May 23, 2023 09:54 UTC
  • Ukatili wa silaha za moto katika shule za Marekani na kimya cha wabunge

Ukatili wa kutumia silaha katika shule za Marekani, ambao mbali na kusababisha idadi kubwa ya vifo na majeruhi miongoni mwa watoto na vijana, vilevile umeibua hofu na wasiwasi kwa wanafunzi na wazazi wao, na unatambuliwa kuwa tatizo kubwa katika sekta ya elimu nchini humo.

Tukio la hivi karibuni zaidi la ufyatuaji risasi ovyo dhidi ya wanafunzi nchini Marekani, ni lile la Machi mwaka huu, katika shule ya binafsi huko Nashville, Tennessee, lililosababisha vifo vya wanafunzi watatu na wafanyakazi watatu wa shule hiyo.

Kulingana na utafiti uliochapishwa katika toleo la Desemba 2022 la Journal of the American Academy of Pediatrics, majeraha yanayohusiana na mashamblizi ya bunduki sasa ndiyo chanzo kikuu cha vifo vya watu walio na umri wa chini ya miaka 24 nchini Marekani. Ripoti ya Everytown pia imeonyesha kuwa, kuanzia mwaka 2015 hadi 2020, kulikuwa na kesi zisizopungua 2,700 za mashambulizi ya bunduki yaliyofanywa na watoto wenye umri wa chini ya miaka 18 nchini Marekani, ambayo yaliua watu 765 na kujeruhi wengine 1,366.

Ripoti ya karibuni ya Kituo cha Kitaifa cha Elimu cha Marekani, inaeleza kuwa mashambulizi ya risasi katika shule za nchi hiyo katika mwaka wa masomo wa 2020-2021 yalifikia kiwango cha juu zaidi katika miaka 20 iliyopita. Kwa mujibu wa ripoti yenye kurasa 31 iliyochapishwa na Kituo cha Kitaifa cha Elimu cha Marekani, jumla ya visa 93 vya ufyatuaji risasi vilitokea katika shule za msingi na sekondari za umma na za binafsi katika mwaka wa shule wa 2020-2021, ikiwa ni pamoja na hujuma 43 za bunbuki zilizosababisha vifo, na kesi 50 za ufyatuaji risasi zilizosababisha majeruhi.

Ingawa kiwango cha ukatili wa mashambulizi ya silaha katika shule za Marekani dhidi ya watoto wa umri wa kati ya miaka 12 hadi 18 kilikuwa cha chini mwaka wa 2019 ikilinganishwa na mwaka wa 2009, lakini mwaka 2021 kuliripotiwa visa vingi zaidi vya mashamblizi ya silaha za moto yaliyosababisha mauaji mashuleni kuliko mwaka mwingine wowote tangu kuanza shughuli ya ukusanyaji wa data hizo mapema muongo wa 2000. Mashambulizi 93 yaripotiwa mwaka 2021 ikilinganiswha na mashambulizi 11 ya bunduki mwaka 2009. Afisa wa usalama wa Marekani anasema kuhusiana na suala hili: "Athari za kudumu za uhalifu huu haziwezi kupimwa kwa takwimu pekee, ingawa data hizi ni muhimu kwa watunga sera, maafisa wa shule na wanajamii kwa ajili ya kutambua na kuchukua hatua za kuzuia na kushughulikia tatizo hilo."

Hapana shaka kuwa, mashambulizi ya silaha za moto mashuleni ni sehemu ndogo tu ya hujuma na mashambulizi ya bunduki yanayoua watu kila siku nchini Marekani. Takwimu za shirika lisilo la serikali linalofuatilia ukatili wa silaha nchini humo zinaonesha kuwa, zaidi ya watu 21,500 waliuawa kwa kupigwa risasi nchini Marekani mwaka 2020.

Katika hali ambayo wanafunzi wa shule za Marekani wanahitaji mazingira salama na yasiyo na vurugu ili kupata elimu mashuleni, lakini inasikitisha kuwa watoto na vijana ambao wamechagua njia ya kutafuta elimu na maarifa katika nchi hiyo wanakabiliwa na hatari ya ukatili na mauaji ya silaha za moto, na wasiwasi wa uwezekano wa kukabiliwa na mashambulizi ya silaha unasababisha athari mbaya za kisaikolojia na kinafsi kwa wanafunzi wa Marekani.

