Mashindano ya makampuni ya teknolojia kwa ajili ya kuwajasisi wateja wao
Mitandao ya kijamii, ambayo imeteka akili na nyoyo za watumiaji, ni vyombo vya habari vinavyoathiri miundo ya kijamii, kitamaduni, kisiasa na kiuchumi ya jamii mbalimbali.
Mitandao hiyo ya kijamii ni matunda ya mchakato wa maendeleo na ustawi wa intaneti na teknolojia zake katika kipindi cha miongo michache iliyopita. Mitandao hii ya kijamii iliingia katika uwanja wa teknolojia tangu 1991, na katika miaka kumi ya kwanza ilikuwa na watumiaji wachache. Kuanzia mwaka 2000 na kuendelea, kulijitokeza kizazi kipya cha mitandao ya kijamii ambacho kiliwavutia watumiaji wengi wa mtandao. Kwa upande mmoja, mitandao hii imezidisha maingiliano na mawasiliano kati ya watu, na kwa upande mwingine, imeandamana na uharibifu mwingi wa kijamii na kiusalama. Sasa baadhi ya mitandao hiyo inatumiwa na mashirika ya ujasusi duniani kujasisi na kudukua taarifa za watumiaji.

Katika miaka ya hivi karibuni, ubora wa juu sana wa mitandao ya kijamii katika kupeana taarifa kwa haraka na bila mipaka, umepelekea kukua na kuongezeka kwa watumiaji kwenye mitandao hii ya kijamii. Kupeana taarifa, kupakua na kupakia nyaraka, picha, miziki, video pamoja na programu na kutoa huduma katika mitandao ni miongoni mwa matumizi ya haraka ya mitandao ya kijamii. Watumiaji wa mitandao hiyo hupeana maelezo, picha, programu, n.k. kwenye mitandao ya kijamii, na makampuni ya utangazaji hupata pesa kwa kutangaza na kuuza bidhaa zao kupitia mitandao hiyo. Katika mitandao ya kijamii, watumiaji wote wanaonekana kuwa katika kiwango sawa, na kwa kutumia uwezo wa chombo hiki, wanaweza kupata mawasiliano ya kina ya binadamu wenzao bila ya kujali mipaka ya kisiasa na kijiografia.
Hata hivyo, wachambuzi wengi wanaamini kwamba, ingawa mitandao ya kijamii ni chombo cha mawasiliano kati ya watu wa kijiji kilichopewa jina la dunia, lakini wakati huo huo ni hatari kubwa kwa wakazi wa kijiji hichho. Nyenzo nyingi za mitandao hiyo ya kijamii, kama vile Facebook, Twitter, YouTube, Google Plus, n.k., vimeunda fursa za kipekee na nzuri kwa mashirika ya ujasusi ya dunia kukusanya taarifa, kueneza ushawishi, kuelekeza na kadhalika kupitia vyombo hivyo. Nyenzo hizi zina ushawishi na zinatumiwa kwa mahesabu maalumu, na tunaweza kusema kuwa mitandao hiyo ya kijamii ni matunda ya mipango na programu makini za mashirika ya ujasusi.

