Umaskini na Ukosefu wa Makazi nchini Marekani
Miji ya Marekani ambayo ina taswira ya kuvutia na iliyojaa anasa wakati unapoangalia kutoka kwa mbali, inakabiliwa na ukweli mchungu wa uozo wa kimaadili na ukosefu wa makazi unapoingia ndani na kuangalia kwa karibu.
Yumkini baadhi ya watu wakahoji: Je, huko Marekani pia kuna tatizo la ukosefu wa makazi? Naam, nchi hiyo tajiri ina idadi kubwa zaidi ya watu wasio na makazi kati ya nchi zote zilizoendelea. Inatupasa kueleza hapa kuwa, hali ya idadi ya watu wasio na makazi katika jamii ina uhusiano na masuala kama vile umaskini uliokithiri, ukosefu wa ajira, uraibu wa dawa za kulevya na unyanyasaji wa wajumbani, na hapana shaka kwamba, kutokuwa na makazi na mahali pa kuishi kunatambuliwa kuwa ni mstari wa mwisho wa waathiriwa na unyanyasaji na matatizo ya kijamii nchini Marekani.
Uchunguzi uliofanywa na serikali na mashirika ya kujitegemea kwa nyakati tofauti umetoa takwimu tofauti kuhusu muundo wa jamii ya watu wasio na makazi huko Marekani. Hata hivyo, katika miaka kumi iliyopita, kuna makubaliano kwamba, moja ya tano ya Wamarekani wasio na makazi ni watoto, na 40% kati yao ni watu walio chini ya umri wa miaka 18. Takriban asilimia 8 ya watu wasio na makazi ni wastaafu wa jeshi, na waliosalia ni wanawake, jamii za waliowachache kikaumu na kimbari, waraibu wa dawa za kulevya au pombe, wazee, watu weusi, na watu wenye magonjwa ya akili.

Takwimu zilizoripotiwa juu ya ukosefu wa makazi huko Marekani zinatofautiana sana, na hili ni tatizo la muda mrefu. Vilevile kuna tofauti kubwa kati ya takwimu za serikali na takwimu za mashirika yasiyo ya serikali. Mnamo 2014 Shirika la Muungano wa Kitaifa wa Kukomesha Ukosefu wa Makazi (National Alliance to End Homelessness), ambalo limekuwa likifanya kazi tangu 1983, lilitangaza kuwa idadi ya watu wasio na makazi nchini Marekani ni karibu milioni moja na nusu; Takwimu ambayo haikukubaliwa na serikali. Kwa upande mwingine, Idara ya Makazi na Maendeleo ya Miji ya Merekani mwaka 2018 ilitangaza idadi ya watu wasio na makazi kuwa ni 553,000. Ingawa mashirika ya umma yaliripoti kuongezeka kwa Wamarekani wasio na makazi, haswa katika miji mikubwa tangu 2016, lakini serikali bado inashikilia idadi hiyo hiyo ya watu karibu 500,000 wasio na maskani. Mwaka 2021, serikali ya Marekani ilitangaza ongezeko la 2.7% la watu wasio na makazi katika nchi hiyo ikilinganishwa na mwaka wa kabla yake na ongezeko la karibu 16% katika jimbo lenye watu wengi zaidi, yaani California, na hatimaye ikakubali kwamba idadi ya watu wasio na makazi ni 567,000.
Vyovyote itakavyokuwa, mamilioni ya Wamarekani hupitia hali ya ukosefu wa makazi mara kwa mara, na ikiwa tutakubali takwimu za serikali, basi zaidi ya watu 500,000 wasio na makazi hulala mitaani katika pembe mbalimbali za Marekani kila siku.
