Fatima Maasuma, Kigezo cha Elimu na Utakasifu
https://parstoday.ir/sw/radio/uncategorised-i90000-fatima_maasuma_kigezo_cha_elimu_na_utakasifu
Tarehe 10 Rabiuthani ulimwengu wa Kiislamu unakuwa katika makiwa na msiba wa kuondokewa na mwanamke adhimu ambaye katika siku za mwishoni mwa umri wake, aliipamba ardhi ya Iran yaani mji wa Qum baada ya kuelekea katika eneo hilo na kufariki dunia katika mji huo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 03, 2022 03:23 UTC
  • Fatima Maasuma, Kigezo cha Elimu na Utakasifu

Tarehe 10 Rabiuthani ulimwengu wa Kiislamu unakuwa katika makiwa na msiba wa kuondokewa na mwanamke adhimu ambaye katika siku za mwishoni mwa umri wake, aliipamba ardhi ya Iran yaani mji wa Qum baada ya kuelekea katika eneo hilo na kufariki dunia katika mji huo.

Kwa mnasaba huu mchungu tunatoa mkono wa pole kwa Waislamu wote hususan wapenzi na wafuasi wa Watu wa Nyumba ya Mtume wetu Muhammad (saw) na katika kipindi hiki tunatupia jicho angalau kwa muhtasari sira na mwenendo wa kimaadili na kijamii wa mwanamke huyu adhimu. 

Bibi Fatima Maasuma alizaliwa katika mji mtakatifu wa babu yake, yaani Madinatul Munawwara katika mwezi Dhul Qaada mwaka 173 Hijria na kufariki dunia tarehe 10 Rabiulthani 201 katika mji wa Qum. Alizaliwa na kukulia katika familia ambayo ni mchemchemi ya elimu, maarifa, taqwa, subira na maadili mema. Baba yake mtukufu, yaani Imam Mussa bin Ja'far (as) ni Imam wa Saba katika kizazi cha Mtume (saw). Mama yake alikuwa Najma na alimzaa baada ya Imam Ridha (as) na kumpa jina la Twahira. Kati ya watoto wote wa Imam Mussa al Kadhim, Bibi Fatima Maasuma ndiye aliyekuwa na makamu na nafasi ya juu zaidi kielimu na kimaadili baada ya kaka yake yaani Imam Ali bin Mussa al Ridha (as). Ukweli huu unaonekana wazi zaidi kutokana na lakabu, majina na sifa alizopewa bibi huyu adhimu na maimamu watoharifu katika kizazi cha Mtume (saw). Miongoni mwa lakabu za bibi huyu mtukufu ni ile ya Karimatu Ahlil Bait ambayo inaakisi sifa makhsusi za kiroho na ilikuwa makhsusi kwake peke yake kati ya wanawake wa kizazi hicho kitoharifu. Lakabu nyingine za Bibi Fatima Maasuma ni Swiddiqah kwa maana ya kweli msana na Muhadditha inayomaanisha mpokezi na msimuliaji wa hadithi za Mtume (saw) na Ahlibaiti zake. Katika kipindi cha Uimamu wa kaka yake, Ali bin Mussa Ridhaa (as), Bibi Fatima al Maasuma alikuwa akinukuu na kusimulia hadithi na kuuelimisha umma. Alinukuu hadithi nyingi kutoka kwa baba na mababu zake ambazo zinakubaliwa na zimepokewa na maulamaa wa Shia na Suni. Miongoni mwa hadithi hizo ni ile iliyopokewa kwa sanadi iliyo madhubuti inayosema: Bibi Fatimatu Zahra (as) amenukuu kutoka kwa baba yake, Mtume wa Mwenyezi Mungu kwamba amesema: "Mtu anayefariki dunia hali ya kuwa anawapenda Aali Muhammad hufa akiwa shahidi, anayefariki dunia hali ya kuwa anawapenda Aali Muhammad hufa hali ya kuwa amesamehewa madhambi yake .. hadi pale mtume (saw) anaposema: Anayefariki dunia hali ya kuwa anawaudhi Aali Muhammad hufa akiwa kafiri na kwamba hatanusa harufu ya Pepo". Hadithi hii imepokewa na maulamaa wakubwa wa Kishia na Kusuni kama al Fakhru Razi katika kitabu cha Attafsirul Kabiir, Imam Zamakhshari katika tafsiri yake ya Qur'ani ya Al Kash-Shaf na Qurtubi katika tafsiri yake ya Qur'ani. (کشاف 4/220، تفسیر فخر رازی 27/165 ، تفسیر قرطبی 8/5843 ، نمونه 20/ 414 )

Bibi Maasuma alikuwa kilele cha utakasifu wa maadili na mwenendo mwema. Sababu ya kuwa kileleni na utukufu wa Bibi huyu mwema ni maadili aali kama vile kujipamba kwa sifa za subira, busara, hikima na istiqama. Wanahistoria wameandika kuwa, siku moja kundi moja la wapenzi na wafuasi wa Watu wa Nyumba ya Mtume wetu mtukufu Muhammad (saw) walikwenda mjini Madina kwa ajili ya kupata majibu ya maswali waliyokuwa nayo kutoka kwa Imam Mussa al Kadhim (as). Walipofika nyumbani kwa mtukufu huyo waliambiwa kwamba, ameenda safarini. Watu hao walilazimika kuandika maswali yao na kuyakabidhi kwa familia ya Imam ili waweze kupata majibu yake watakapokuja tena mjini Madina. Siku kadhaa baadaye watu wa kundi hilo walikwenda nyumbani kwa Imam Kadhim kwa ajili ya kuaga familia yake lakini walikuta kwamba, Bibi Masuma alikuwa tayari amejibu maswali yao yote ya kielimu na kifiqhi kwa maandishi. Walifurahishwa na jambo hilo na walipokuwa njiani wakirejea makwao walikutana na Imam Kadhim (as) na kumhadithia yaliyotukia. Imam alisoma majibu ya Bibi Fatima Maasuma na kuyapasisha yote na kisha akasema: "Baba yake awe fidia na mhanga wake".

