Askari 6 wa Misri wauawa katika mpaka na Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i10354-askari_6_wa_misri_wauawa_katika_mpaka_na_libya
Habari kutoka Cairo, mji mkuu wa Misri zinasema kuwa, kwa akali skari 6 wa jeshi la nchi hiyo wameuawa kwenye makabiliano na kundi la watu wanaofanya magendo ya silaha na mihadarati katika mpaka wa nchi hiyo na Libya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 01, 2016 03:34 UTC
  • Askari 6 wa Misri wauawa katika mpaka na Libya

Habari kutoka Cairo, mji mkuu wa Misri zinasema kuwa, kwa akali skari 6 wa jeshi la nchi hiyo wameuawa kwenye makabiliano na kundi la watu wanaofanya magendo ya silaha na mihadarati katika mpaka wa nchi hiyo na Libya.

Taarifa ya jeshi la Misri imesema kuwa, askari wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika waliokuwa wanashika doria katika eneo la mpakani karibu na eneo la Sinai Kaskazini, walikabiliana na wavamizi hao waliowavizia ghafla na kisha kujiri makabaliano makali ya risasi na hapo ndipo wanajeshi wake 6 waliuawa. Habari zaidi zinasema kuwa, idadi kubwa ya walanguzi hao wa mihadarati na silaha wameuawa katika makabiliano hayo ya jana Alkhamisi. Hata hivyo taarifa ya jeshi la Misri haijabainisha idadi ya wavamizi waliouawa. Magaidi wenye mfungamano na kundi la kitakfiri la Daesh wameshadidisha harakati zao katika eneo la Sinai Kaskazini nchini Misri licha ya askari usalama wa nchi hiyo kunzisha operesheni ya kuliandama kundi hilo. Hivi karibuni, maafisa polisi 18 waliuawa na wengine 7 kujeruhiwa baada ya genge la magaidi kulenga kituo cha ukaguzi cha al-Safaa katika mji wa al Arish huko kusini mwa Sinai Kaskazini. Baadaye Jeshi la Misri lilitoa taarifa na kutangaza kuwa, limefanikiwa kuua magaidi wasiopungua 85 kwenye maeneo ya Sheikh Zuweid na Rafah, katika rasi ya Sinai ya kaskazini mwa nchi hiyo.