Kutolewa dikrii ya kufutiliwa mbali Vikosi vya Msaada wa Haraka vya Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i101972-kutolewa_dikrii_ya_kufutiliwa_mbali_vikosi_vya_msaada_wa_haraka_vya_sudan
Abd al-Fattah al-Barhan, Kamanda wa Jeshi na Mkuu wa Baraza Tawala la Sudan, ametoa dikrii ya kufuiliwa mbali Vikosi vya Msaada wa Haraka kwa mujibu wa kipengee cha katiba ya nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 07, 2023 23:13 UTC
  • Kutolewa dikrii ya kufutiliwa mbali Vikosi vya Msaada wa Haraka vya Sudan

Abd al-Fattah al-Barhan, Kamanda wa Jeshi na Mkuu wa Baraza Tawala la Sudan, ametoa dikrii ya kufuiliwa mbali Vikosi vya Msaada wa Haraka kwa mujibu wa kipengee cha katiba ya nchi hiyo.

Jenerali al Burhan

Hii ni katika hali ambayo, mjumbe mmoja wa Baraza la Ushauri la Vikosi vya Msaada wa Haraka, ameashiria dikrii iliyotolewa na al-Barhan ya kuvifuta vikosi hivyo na kusema uamuzi huo wa al-Barhan unaenda kinyume na katiba ya Sudan hivyo hautatekelezwa.

Dikrii ya al-Barhan ni tukio jipya katika mkondo wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan, ambavyo sasa vimeingia katika mwezi wake wa tano baada ya kuwa vimepelekea maelfu ya watu kuuawa na kujeruhiwa vimepelekea pia mamia ya maelfu ya wengine kukosa makazi na kusababisha uharibifu mkubwa nchini. Mapigano ya silaha kati ya vikosi vya Abd al-Fattah al-Barhan, Kamanda wa Jeshi na Mkuu wa Baraza la Mpito la Utawala wa Sudan, na Mohammed Hamdan Degalo aliyepewa jina la utani la "Hamidti", Naibu wa al-Barhan na Kamanda wa Vikosi vya Msaada wa Haraka yalianza huko Khartoum, mji mkuu wa Sudan, tangu Aprili 15, 2023 na kisha kuenea katika maeneo mengine ya nchi.

Mbali na Khartoum na Omdurman, mapigano kati ya pande mbili hizo hasimu yanaendelea katika majimbo ya Kordofan Kaskazini na Darfur Kusini. Usitishaji mapigano kati ya pande hizo umetangazwa mara kadhaa, lakini umekuwa ukikiukwa na pande husika kwa madhara ya raia wa kawaida wa Sudan. La muhimu ni kwamba kutokana na uwiano karibu sawa wa nguvu wa pande zinazohasimiana, na licha ya mapigano makali, lakini hakuna upande wowote uliofanikiwa kupata ushindi wa mwisho katika mapigano hayo. Sasa al-Barhan ameamuru kufutwa Vikosi vya Msaada wa Haraka kama mbinu ya kuushinda upande wa pili. Huku vita vikiendelea kati ya vikosi vinavyoongozwa na Jenerali Abdul Fattah al-Barhan na vile vya Hamidti, kundi kubwa la wanamgambo limetangaza kuwa liko tayari kujiunga na vikosi vya Hamidti.

Abdul Baqi Qarfa, kamanda wa wanamgambo wa vuguvugu maarufu linalojiita "Wafuasi wa Ukweli" wa Sudan lenye wapiganaji 25,000, lilitangaza Jumanne kupitia ujumbe wa video kwamba linamuunga mkono Jenerali Hamidti. Ahmed Abul Ghait, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, anasema: Mgogoro wa Sudan unaendelea na unaacha nyuma gharama kubwa ambayo iko nje ya uwezo wa watu wa Sudan...Sudan inakaribia kushuhudia vita vya pande zote vya wenyewe kwa wenyewe.

Ahmed Abul Ghait

Abd al-Fattah al-Barhan, alikuwa mkuu wa Baraza la Utawala la Sudan tangu Aprili 12, 2019 hadi Oktoba 25, 2021, baada ya kuondolewa madarakani Rais Omar al-Bashir, kufuatia maandamano makubwa ya watu wa Sudan. Ili kuimarisha nafasi yake, alichukua hatua kadhaa kama vile kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel na kuimarisha ushirikiano na Marekani, jambo ambalo bila shaka limekabiliwa na upinzani mkubwa wa Wasudani. Al-Barhan, licha ya kutoa ahadi nyingi za kukabidhi madaraka kwa raia, sio tu kwamba hakuchukua hatua yoyote muhimu katika uwanja huo, bali alifanya mapinduzi dhidi ya serikali ya mpito ya kiraia iliyoongozwa na Abdullah Hamdouk, ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa Sudan tangu Agosti 21, 2019, na kuindoa madarakani mnamo Oktoba 25, 2021 na hivyo kuchukua mamlaka kamili ya nchi hiyo.

Al-Barhan alivunja Baraza la Utawala, ambalo awali liligawa madaraka kati ya jeshi na raia. Vyama vya kisiasa vya Sudan vilitaja kuondolewa madarakani Waziri Mkuu Hamdok na kukamatwa viongozi na maafisa wa Sudan na jeshi kuwa mapinduzi ya kijeshi. Baada ya mapinduzi ya Oktoba 25, 2021 na kumalizika ushirikiano wa mpito na vyama vya siasa, Abdullah Hamdouk aliingia tena madarakani Novemba 21, 2021 kutokana na mashinikizo makubwa ya ndani na nje, na al-Barhan na Hamdouk wakatia saini makubaliano ya kisiasa ambayo yalijumuisha kurejeshwa waziri mkuu katika nafasi yake, kuundwa serikali ya wataalamu na kuachiliwa huru wafungwa wa kisiasa. Lakini hatimaye Hamdok alijiuzulu Januari 2, 2022 kutokana na kuendelea mivutano, na Osman Hussein akateuliwa kusimamia kwa muda nafasi ya waziri mkuu.

Mohammed Hamdan Dagalo "Hamidti"

Mnamo Desemba 2022, makubaliano yalifikiwa kati ya makundi ya kiraia na Baraza Tawala la Kijeshi la Sudan ili kutatua mzozo wa kisiasa wa nchi hiyo. Makundi hayo yalikubaliana juu ya kipindi cha mpito cha miezi 24 ambacho kingeanza tokea wakati wa kuteuliwa waziri mkuu wa mpito. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, serikali ya mpito ilitakiwa kuwa ya kiraia na kidemokrasia moja kwa moja bila ya ushiriki wa jeshi. Kutokana na hali mbaya ya kiuchumi na kijamii ya Sudan, kuendelea mkwamo wa kisiasa na kuongezeka ukosoaji dhidi ya utendaji kazi wa Baraza la Uongozi, hasa wa kujaribu kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni, ilitarajiwa tangu mwanzo kwamba mzozo wa madaraka katika nchi hiyo ya Kiafrika ungeibuka tena kutokana na dhamira ya wazi ya Jenerali al-Barhan ya kutaka kung'ang'ania madaraka ya nchi. Ingawa katika miaka ya karibuni kumekuwepo na makabiliano na tofauti kati ya serikali ya kiraia na jeshi, lakini sasa tofauti kubwa zinashuhudiwa katika ngazi ya makamanda wakuu wa jeshi yaani kati ya al-Barhan na Hamidti, jambo ambalo limepunguza pakubwa uwezekano wa kupatikana utatuzi wa haraka wa mgogoro unaoikabili nchi hiyo ya Kifrika.