Mtazamo Mpya wa Wanawake Kuhusu Vazi la Hijabu
https://parstoday.ir/sw/radio/uncategorised-i90522-mtazamo_mpya_wa_wanawake_kuhusu_vazi_la_hijabu
Vazi la staha la mwanamke wa Kiislamu, hijabu, ni moja na maudhui zinazozusha mijadala na mivutano mingi katika zama hizi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 14, 2022 06:55 UTC
  • Mtazamo Mpya wa Wanawake Kuhusu Vazi la Hijabu

Vazi la staha la mwanamke wa Kiislamu, hijabu, ni moja na maudhui zinazozusha mijadala na mivutano mingi katika zama hizi.

Misimamo ya nchi za Magharibi ya kutaka kuwalazimisha na kuwatwisha watu utamaduni na mtindo wa maisha wa Kimagharibi umewafanya wanawake wanaovaa vazi la hijabu wakabiliwe na matatizo mengi. Hata hivyo katika makala hii hatuna nia ya kuzungumzia matatizo na vikwazo vinavyowekwa na nchi za Magharibi dhidi ya vazi la hijabu, bali tutatazama maudhui ya hijabu kwa mtazamo tofauti. Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali za vyombo vya mawasiliano ya umma, wanawake wa Kiislamu katika nchi za Ulaya ambao wengi wao ni kutoka tabaka la vijana wameweza kulitangaza vazi la hijabu kama nembo na utambulisho wao wa Kiislamu kwa kujichagulia suruali, gauni refu na mtandio wa kujifunika kichwani. Wanawake hao wa Kiislamu wamefanikiwa kwa aina fulani kulitambulisha vazi lao kama modeli na mtindo unaopendelewa na wanawake wengine katika jamii za Magharibi. Ripoti hizo zinasema, vazi la hijabu limewavutia wanawake wengi wanaoshabikia mavazi maridadi na ya heshima katika mazingira ya kazi, sherehe na mahafali. Kwa mfano shirika la habai la Reuters liliwahi kutayarisha ripoti ndefu juu ya sababu kuu zinazowafanya wanawake wa Ulaya wavutiwe na vazi la hijabu la wanawake wa Kiislamu na kuashiria nukta hii kwamba, mbali na umaridadi na kumpa mtu hadhi na heshima, vazi la hijabu pia linasifika kwa kumpa mwanamke sura safi, umaasumu na utakasifu wa roho na tabia.

Si jambo la kushangaza pia kusikia katika ripoti za vyombo vya habari kwamba baadhi ya viongozi wa serikali za nchi za Ulaya wameingiwa na wasiwasi kutokana na kuenea kwa vazi la hijabu na kuchukuliwa kama mtindo unaowavutia wanawake katika baadhi ya nchi hizo. Wakati huo huo kukubalika kwa vazi la hijabu huko Ulaya kunaonyesha kwa aina fulani uhusiano wa karibu mno wa hijabu na fitra na maumbile safi ya mwanaadamu mwanamke. Kwani hamu ya kusitiri mwili ni jambo liliko ndani ya dhati ya mwanaadamu. Kimsingi hijabu na “ifaf” kwa maana kujizuia mambo machafu, vinahesabiwa kuwa thamani muhimu katika jamii ya mwanaadamu hususan jamii za Kiislamu, na daima mambo hayo mawili yamekuwa yakiambatana. Hijabu husitiri dhahiri na mwili wa mtu, na mara nyingi umbo lake huathiriwa na itikadi za kidini za mvaaji na pia ada na desturi za jamii yake. Kwa msingi huo vazi linalositiri na kulinda mwili wa mwanamke wa Kiislamu mbele ya macho ya watu waovu huitwa hijabu. Lakini "ifaf" ni ile hali inayopatikana ndani ya nafsi ya mwanamke aliyevaa hijabu na kumpa uwezo wa kukabiliana na vishawishi na matamanio ya kinafsi. Qur'ani Tukufu inaitaja "ifaf" kuwa ni kujilinda na kujiweka safi kiroho, na kwa hakika ni aina fulani ya hijabu ya ndani ya nafsi. Kwa msingi huo vazi la hijabu hukamilika na kupata maana yake halisi pale linapoambatana na "ifaf", kwa maana ya ile hali ya usafi na kujizuia na maovu, au kwa maana nyingine, hijabu ya ndani ya nafsi na roho ya mwanaadamu. Kwa maana nyingine tunaweza kusema kuwa, hijabu ya kidhahiri ni vazi linalositiri mwili wa mwanamke, kuakisi na kuonyesha ifaf na na usafi wa kiroho wa mwanamke Muislamu.