Ben Carson, aliyekuwa Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Miji wa Marekani hadi mwaka 2021, alitangaza hivi karibuni kwamba: "Tunaendelea kushuhudia ongezeko la idadi ya watu wasio na makazi mitaani katika maeneo ya Magharibi mwa nchi (Marekani); ambako gharama ya nyumba iko juu sana." Ben Carson alitoa tahadhari nyingine kwa jamii ya Marekani. Katika siku ambazo, kulingana na uchunguzi, ukosefu wa makazi katika majiji makubwa ulikuwa ukiongezeka, waziri huyo wa zamani alisema: "Ukosefu wa makazi sio tatizo la Serikali ya Shirikisho pekee, bali ni tatizo la nchi nzima. Ukosefu wa makazi huko California uko katika hatua mbaya na unahitaji kushughulikiwa haraka na maafisa wa serikali za mitaa na serikali za majimbo."
Kabla ya hapo, uchunguzi wa serikali ulionyesha kuwa ukosefu wa makazi umeongezeka katika majimbo 21 ya Marekani; hasa katika majimbo ya California na New York. Majimbo haya yana idadi kubwa zaidi ya familia zisizo na makazi nchini Marekani. Mnamo 2021, watu wazima na watoto laki moja na 7,510 wasio na makazi walilala katika makazi wa Idara ya Watu Wasio na Makazi ya Jiji la New York (DHS); na 31,947 kati yao walikuwa watoto. Takwimu zinaonyesha kuwa, idadi ya wakazi wa New York wasio na makao wanaolala katika kambi za manispaa imeongezeka kwa asilimia 16 ikilinganishwa na miaka kumi iliyopita, na idadi ya watu wazima wasio na makazi imeongezeka kwa asilimia 91, ikilinganishwa na miaka kumi iliyopita. Utafiti pia unaonyesha kwamba, ikilinganishwa na familia zisizo na makazi, watu wazima ambao hawajaoa au kuolowe wasio na makazi wana kiwango kikubwa cha watu wenye magonjwa mabaya ya akili, matatizo ya uraibu na matatizo mengine makubwa ya afya.
Gazeti la New York Times pia lilitangaza katika ripoti yake kwamba: "Asilimia 15 ya watu wasio na makazi, yaani karibu watu elfu 85, hawana makazi daima". Vigezo vya Marekani vya watu wasio na makazi daima ni kwamba mtu amekuwa bila makazi kwa zaidi ya mwaka mmoja, na haya yote yalikuwa kabla ya maambukizi ya Corona; Wakati mamilioni ya Wamarekani walikuwa bado hawajapoteza ajira zao. Sasa, kulingana na utafiti, Chuo Kikuu cha Columbia kimetangaza kwamba idadi ya watu wasio na makazi inaweza kuongezeka kwa 45% kutokana na kupoteza kazi na udhaifu wa kifedha wa kulipa kodi. Tukijumuisha na takwimu za serikali, hii ina maana kwamba zaidi ya watu laki mbili na 55 elfu waliongezeka katika idadi ya Wamarekani wasio na makazi.
Utafiti wa Wizara ya Elimu ya Marekani mwaka 2018 pia ulionyesha kuwa zaidi ya wanafunzi milioni 1.5 walipitia hali ya ukosefu wa makazi katika mwaka wa shule; Wengi wao wamekaa kwa muda au kwa kudumu kwenye nyumba za marafiki au familia, na sehemu ndogo wamelala mitaani na katika maeneo ya umma kwa muda.
Ukosefu wa makazi uliongezeka kuanzia mwaka 1870 katika miji inayoendelea ya Marekani ikijumuisha New York na kuwa tatizo la kitaifa. Wahamiaji waliokwenda kwenye miji mikubwa kwa ajili ya kutafuta kazi ndio waliounda idadi kubwa zaidi ya watu wasio na makazi, na baadhi ya wakazi maskini zaidi wa miji hiyo pia walijiunga na kundi la watu wasio na makazi kutokana na kupanda kwa gharama za kukodi ya nyumba. Baadaye katika miaka ya 1930, idadi ya watu wasio na makazi iliongezeka tena na kubaki juu kwa takriban muongo mmoja kutokana na mdororo mkubwa wa kiuchumi ulioikumba nchi hiyo. Wakati huo, idadi ya watu wasio na makazi huko Marekani ilikadiriwa kuwa zaidi ya watu milioni 2.

