Dec 07, 2023 02:53 UTC
  • Kujiondoa Niger na Burkina Faso katika kundi la nchi za Sahel ya Afrika

Nchi mbili za Niger na Burkina Faso zimetangaza kujiondoa katika kundi la nchi za eneo la Sahel ya Afrika kufuatia matukio ya kisiasa katika baadhi ya nchi na kuongezeka tofauti baina ya nchi wanachama wa kundi hilo.

Huku zikiashiria matatizo yanayozikabili nchi za eneo hilo katika kufikia malengo yao, Niger na Burkina Faso, zimesisitiza katika taarifa kuwa, kundi hilo linapinga uhalali wa serikali zao na jitihada za kulifanya eneo hilo kuwa lenya amani na ustawi.

Niger, Burkina Faso na Mali ni nchi tatu ambazo, pamoja na Chad na Mauritania, ziliunda muungano wa kijeshi unaojulikana kama G-5 Sahel Joint Force, kwa himaya ya Ufaransa na kwa shabaha ya kupambana na makundi ya kigaidi katika eneo hilo. Kundi hilo liliasisiwa mwaka 2014 huko Nouakchott, mji mkuu wa Mauritania, kwa lengo la kukabiliana na changamoto za kiusalama na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi.

Kwa hakika kushtadi harakati za makundi mbalimbali ya kigaidi katika eneo la Sahel hususan baada ya kushindwa makundi hayo katika nchi za Asia Magharibi kama vile Iraq na Syria, kumeimarisha nia ya nchi za eneo ya kushirikiana kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za kiusalama na kupambana na ugaidi.

Viongozi wa Kijeshi wa Niger

Ama kutokana na matukio ya mwaka uliopita katika nchi za eneo la Sahel, hasa katika nchi za Niger, Mali na Burkina Faso, na kutoridhishwa baadhi ya nchi na mabadiliko ya kisiasa katika nchi hizo, kivitendo shughuli za pamoja za kikanda zimekabiliwa na matatizo ambayo hivi sasa yamepelekea nchi hizo tatu zichukue maamuzi ya kujiondoa katika kundi la nchi wanachama wa Sahel.

Niger, Mali, na Burkina Faso zimeshuhudia mabadiliko makubwa ya kisiasa katika miaka ya hivi karibuni, kufuatilia kufanyika mapinduzi ya kijeshi katika nchi hizo. Pamoja na hayo tawala za kijeshi katika nchi hizo zina uungaji mkono mkubwa wa wananchi kwa sababu ya kupinga na kuwafukuza wakoloni na mabeberu kama vile Ufaransa katika nchi hizo. Kwa upande mwingine, nchi nyingi za Kiafrika, ambazo bado ziko chini ya ushawishi wa moja kwa moja na usio wa moja kwa moja wa nchi za Ulaya na Marekani, zinatishia kuzishambulia kijeshi nchi za Niger, Mali, na Burkina Faso na kukata uhusiano wa kisiasa; suala ambalo limezifanya nchi hizo kujiondoa katika baadhi ya taasisi na jumuiya za kikanda kama vile Sahel ya Afrika. Gazeti la al-Quds al-Arabi limeandika kuhusiana na suala hilo kwamba taarifa ya pamoja ya Niger na Burkina Faso inaonyesha kuwa, kujitoa nchi mbili hizo katika kundi la Sahel kunatokana na upinzani wao dhidi ya kuwepo uhusiano wowote na Ufaransa, kwa sababu zinaamini kuwa kupitia kundi hilo, Paris imeweza kudhibiti na kuimarisha ushawi wake katika serikali za nchi za eneo hilo kwa kisingizio cha kupambana na makundi ya kigaidi.

Maandamano ya kufukuzwa Ufaransa nchini Niger

Kwa hakika kushadidi harakati za makundi ya kigaidi katika eneo la Sahel katika miaka ya hivi karibuni kumeziandalia nchi za Ulaya hususan Ufaransa uwanja wa kuendelea kuwepo na kujiimarisha kiuchumi na kibiashara katika eneo hilo na bara zima la Afrika.

Hivi sasa, pamoja na matukio ambayo yamepelekea Ufaransa kuondoka katika nchi tatu muhimu za eneo la hilo, na kivitendo kufukuzwa jeshi lake katika eneo hilo, Paris inazitumia baadhi ya nchi hizo kutoa mashinikizo katika uwanja huo.

Hii ni katika hali ambayo nchi za Niger, Mali na Burkina Faso, kabla ya kujiondoa katika jumuiya ya kikanda ya G-5, zilitiana saini mkataba wa pamoja wa kiusalama unaojulikana kama "Muungano wa Nchi za Sahel" kwa lengo la kupambana na ugaidi na kuimarisha ushirikiano wao wa kijeshi na kieneo.

Kuhusiana na suala hilo Asmi Guita, Mkuu wa Baraza la Kijeshi la Mali ametangaza kuwa, nchi hizo tatu zimeunda muungano mpya wa kijeshi kwa lengo la kuimarisha amani na usalama wa pamoja na kuboresha mashauriano kati ya wanachama wake.

Inaonekana kwamba nchi tatu za Niger, Burkina Faso na Mali kwa kubuni jumuia mpya ya kikanda zimedhamiria kuiondoa Ufaransa katika taasisi za kikanda na kuizuia kuingilia masuala ya ndani ya nchi za eneo hilo. Kwa hivyo kujiondoa kwao katika Kundi la G-5 kivitendo kutapelekea kuvunjika kundi hilo.