Kenya yakanusha ripoti ya UN ya kuua raia 29 Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i10852-kenya_yakanusha_ripoti_ya_un_ya_kuua_raia_29_somalia
Kenya imekanusha vikali ripoti ya Umoja wa Mataifa inayodai kuwa Jeshi la Ulinzi la nchi hiyo KDF liliua raia wapatao 29 katika hujuma ya anga iliyolifanya baada ya wanamgambo wa al-Shabaab kuvamia kambi ya jeshi hilo katika eneo la El-Adde nchini Somalia Januari mwaka huu na kuua idadi kubwa ya askari wa Kenya waliokuwa chini ya kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM).
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 08, 2016 23:51 UTC
  • Kenya yakanusha ripoti ya UN ya kuua raia 29 Somalia

Kenya imekanusha vikali ripoti ya Umoja wa Mataifa inayodai kuwa Jeshi la Ulinzi la nchi hiyo KDF liliua raia wapatao 29 katika hujuma ya anga iliyolifanya baada ya wanamgambo wa al-Shabaab kuvamia kambi ya jeshi hilo katika eneo la El-Adde nchini Somalia Januari mwaka huu na kuua idadi kubwa ya askari wa Kenya waliokuwa chini ya kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM).

Taarifa ya serikali ya Nairobi imesema madai hayo ya mauaji yaliripotiwa na vyombo vya habari vya Somalia bila ya kuwa na ushahidi wowote.

Kenya imekanusha madai hayo siku moja baada ya Ban Ki-moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuliambia Baraza la Usalama la umoja huo kuwa Kenya ilitumia mabomu ya vishada katika hujuma hiyo iliyoonekana kuwa ya kulipiza kisasi na kuua raia 29 pamoja na idadi kubwa ya mifugo, mbali na kusababisha uharibifu mkubwa wa nyumba na visima.

Kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab lilitoa kanda ya video inayoonyesha athari za mashambulizi ya El-Adde, na kudai kuwa liliua wanajeshi zaidi ya 100 wa Kenya katika hujuma hiyo. Hata hivyo msemaji wa jeshi la Kenya, Kanali David Obonyo alipuuzilia mbali idadi hiyo na akisisitiza kuwa wanajeshi kadhaa wa KFD walijeruhiwa katika uvamizi huo. Hadi sasa jeshi la Kenya halijatoa idadi rasmi ya wanajeshi wake waliouawa katika hujuma hiyo ya mwezi Januari mwaka huu.

Kenya inachangia wanajeshi 4,000 kwenye kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM). Kikosi hicho kina wanajeshi 22,000 kutoka nchi mbalimbali za Afrika.