Jan 27, 2024 11:55 UTC
  • Algeria kuliomba Baraza la Usalama lishinikize kutekelezwa hukumu ya ICJ dhidi ya Israel

Rais Abdelmadjid Tebboune wa Algeria ameitaka Ofisi ya Kudumu ya nchi hiyo ya Kiarabu katika Umoja wa Mataifa iwasilishe ombi la kufanyika mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la umoja huo, wa kujadili namna Israel itashinikizwa kuheshimu kivitendo maamuzi ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ).

Shirika la habari la Anadolu limenukuu taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Algeria inayosema kuwa, nchi hiyo inafuatilia kwa makini maamuzi ya muda ya ICJ yanayoutaka utawala huo unaokalia kwa mabavu wa ardhi ya Palestina, uwasilishe majibu yake ndani ya mwezi mmoja.

Taarifa ya wizara hiyo imebainisha kuwa, Algeria inauchukulia uamuzi wa ICJ kama mwanzo wa mwisho wa enzi za utawala ghasibu wa Israel kutowajibishwa kwa kukanyaga sheria. Ukiukaji huo wa sheria, imesema Wizara ya Mambo ya Nje ya Algeria, umewazidishia masaibu na mbinyo Wapalestina na kuwanyima haki zao halali za taifa.

Kabla ya hapo, Rais wa Algeria alitoa mwito wa kushtakiwa Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) na kusisitiza kwamba, utawala huo ghasibu haujali wala kuheshimu maamuzi ya taasisi muhimu za kimataifa kama Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Algeria ni miongoni mwa mataifa ambayo yamekuwa mstari wa mbele kupaza sauti kuliunga mkono taifa la Palestina na kulaani jinai za Israel dhidi ya wananchi hao madhulumu.

Majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ)

Kadhalika jana jioni, Bunge la Afrika Kusini sambamba na kukaribisha kwa furaha "uamuzi wa kihistoria" wa ICJ, lilitoa mwito kwa jamii ya kimataifa kuushinikiza utawala wa Kizayuni kuheshimu na kutekeleza kivitendo amri ya mahakama hiyo.

Bunge la Afrika Kusini limeitaka Israel kuheshimu amri hiyo ya lazima na kusitisha vitendo vyote vya mauaji ya halaiki huko Gaza na dhidi ya watu wa Palestina. Idadi ya vifo vya Wapalestina kutokana na vita vya mauaji ya kimbari vya jeshi katili la Israel huko Gaza tangu Oktoba 7 imepindikua 26,200.

Viongozi, mataifa na taasisi mbalimbali za kimataifa duniani zimeendelea kupongeza uamuzi wa Ijumaa wa Mahakama ya ICJ wa kuitaka Israel ichukue hatua zote zinazohitajika kuzuia vitendo vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

Tags