Katika miaka ya 1980, baadhi ya wabunge wa Kongresi waliidhinisha sheria ya kuwasaidia wasio na makazi, ambayo ilijulikana kama Sheria ya McKinney-Vento, na Rais wa wakati huo wa Marekani, Ronald Reagan alitia saini sheria hiyo mwaka 1987. Katika miaka ya 1990, maeneo ya malazi na kugawa chakula kwa watu wasio na makazi na wenye njaa yaliongezeka kutokana na bajeti iliyotengwa kutokana na kupasisha sheria hiyo, pamoja na usaidizi mwingine unaohusiana na ukosefu wa makazi katika miji mikubwa.
Hali hii iliendelea hadi ulipotokea mgogoro wa kifedha wa 2008 na hali ikawa mbaya tena. Wakati huo Barack Obama ililazimika kutia saini sheria kadhaa za dharura ili kuzuia kasi ya ongezeko la ukosefu wa makazi na kutenga bajeti kubwa zaidi ya umma kwa ajili ya kutoa huduma za kimsingi kwa watu wasio na makazi. Hata hivyo hali ya ukosefu wa Makazi bado ni kubwa nchini Marekani na inaongezeka siku baada ya nyingine.
Swali linalojitokeza ni kwamba, imekuwaje ukosefu wa makazi huko Marekani umekuwa tatizo la miaka 150? Kwa nini utajiri na nguvu za kiuchumi za Marekani zisiweze kukidhi hitajio hili la kimsingi kwa raia wake na kutayarisha makazi kwa ajili yao?
Jibu la maswali haya linapaswa kutafutwa katika mfumo wa kiuchumi na kisiasa unaoongoza jamii ya Marekani. Ripoti ya Philip Alston, Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu umaskini uliokithiri na haki za binadamu mwaka 2018, inaeleza sera ya serikali ya Marekani kuhusu umaskini na inaangazia ukweli wa jamii ya Marekani ya leo. Alston anasema: "Jibu la Marekani kwa umaskini katika karne ya 21 ni kuwaadhibu maskini na kuwafunga jela. Wafanyakazi ambao hawawezi kulipa madeni yao, raia ambao hawawezi kulipa makampuni binafsi ya dhamana, watu wasio na makazi, wagonjwa wa akili, baba ambao hawawezi kulipa gharama za maisha za watoto wao na wengine wengi hupata majibu kama haya; adhabu au kufungwa jela. Kifungo cha umati kinatambuliwa kama suluhisho la kuondoa matatizo ya kijamii nchini Marekani."
Ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya umaskini nchini Marekani ilikabiliwa na majibu hasi na makali kutoka kwa maafisa wa serikali ya nchi hiyo. Mojawapo ya sababu ni kwamba, katika sehemu inayohusu ukosefu wa makazi, ripoti hiyo inahitimisha ikisema: "Ukosefu wa makazi katika kiwango hiki unaweza kusuluhishwa kabisa, ingawa maafisa wa serikali wanategemea zaidi mabavu na mkono wa chuma, na sio kutayatarisha nyumba za bei nafuu, kutoa matibabu, ushauri wa kisaikolojia na mafunzo ya jinsi ya kupata ajira. Mifumo mipya ya kurekodi data za watu wasio na makazi nchini Marekani inawapa watu hao wasio na makazi hisia kwamba, wanalazimika kutoa haki yao ya faragha mkabala wa kupata haki ya kuwa na makazi."
Sentensi hii ya mwisho ya Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya umaskini uliopindukia na ukosefu wa makazi nchini Marekani inatoa maana ambayo ni pana zaidi ya tatizo la kiuchumi. Huwenda sentensi hii ina maana ya matajiri kuwadhibiti watu maskini katika jamii ya nchi hiyo. Alaa kulli hal, ukosoaji na shutuma za mara kwa mara dhidi ya mfumo wa kisiasa unaotawala Marekani ni kwamba unatumikia maslahi ya matajiri na kuwatelekeza watu maskini.