Facebook ndio mtandao maarufu wa kijamii wenye idadi kubwa ya watu wa intaneti ambao uliasisiwa Februari 2004. Kulingana na kampuni ya Facebook, madhumuni ya kuundwa mtandao huo wa kijamii ni kuifungua na kuiunganisha pamoja dunia. Taarifa ya hivi karibu ya kampuni inayomiliki Facebook (Meta) ni kwamba watu hutumia mtandao huo wa kijamii kuwasiliana na marafiki na familia na vilevile kugundua kupata habari za kila kitu kinachotokea duniani. Swali linalojitokeza ni kwamba, je, huo ndio ukweli wa mambo kuhusiana na Facebook?
Hii leo, ni jambo lisilopingika kwamba tovuti nyingi zinahudumia makampuni ya habari na ya upepelelezi. Ingawa uanachama katika tovuti na mitandao hiyo ni bure, lakini ukweli ni kwamba hakuna kitu ambacho ni bure katika mitandao hiyo ya kijamii; kwani mkabala wa matumizi yasiyo na malipo na ya bure ya huduma za kielektroniki, tovuti na mitandao ya kijamii; watumiaji hutoa na kuanika wazi na kwa urahisi siri nyingi za maisha yao. Mwanzilishi wa WikiLeaks, Julian Assange anasema: "Facebook ndio chombo kibaya zaidi cha ujasusi kilichowahi kuundwa hadi hivi sasa. Mtu yeyote anayeongeza majina na wasifu wa marafiki zake kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook anapaswa kujua kwamba, anahudumia mashirika ya kijasusi ya Marekani bila malipo.." Mwasisi wa WikiLeaks anasema, Facebook ni hazina kubwa ya majina na rekodi za watu, ambayo watumiaji huitoa na kuikabidhi kwa hiari na bila kujua kwa mtandao huo wa kijamii, lakini chombo hiki kinatumiwa na mashirika ya usalama na ya kijasusi ya Marekani. Assange ameongeza kuwa, uwezo wa mashirika ya ujasusi ya Marekani wa kupata kirahisi taarifa na rekodi zinazohifadhiwa kwenye Facebook umekifanya chombo hicho na mfano wake kuwa zana hatari sana dhidi ya mataifa mbalimbali ya dunia.

Katika ripoti iliyochapishwa Agosti 27, 2013, Facebook ilitangaza kuwa imetoa taarifa za watumiaji wake kwa serikali za nchi mbalimbali kutokana na maombi ya serikali hizo. Ripoti hiyo imeeleza kuwa, katika nusu ya kwanza ya mwaka 2013, serikali za nchi mbalimbali ziliomba kupata taarifa za watumiaji zaidi ya 38,000 wa mtandao huo wa kijamii, na asilimia 80 ya maombi hayo yalitimizwa. Zaidi ya nchi 74 za dunia ziliwasilisha maombi hayo kwa Facebook, na zaidi ya nusu ya maombi hayo yalitolewa na serikali ya Marekani. Facebook pia ilitangaza katika makala yaliyochapishwa Desemba 2013 kwamba ina uwezo wa kuhifadhi na kujilimbikizia rasimu za maandiko ya watumiaji wake wakati yanataipiwa ambayo hatimaye watumiaji huamua kutoyachapisha. Ripoti hiyo imeonesha kuwa Facebook inapata hata taarifa za mawazo ya watu kabla ya kuchapishwa na kusambazwa kwa watu wengine kupitia chombo hicho.

WhatsApp pia ni programu nyingine ya kutuma ujumbe wa papo hapo kwa kutumia rununu yaani simu ya kiganjani au ngamizi yaani kompyuta. Programu hiyo iliundwa na WhatsApp na hatimaye ilinunuliwa na kampuni ya Meta. Mapema 2021 watumiaji wa programu hii, ambao ni zaidi ya watu bilioni 2, walichanganyikiwa na kushangazwa na ujumbe usio wa kawaida kutoka kwa WhatsApp. Katika ujumbe huo, WhatsApp ilitangaza kuwa, ili kuendelea kutumia jukwaa hili, watumiaji wanapaswa kukubaliana na sheria mpya za programu hiyo na kuiruhusu WhatsApp kutoa habari na taarifa binafsi za watumiaji wake kwa shirika la Facebook. WhatsApp ilitangaza kuwa watumiaji ambao hawakubaliani na sharti hilo hawawezi kutumia tena programu hiyo.
Tukio hilo lilizua wimbi kubwa la ukosoaji sio tu dhidi ya WhatsApp bali pia Facebook yenyewe, ambayo ndio mmiliki mkuu wa WhatsApp na kampuni yake nyingine tanzu, Instagram. Hii ni licha ya ukweli kwamba, tangu kuanzishwa kwake, WhatsApp imekuwa ikidai kulinda usiri wa watumiaji wake. Vilevile Pavel Durov, mmiliki wa mtandao wa kijamii wa Telegram, anasema kuwa WhatsApp ina matundu mengi ya usalama na sio mtandao salama, na kwamba wadukuzi wanaweza kupata taarifa zote zilizoko kwenye simu za watumiaji wa WhatsApp. Anasema: Kwa kutuma video au simu tu kupitia WhatsApp, wadukuzi wanaweza kuingia kwenye taarifa zako zote na kuzidukua.

