Mar 25, 2018 14:26 UTC
  • Ripoti: Uingereza inaficha uuzaji wa silaha Mashariki ya Kati kwa mikataba ya siri

Ripoti ya karibuni imefichua kuwa Uingereza inatumia vibali vya siri kuficha kiwango cha silaha zake inazoziuza kwa nchi zenye rekodi za kutisha kuhusu haki za binadamu katika eneo la Mashariki ya Kati.

Tovuti ya habari ya Middle East Eye Online imeeleza kuwa takwimu zilizokusanywa na Harakati dhidi ya Biashara ya Silaha (CAAT) zinaoonyesha kuwa hatua ya Uingereza ya kutumia vibali vya wazi vyenye utata kuidhinishia uuzaji wa silaha katika Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika imeongezeka kwa asilimia 22. Ripoti hiyo imebainisha kuwa, Uingereza imekuwa ikificha kanuni za siri za uuzaji silaha ili kukwepa upinzani wa wananchi ili kuficha thamani ya silaha na kiwango inachouza katika nchi za eneo la Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika.

Watoto ni waathirika wakubwa wa hujuma ya Saudia dhidi ya Yemen. Hujuma hiyo inategemea silaha za nchi za Magharibi, Uingereza ikiwemo

Ripoti hiyo imeongeza kuwa silaha zinazouzwa na Uingereza kwa mwaka zina thamani ya dola bilioni 8.3 kwa uchumi wa nchi hiyo. Chini ya mpango huo wa mauzo ya siri unaofanywa na Uingereza, Saudi Arabia ndiyo mnunuaji mkubwa wa silaha kutoka nchi hiyo. Watu wasiopungua 14,000 wameuawa tangu Saudi Arabia ianzishe uvamizi wake wa kijeshi huko Yemen mwezi Machi mwaka 2015.  

 

Tags