Kuwepo mazingira salama, yenye afya na amani ni miongoni mwa masharti ya kuwepo mazingira yanayofaa na mazuri kwa ajili ya wanafunzi. Hata hiyo hali katika shule za Marekani inazidi kuwa mbaya kiasi kwamba, baadhi ya watengenezaji wa vifaa vya shule wamezindua mikoba ya kuzuia risasi, au wanafunzi wa shule za msingi na upili wanafanya mazoezi mara kwa mara ya jinsi ya kukabiliana na uwepo wa mpiga risasi katika mazingira ya shule; na hii ni hatua iliyochukuliwa na serikali badala ya kufanya marekebisho ya kimsingi ya hali hiyo ya kutisha.

Mazingira mabaya na yasiyofaa ya elimu kwa ajili ya wanafunzi yanayosababishwa na vitisho vya hujuma na mashambulizi ya silaha za moto yamewafanya maelfu ya wanafunzi kuacha shule katika miezi ya hivi karibuni kote nchini Marekani ili waweze kushiriki katika maandamano ya kupinga sheria za umiliki wa bunduki.

Takwa la pamoja la wanafunzi wa Marekani ni kupigwa marufuku uuzaji wa silaha za moto na bunduki kubwa kama ile iliyotumiwa na Nikolas Cruz katika mauaji ya Shule ya Upili ya Marjory Stoneman. Februari 14, 2018, Nikolas Cruz aliyekuwa na umri wa miaka 19 alishambulia Shule ya Upili ya Marjory Stoneman Douglas huko Florida, na kuua watu 17 na kuwajeruhi wengine 15. Hiyo ilikuwa hujuma mbaya zaidi ya shambulizi la bunduki mashuleni katika historia ya Marekani.

Hujuma ya Nikolas Cruz katika Shule ya Upili ya Marjory Stoneman Douglas

Licha ya miito mingi iliyotolewa sehemu mbalimbali za Marekani ya kutaka kubadilishwa sheria zinazohusiana na ubebaji wa silaha, ambao unatambuliwa kuwa sababu kuu ya kukithiri kwa ukatili na mauaji yakiwemo yale yanayoshuhudiwa katika shule za nchi hiyo, lakini kimya cha maafisa wakuu na watunga sheria (wabunge) wa Merekani katika suala hili ni jambo la kutiliwa maana sana.

Uhuru wa kutumia silaha nchini Marekani unasababisha machafuko ya kila siku ya ufyatuaji ovyo wa risasi kote nchini humo; Lakini makundi ya mashinikizo yanayotetea umiliki wa bunduki yana nguvu kubwa kiasi kwamba, hata Bunge la Congress la Marekani haliko tayari kupitisha sheria za kudhibiti ubebaji wa silaha. Ripoti ya Kituo cha Utafiti cha Congress ya Marekani inasema, raia wa Marekani wanamiliki takriban nusu (yaani asilimia 48) ya jumla ya silaha za moto, yaani bunduki milioni 650 kote duniani.

Kutokana na ongezeko la ukosoaji katika vyombo vya habari na pia katika duru za umma, hasa wasiwasi wa familia kuhusu kukithiri kwa ukatili wa kutumia silaha za moto nchini Marekani, maafisa wa serikali ya nchi hiyo wamelazimika angaa kijitokeza hadharani na kuzungumzia hali hiyo ya kutisha na ya mchafukoge katika hotuba zao au kwenye mitandao ya kijamii. Rais wa Marekani, Joe Biden, hivi majuzi alikosoa utamaduni wa kumiliki bunduki nchini mwake na kusema kuwa, watoto hawawezi kuhudhuria sherehe za kuzaliwa kutokana na hofu ya kupigwa risasi. Biden aliandika kwenye Twitter kwamba: "Bunduki ndio sababu kuu ya mauaji ya watoto nchini Marekani, na idadi inaongezeka. Kitu gani kimeisibu nchi yetu kiasi kwamba watoto hawawezi kuhudhuria sherehe ya kuzaliwa bila hofu? Hadi lini wazazi wataendelea kuwa na wasiwasi kila mara watoto wao wanapoenda shuleni, ukumbi wa michezo au kwenye bustani?"

Ujumbe huo wa Twitter wa Biden ulichapishwa siku moja baada ya takriban watu 4 kuuawa na wengine zaidi ya 28 kujeruhiwa kwenye sherehe ya kuzaliwa barobaro wa Kimarekani huko Dadeville, Alabama.

