Jun 26, 2016 10:50 UTC
  • Shambulio la kigaidi nchini Somalia

Shambulio la kigaidi la wanamgambo wa al-Shabab dhidi ya hoteli moja katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu kwa mara nyingine tena limepelekea zaidi ya watu 40 kuuawa na kujeruhiwa.

Hoteli ya Nasa Hablod iliyoko katika mji wa Mogadishu Jumamosi ya jana ilikabiliwa na shambulio la kigaidi la wanamgambo wa al-Shabab ambapo kwa akali watu 15 waliuawa. Ripoti ya Polisi ya Somalia inaeleza kuwa, mtu mmoja aliyekuwa kwenye gari lililokuwa na mada za milipuko ndiye aliyetekeleza shambulio hilo mbele ya mlango wa kuingilia hotelini hapo. Aidha baada ya mlipuko huo watu kadhaa waliokuwa na silaha waliingia katika hoteli hiyo na kuwateka nyara watu kadhaa.

Polisi ya Somalia inasema kuwa, watu 15 wameuawa na wengine 27 kujeruhiwa katika shambulio hilo. Hadi sasa hakujatangazwa idadi kamili ya watu waliotekwa nyara katika shambulio hilo la kigaidi. Kundi la kigaidi na wanamgambo wa al-Shabab limetangaza kuhusika na sambulio hilo. Hili ni tukio la hivi karibuni kwa hoteli mjini Mogadidhu kukabiliwa na shambulio la kigaidi. Shambulio jingine la kigaidi lilikuwa dhidi ya hoteli ya Ambassador ambapo watu wasiopungua 10 waliuawa. Wataalamu wa mambo wanaamini kuwa, shambulio la jana la wanamgambo wa al-Shabab lilikuwa ni jibu kwa mafanikio ya jeshi la Somalia katika kupambana na kundi hilo la kigaidi.

Juma lililopita vikosi vya Somalia viliwaua wanachama 7 wa kundi la al-Shabab lenye misimamo ya kuchupa mipaka katika operesheni yake dhidi ya wanamgambo hao katika eneo la Galgaduud katikati mwa nchi hiyo.

Kamanda wa kijeshi wa Galgaduud sanjari na kuonesha kuridhishwa kwake na mwenendo wa utekelezwaji wa operesheni dhidi ya wanamgambo wa al-Shabab katika eneo lake hilo amesema kuwa, vikosi vyao vimefanikiwa kung'oa mizizi ya kundi hilo katika eneo la Galgaduud.

Kundi la wanamgambo wa al-Shabab ni miongoni mwa makundi ya wanamgambo barani Afrika ambalo kwa muda mrefu limeifanya Somalia kuwa ngome yake ya kutekelezea operesheni za kigaidi ambapo jeshi la Somalia likishirikiana na kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Afrika AMISOM kwa miaka kadhaa sasa limekuwa likifanya juhudi za kupambana na kundi hilo. Wanachama wa kundi hilo ambao wametimuliwa na kukimbilia katika vijiji vya kusini mwa Somalia wangali wanaendeleza mashambulio yao dhidi ya wanajeshi na raia wa kawaida.

Mbali na Somalia wanamgambo wa al-Shabab wamekuwa wakiendesha mashambulio yao katika nchi jirani kama vile Kenya. Hata kama kwa miaka kadhaa sasa makundi ya wanamgambo yamekuwa yakiendesha harakati zao barani Afrika, lakini katika miaka ya hivi karibuni wigo wa harakati za makundi hayo umechukua mkondo mpana zaidi. Filihali, makundi ya al-Shabab, Boko Haram na al-Mutarabituun ni miongoni mwa makundi amilifu ya wanamgambo kwa sasa katika bara hilo. Muda si kitambo kundi la al-Shabab lilitangaza mfungamano wake na kundi la mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda na likashadidisha mashambulio yake nchini Somalia. Hii ni katika hali ambayo, kwa muda sasa Somalia imekuwa ikipitia katika kipindi kigumu na hali mbaya ya mchafukoge kutokana na harakati za kigaidi na sokomoko la kisiasa. Hali hiyo imewafanya raia wengi wa Somalia kulazimika kuwa wakimbizi. Fauka ya hayo Somalia inakabiliwa na tatizo la ukame na uhaba wa chakula hali ambayo imeongeza matatizo juu ya matatizo ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Licha ya serikali ya Somalia kufanya kila iwezalo ikishirikiana na AMISON kuhakikisha kwamba, inaisafisha nchi hiyo na uwepo wa wanamgambo wa Somalia, lakini juhudui zake zinaonekana kutozaa matunda kwa sasa.

Shambulio la jana pia mjini Mogadishu linatathminiwa na wajuzi wa mambo kuwa, limefanyika katika fremu ya kuzidi kuitumbukiza Somalia katika vurugu na machafuko na hivyo kukwamisha juhudi za serikali za kurejesha amani na uthabiti katika nchi hiyo.

Tags