Japokuwa cheo cha i'sma, umaasumu na kutofanya dhambi licha ya kuweza kufanya hicho ni cheo adhimu na makhsusi kwa Manabii wakubwa na wasii wao, lakini wapo watu wengine katika historia ambao walifikia daraja ya juu ya taqwa na kumcha Mwenyezi Mungu na kufikia daraja ya isma na umaasumu kwa ikhasi na ukatasifu wa nafsi zao. Jina la Bibi Maasuma ni Fatima al Kubra lakini mwanamke huyu alifikia nafasi ya juu ya kiroho na kutakasa nafsi kiasi kwamba, Imam Ridha (as) alimpa lakabu ya Maasuma kwa maana ya maasumu ya mtu asiyetenda dhambi. 

Haram ya Bibi Fatima Maasuma (as) katika mji wa Qum

Sira na mwenendo wa kisiasa na kijamii wa mtukufu huyo inaonekana waziwasi kwa kutadabari katika safari iliyofanywa na Bibi Maasuma kwenda kumtembelea Imam Ridha (as) ambaye wakati huo aliwa Khurasan kwa amri ya mtawala wa wakati huo wa kizazi cha Banii Abbas. Wakati khalifa wa utawala wa Banii Abbas, Maamun alipomlazimisha Imam Ridha kuhamia Marw iliyokuwa kaskazini mwa Iran ya zama hizo kwa shabaha ya kutuliza malalamiko ya wananchi na kuwahadaa kwamba Imam alikuwa mrithi wa kiti cha utawala na ukhalifa, Bibi Maasuma akiwa pamoja na kaka zake kadhaa, alielekea katika eneo hilo kwa shabaha ya kufichua uso wa kinafiki wa Banii Abbas na kuuzindua Umma wa Kiislamu kuhusu nafasi ya Uimamu na utawala wa kizazi maasumu cha Mtume (saw). Kuondoka kwa Bibi Maasuma katika mji wa Madina na kukabiliana kwake na maafisa wa utawala wa Kiabbasi alipokuwa njiani, kuliwafanya watu waelewe kwamba, kauli ya Khalifa Maamun kwamba Imam Ridha (as) alikuwa mrithi wa kiti cha ukhalifa baadaye yake ilikuwa hadaa na ujanja mtupu. Hususan pale msafara wa Bibi Maasuma ulipofika eneo la Saweh na kuhujumiwa na maafisa wa mtawala huyo wa Kiabbasi. Maafisa wa utawala huo waliuzuia msafara huo kuendelea na safari ya kuelekea Marw na kuwaua shahidi baadhi ya watu waliokuwa pamoja na Bibi Maasuma wakiwemo kaka na ndugu zake kadhaa. Tukio hilo lilikuwa chungu na zito sana kwa mtukufu huyo kiasi kwamba, alipatwa na maradhi shadidi. Baada ya kutambua kuwa hawezi tena kuelekea Marw, Bibi Maasuma aliwataka watu wa karibu yake wampeleke katika eneo la Qum. Alisema nipelekeni Qum kwa sababu nimemsikia baba yangu akisema: Mji wa Qum ni kituo cha wapenzi wa Ahlibaiti wa Mtume". 

Haram ya Bibi Fatima Maasuma (as) katika mji wa Qum

Baada ya habari hiyo kuwafikia watu wa Qum, watu wengi sana walijitokeza kwenda kumlaki Bibi Maasuma. Miongoni mwao alikuwa Mussa bin Khazraj kutoka kizazi cha Saad ambaye aliharakia kwenda kuulaki msafara wa mtukufu huyo. Alishika hatamu ya ngamia ya Bibi Fatima Maasuma na kuongoza msafara huo hadi Qum. Mussa bin Khazraj Alikwenda moja kwa moja nyumbani kwake na kupata fahari ya kuwa mwenyeji wa mtukufu huyo. Hata hivyo Bibi Maasuma ambaye baada ya kuuawa shahidi kaka zake waliokuwa pamoja naye safarini alikuwa amepatwa na maradhi makali, alifariki dunia siku 16 au 17 baaye na kurejesha roho kwa Mola Muumba. Inna Lillah, wainna ilayhi rajiuun.

Haram ya Bibi Fatima Maasuma (as) katika mji wa Qum

Katika siku kadhaa za kuweko kwake katika mji wa Qum, Bibi Fatima alikuwa na eneo maalumu la ibada na kunong'ona na Mola wake ambalo lingalipo hadi hii leo katika madrasa inayojulikana kwa jina la Settieh. 

Baitu Nur