Google ni kampuni inayojulikana sana ya Kimarekani katika uwanja wa teknolojia ya habari, ikijumuisha utafutaji taarifa za mtandaoni, programu na kadhalika. Kampuni hiyo ilianzishwa na Larry Page na Sergey Brin, ambao wote walikuwa wanafunzi wa PhD katika Chuo Kikuu cha Stanford na walijulikana kama "Google Men". Hii leo, watu wengi duniani hutumia injini hii ya utafutaji mahiri. Lakini je, faragha ya watumiaji inaheshimiwa katika matumizi ya kampuni hii kubwa ya teknolojia ya mawasiliano?
Ingawa Google imezingatia sana ufaragha wa mtumiaji katika toleo jipya zaidi la Android, lakini ushahidi unaonyesha kuwa kampuni hiyo imefanya vigumu kuficha eneo (location ) kwa watumiaji wa mfumo huu wa uendeshaji wa vifaa vya kielektoniki. Ukweli ni kwamba, wakati kitufe cha chaguo la eneo cha vifaa vya Android kinapokuwa kimezimwa, kampuni hiyo ya Google huwa inaendelea kukusanya data zinazohusiana na eneo la watumiaji na kuzitumia data hizo! Jambo la kuzingatiwa hapa ni kwamba, idadi kubwa ya wahandisi na wakurugenzi wa Google walifahamu vyema suala hili.
Kwa kuzingatia uhalifu huu, Mwanasheria wa Serikali (AG) katika jimbo la Arizona, ameifungilia mashtaka Google kwa ulaghai wake kuhusu location ya watumiaji wa vifaa vya Android. AG alisema kuwa Google imetumia wenzo wa "eneo" (location) wa vifaa vya watumiaji wake kwa manufaa ya kibinafsi wakati kitufe cha wenzo huo kinapokuwa kimezimwa. Hii ni pamoja na kwamba, kampuni ya Google ilikuwa imewaaminisha watumiaji wake kwamba kuzima kitufe cha location kuna maana ya kuficha eneo la mtumiaji!

Kulingana na utafiti uliofanywa na Tume ya Biashara ya Serikali ya Shirikisho ya Marekani, YouTube, ambayo ni mojawapo ya makampuni yaliyo chini ya kundi la Google, Ilikiuka faragha ya watumiaji wake watoto, na kwa sababu hii, Google ilihukumiwa kulipa faini ya dola milioni 170 mnamo Septemba 2019. Kwa mujibu wa shutuma hizo, mtandao wa kijamii wa YouTube ulikuwa ukikusanya taarifa kutoka kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 13 bila idhini na utambuzi wa wazazi wao. Tume ya Biashara ya Shirikisho la Marekani, katika notisi yake ya mashtaka, ilidai kuwa Google ilitumia maelezo yaliyokusanywa kwa ajili ya kutayarisha na kutoa matangazo yaliyowalenga watoto, kinyume na Sheria ya Kulinda Faragha ya Watoto Mtandaoni ya 1998. Hii ni baadhi tu ya mifano michache sana ya uhalifu na udukuzi unaofanywa na mitandao ya kijamii dhidi ya watumiaji wake.

Kwa utaratibu huu, inaonekana kwamba usalama na faragha ya watu vinapuuzwa zaidi katika zama hizi kuliko siku za nyuma kutokana na kuibuka na kustawi kwa mtandao ya kijamii na teknolojia ya habari na mawasiliano; na haki za mtu binafsi na za kijamii hazizingatiwi ipasavyo. Hata hivyo kwa kuzingatia umuhimu wa suala hili na athari zake mbaya kwa kila mwanajamii, suala hili haliwezi kuachwa bila kutafutiwa ufumbuzi.

Ingawa suala la faragha linaweza kuzusha mjadala katika kuarifisha dhati ya faragha na mipaka yake, lakini ni muhimu kuchukua hatua kama vile masuluhisho ya kisheria, kuandaa kanuni za pamoja na mambo mengine kama vile mbinu mpya za usimbaji fiche (encryption). Wakati huo huo, kuwahimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kulinda taarifa zao za kibinafsi kunaweza kuwa hatua ya awali na muhimu sana katika hali ya sasa.