Katika mtazamo wa Kiislamu vazi la hijabu huwa na taathira kubwa katika medani nyingi za kisiasa, kiutamaduni na kijamii. Hijabu huimarisha akhlaki na maadili mema ya mtu binafasi na kulinda nishati ya mwanamke na ujana wake visitumike ovyo na katika mambo yasiyokuwa na faida yoyote. Kwa hakika vazi la hijabu si mpaka na kizuizi kwa mwanamke, bali ni kinga na ulinzi kwake yeye na jamii nzima. Hii ni kutokana na kwamba, katika Uislamu mwanamke anatambuliwa kuwa ndiye mlezi wa familia na jamii.

Vazi la mwanamke katika Uislamu lina mipaka na taratibu maalumu ingawa watu wa kila jamii wanaweza kujichagulia aina ya vazi lao wenyewe kwa kutilia maanani utamaduni, ada na desturi zao lakini katika mipaka ya sheria za dini ya Mwenyezi Mungu. Vazi la hijabu ni chombo na wasila wa kuratibu mahusiano sahihi kati ya wanawake na wanaume katika jamii. Vazi zuri, la heshima na staha huondoa mazingira ya hisia za ngono na matamanio ya kinafsi na kutayarisha uwanja wa utendaji kazi mzuri kati ya jinsia mbili. Kwa maana kwamba, msingi wa vazi la hijabu ya Kiislamu ni kuimarisha na kukuza vipawa vya kibinadamu vya mwanamume na mwanamke. Kwani Mwenyezi Mungu Muumba wa walimwengu anataka mazingira ya jamii kuwa safi kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kijamii na si kutayarisha mazingira ya kumtazama mwanamke kama bidhaa inayouzwa na kununuliwa. Kwa mfano tu, Mwanamke anayevaa vazi la hijabu wa Iran anasoma kwa urahisi na kwa usalama katika vyuo vikuu na anafanya kazi maofisini. Wanawake wa Iran wamepata mafanikio na ustawi bega kwa bega na wanaume, katika mazingira ya kisayansi na michezo, katika soko la uchumi na ajira, katika biashara na sekta ya madini, na vazi lao la hijabu halijawahi kuzuia mafanikio yao makubwa. Pamoja na hayo, katika propaganda zao za vyombo vya habari, nchi za Magharibi zinajaribu kuutambulisha Uislamu na Jamhuri ya Kiislamu kama mfumo unaopinga haki za wanawake. Ijapokuwa waandishi na maripota wa habari wa Kimagharibi wanalitaja vazi la hijabu kuwa ni sababu ya kudumaa na kubakia nyuma kwa wanawake, lakini wameshindwa kutoa mtazamo na maoni sahihi ya kuhalalisha ushiriki wa wanawake wa Kiislamu katika nyanja mbalimbali ambao, licha ya kuwa na vazi hilo, wamekuwa na mafanikio na ustawi wa pande zote.

Kwa mtazamo wa Uislamu, mwanamke sawa kabisa na alivyo mwanaume, ni kiumbe mwenye thamani kubwa za kibinadamu ambaye ana nafasi na majukumu mazito ya kulea kizazi na kustawisha jamii. Kwa msingi huo kuna udharura wa kulinda heshima na hadhi yake.

Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran anasema kuhusu kaulimbiu ya uwongo ya "uhuru wa wanawake" kwamba: "Jambo lililoenea hii leo duniani kwa anwani ya "uhuru wa mwanamke" na kupigiwa debe katika tamaduni mbovu za Kimagharibi, msingi wake ni kumuweka uchi mwanawake mbele ya wanaume ili kuwastarehesha. Ni kuhakikisha kwamba wanaume wanapata starehe kutoka kwa wanawake hao wanaofanywa wenzo wa kushibisha matakwa ya kingono ya wanaume. Je, huu ndio uhuru wa mwanamke? Wale wanaodai kuwa wanatetea haki za binadamu katika ulimwengu wa kijahilia, ulioghafilika na kupotea wa ustaarabu wa Magharibi, kwa hakika ni madhalimu wa wanawake. Mpeni mwanamke hadhi yake ya juu ili mupate kujua ukamilifu, haki na uhuru wake.

Vazi la staha la mwanamke wa Kkiislamu

Kwa hakika hatua ya wanawake wa Magharibi ya kulipokea vazi la hijabu kama vazi la heshima na staha inatoa matumaini na bishara njema ya kurejea tena jamii za Magharibi, hususan tabaka la akina mama, katika masuala ya kiroho na kimaadili.

Naam wapenzi wasikilizaji, licha ya propaganda zote mbaya zinazoendeshwa na nchi za Magharibi dhidi ya vazi la staha la hijabu ya Kiislamu lakini bado vazi hilo linawavutia wengi kwa kiasi cha kushangaza. Suala hilo bila shaka linaonyesha kwamba, mafundisho ya Kiislamu yaliyoteremshwa kutoka kwa Mola wa ulimwengu na mwanadamu yanaoana na kwenda sambamba na maumbile safi na asili ya mwanaadamu.