Sep 28, 2023 02:59 UTC
  • Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC: Najisikia aibu hatujafanya kazi nzuri huko Sudan

Karim Khan, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) amezungumza na televisheni ya France 24 pambizoni mwa Mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa huko New York akikiri kwamba taasisi hiyo haijafanya kazi nzuri kuhusiana na yanayojiri nchini Sudan.

Khan ameashiria uchunguzi wa Mahakama ya ICC kuhusu jinai zonazodaiwa kufanywa na katika maeneo mbalimbali ya dunia na kujadili hali ya mambo huko Sudan ambapo Mahakama ya ICC imeanzisha uchunguzi mpya miezi miwili iliyopita kuhusu madai ya kujiri jinai za kivita huko Darfur. 

Alipoulizwa na mwandishi wa habari kuhusu waranti uliotolewa na Mahakama ya ICC wa kumtia mbaroni Rais Vladimir Putin wa Russia kwa kile kinachodaiwa kuwa kuhamishwa kinyume cha sheria watoto kutoka Ukraine hadi Russia, Khan amedai: Uchunguzi unaendelea kwa mapana zaidi kuhusu jinai mbalimbali zilizotekelezwa na zinazoendelea kufanywa kila siku na kwamba wajibu wao ni kupata ukweli. 

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai yenye makao yake huko Hague nchini Uholanzi amegusia pia mgogoro wa Sudan na hali ya mambo katika jimbo la magharibi mwa nchi hiyo la Darfur na kusema: ICC ina jukumu la kuchunguza matukio yaliyojiri tangu mwaka 2005 na kushughulikia wimbi jipya la machafuko lililoanza mwezi Aprili na taarifa za kuhuzunisha zinazotoka Sudan."

Vita Sudan 

Karim Khan amesema, siku chache zilizopita alikutana na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, Mkuu wa majeshi ya Sudan, na kwamba, licha ya pande za Sudan kutoa ahadi nyingi kuhusu haki za binadamu, lakini pande zinazozozana haziwasilisha ICC hata karatasi moja wala ushahidi wowote wa kweli kuhusu mgogoro unaondelea huko Sudan.  

Karim Khan amesema: "Tumedhamiria kuhakikisha kwamba tunapata ukweli. Watu wa Sudan, watu wa Darfur na wakimbizi walioko Chad wanahitaji kutambua kwamba, maamuzi na ahadi tulizotoa New York, au maazimio ya Mkataba wa Roma yanakuwa na natija." 

Tags