Licha ya Rais wa Marekani kukiri waziwazi juu ya hali ya kutisha ya mazingira ya shule za nchi hiyo, lakini kukiri huko kuchungu kwa Biden kwamba Marekani siyo salama kwa watoto, na vilevile marekebisho ya kimaonyesho tu yaliyofanywa na serikali yake katika sheria ya bunduki havitatui mgogoro wa sasa katika shule za nchi hiyo, sambamba na uwepo wa kiwango kikubwa cha bunduki na silaha za moto baina ya raia wa Marekani na ushawishi mkubwa wa makundi ya mashinikizo yanayotetea umiliki wa bunduki na biashara ya silaha za moto.

Mashambulizi ya kutumia silaha moto na mauaji katika shule za Marekani huenda yakashika kasi zaidi kwa kuendelea kuwepo sheria za sasa za umiliki wa bunduki. Tangu 1999, wakati duru za kielimu zilipoanza kulengwa baada ya mauaji ya Shule ya Upili ya Columbine, hali hii imeendelea kushuhudiwa nchini Marekani. Kwa mfano, kumeshuhudiwa mauaji makubwa katika Chuo Kikuu cha Virginia Tech (2007), Shule ya Msingi ya Sandy Hook (2012), na Shule ya Upili ya Parkland (2018). Tangu baada ya ufyatuaji risasi katika shule ya Columbine mnamo 1999, zaidi ya wanafunzi laki 3 na 38 elfu wa Marekani wamepitia vurugu na ukatili wa kutumia silaha katika shule zao.

Ripoti za Taasisi ya "Sandy Hook Promise", ambayo inajishughulisha na kazi ya kurekodi visa vya ukatili wa kutumia silaha mashuleni na kutoa mafunzo ya kukabiliana na mashambulizi hayo, inakiri kuwa: Ukatili wa kutumia silaha za moto na risasi shuleni ni janga makhsusi la Marekani ambalo linasababisha mauaji ya watoto kila siku.

Mtaalamu wa vitendo vya ufyatuaji risasi ovyo katika shule wa Marekani, Cheryl Lero Johnson anasema: Kila tukio kubwa la ufyatuaji risasi linapelekea kutolewa wito wa wazazi wa kuzidishwa usalama mashuleni ili kuhakikisha watoto wao hawawi wahanga wa Columbine, Virginia Tech au Sandy Hook nyingine.

Maafa yanakuwa dhahiri zaidi wakati, ripoti ya "Gun Safety Support Foundation in Every City" inapoonyesha kuwa, zaidi ya asilimia 95 ya shule za msingi za Marekani zinafanya mazoezi ya kujiandaa kwa mshambuliaji silaha za moto; mazoezi ambayo badala ya kuwaandaa wanafunzi kwa ajili ya hujuma kama hizo yanawazidishia hali ya hofu na ukosefu wa amani.

Ushawishi wa makundi ya watetezi wa uuzaji na ununuzi wa bunduki, maarufu zaidi likiwa lile la National Rifle Association (NRA), una taathira kubwa katika matukio ya ukatili wa mara kwa mara wa silaha za moto na ufyatuaji wa risasi unaosababisha vifo vya wanafunzi mashuleni na katika mazingira ya elimu nchini Marekani. Likiwa na wanachama milioni tano, NRA linawekeza mamia ya mamilioni ya dola kwa ajili ya kuwaunga mkono na kuwafadhili wagombea wa chama cha Republican wanaopinga sheria kali zaidi za kudhibiti umiliki wa silaha. Katika miaka ya karibuni makundi haya yameweza kuwa na taathira kubwa katika siasa na sera za Marekani zinazohusiana na uuzaji na ununuzi wa silaha kutokana na bahashishi zinayopewa kutoka kwa mashirika na makampuni ya kutengeneza silaha na raia wanaotetea umuliki wa silaha za moto. 

Baadhi ya ripoti zinasema, Chama cha Kitaifa cha Bunduki kinatumia kiasi kikubwa cha fedha ambacho ni mara 15 zaidi ya kiwango cha fedha zinazotumiwa na wapinzani wa umuliki wa bunduki kwenye matangazo; na kupitia ushawishi wake wa kisiasa, kimeweza kuzuia mabadiliko ya sheria katika eneo hili.

National Rifle Association (NRA), ina ushawishi mkubwa kati ya wahafidhina na mrengo wa kulia wa Marekani. Himaya na uungaji mkono mkubwa wa Rais wa zamani, Donald Trump, na maseneta wa Republican kama Ted Cruz, unaweza kutathminiwa katika uwanja huu.