ambao huungua ili kupitia nuru yake wengine wakae na kupata mwanga na utulivu. Kwa mtazamo huu kuuawa shahidi ni jambo tukufu kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu. Ni kwa msingi huo, ndio maana mwenye kutaka shahada hufanya hivyo kwa ajili ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu na hivyo kukwea daraja.

Shahidi Qassim Suleimani amefanya mambo ambayo hata maadui zake wamelazimika kufungua   vinywa na kusifia ushujaa, upeo wake mkubwa wa maarifa pamoja na tadibiri yake iwe ni katika kipindi cha kujihami kutakatifu yaani wakati wa vita vya miaka minane vya kulazishwa Iran vilivyoanzishwa na utawala wa wakati huo wa Iraq chini ya uongozi wa dikteta Saddam au katika kipindi hiki cha migogoro ya kupandikizwa katika eneo hili la Asia Magharibi.

 

Wakati wa vita, Luteni Jenerali Qassim Suleimani alikuwa mstari wa mbele kuandaa mipango bora kabisa ya kumshambulia adui na yeye mwenyewe alikuwa mstari wa mbele kuitekeleza akiwa bega kwa bega na wanamuqawama wengine.

 

Shahidi Qassim Suleimani alikuwa kamanda ambaye hakujua maana ya kuchoka ni nini, ambapo akiwa na upeo wa juu wa ufahamu aliweza kuvifanya vikosi alivyoviongoza kutoa pigo kwa adui.

Mafanikio makubwa ya kikosi cha 14 cha Tharallah cha Kerman wakati wa vita vya miaka minane vya kujihami kutakatifu yalipatikana chini ya uongozi wa wake. Wakati wa operesheni dhidi ya maadui Qassim Suleimani alikuwa akiwaambia wapiganaji waliokuwa chini ya uongozi wake, 'njooni' na sio 'nendeni', kwa maana kwamba, yeye mwenyewe alikuwa mstari wa mbele katika vita na operesheni dhidi ya maadui tofauti na walivyo makamanda wengine ambao hutoa tu amri ya kufanywa mashambulio.

Moja ya sifa muhimu za shahidi Qassim Suleimani akiwa kamanda na kiongozi wa wapiganaji ni kwamba, alikuwa yeye mwenyewe akitekeleze operesheni ya kutambua maeneo ya adui na kisha kuongoza operesheni za mashambulio. Sifa nyingine muhimu ya Luteni Jenerali Qassim Suleimani ni uwiano na wastani wa mambo katika miamala na vitendo vyake. Katika uga wa masuala ya kisiasa na kijamii alikuwa na misimamo na miamala ya wastani na ndio maana hakuna mrengo wowote wa kisiasa unaoweza kudai kwamba, Qassim Suleimani alikuwa miongoni mwao.

 

Ikhlasi ni sifa nyingine muhimu aliyojipamba nayo mwanajihadi huyu, sifa ambayo inatajwa katika mafundisho ya Kiislamu kuwa, moja ya tabia muhimu za kimaadili ambayo humkurubisha mja kwa Mola wake mlezi. Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, siri ya kupendwa shahidi Qassim Suleimani inatokana na ikhalsi yake na kutokuwa na tabia ya kufanya mambo kwa ria na kujionyesha. Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mpainduzi ya Kiislamu amemsifia na kumtaja Haj Qassim Suleimani kuwa mtu aliyejipanga kwa ikhlasi.

Kwa hakika shahidi Qassim Suleimani ameasisi na kuanzisha maktaba ambayo misingi yake ni kujenga na kulea wanadamu, utu, udugu, ushujaa, uwezo, jihadi na hima na idili ya usiku na mchana, huba, huruma, kuishi maisha ya kawaida yasiyo na fakhari na majivuno, unyenyekevu, kuwa mtu wa vitendo na siyo maneno matupu na kadhalika, mambo ambayo aliyaonyesha kivitendo na katika mwenendo wake wakati wa uhai wake.  Sifa hizi ni maalumu kwa watu wasio na madai matupu kama Luteni Jenerali Qassim Suleimani.

Shahidi Qassim Suleimani akiwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

 

Wimbi alilolianzisha shahidi Qassim Suleimani katika Umma wa Kiislamu, linabainisha kwamba, kila tone moja la damu ya shahidi litabadilika na kuwa, mamia na maelfu ya matone bali bahari ya damu ya mashahidi ambayo itatiwa katika mwili wa jamii na hivyo kuifanya kuwa, hai na siku zote harakati yake iwe amilifu na hai.

Wapenzi wasikilizaji na hadi hapa ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki maalumu kilichokujieni kwa mnasaba wa kukumbuka mwaka mmoja tangu alipouawa shahidi Luteni Jenerali Qassim Suleimani. Ni matumaini yangu mmenufaika na yale niliyokuandalieni. Ahsanteni kwa kunitegea sikio na kwaherini.

 

Tags