Bobi Wine, kiongozi wa upinzani Uganda atiwa mbaroni
Kwa mara nyingine tena, mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda ambaye pia alikuwa mgombea urais wa chama cha upinzani cha NUP katika uchaguzi uliopita, Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine, amekamatwa mjini Entebbe.
Hayo yametangazwa na David Lewis Rubongoya, Katibu Mkuu wa NUP katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa X (Twitter) na kueleza kuwa, Bobi Wine amekatwa leo katika uwanja wa ndege akirejea nchini kutoka ughaibuni.
Amesema: Rais wetu Bobi Wine, amechukuliwa na maafisa wa serikali mara tu alipotua katika uwanja wa ndege wa Entebbe.
Video iliyosambaa mitandaoni imeonyesha mwanasiasa huyo wa upinzani mwenye miaka 41 akivutana na na maafisa usalama ambao hawakuwa wamevalia sare zao rasmi, kabla ya kumtia nguvuni.
Polisi ya Uganda imekanusha madai kuwa Wine amekamatwa, ikisisitiza kuwa mwanasiasa huyo wa upinzani ambaye pia ni mwanamuzi maarufu nchini humo alisindikizwa tu na maafisa usalama hadi katika makazi yake mjini Kampala.
Taarifa ya polisi ya Uganda inasema: Tunapenda kuutarifu umma kuwa, Rais wa NUP, Mheshimiwa Kyagulanyi Robert, amesindikizwa kwa mafanikio na maafisa wetu kutoka Entebbe hadi nyumbani kwake Magere.

Hata hivyo viongozi wa upinzani nchini humo wanasisitiza kuwa, kinara huyo wa chama cha National Unity Platform NUP angali anashikiliwa na maafisa usalama wa nchi hiyo.
Katika uchaguzi wa rais wa Januari 16 mwaka 2021 na kwa mujibu wa matokeo ya Tume ya Uchaguzi, Museveni alishinda uchaguzi huo kwa kura milioni 5.85 sawa na asilimia 58.64 ya kura zote, huku Bobi Wine akipata kura milioni 3.48 sawa na asilimia 34.83 ya kura zote.